LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu machachari Mercy Johnson wa Nigeria ndiye anayeongoza kwa utajiri kwa sasa miongoni mwa wacheza filamu wa kike nchini humo.
Mercy, mzaliwa wa kitongoji cha Igbira kilichoko katika Jimbo la Kogi, ndiye mwigizaji anayecheza filamu nyingi kuliko wanawake wenzake wa Nollywood.
Uchunguzi uliofanywa na mtandao wa YES International, umebaini kuwa, Mercy amekuwa akilipwa kati ya Naira milioni 1.5 hadi Naira milioni mbili kwa filamu moja.
Kwa mujibu wa mtandao huo, haipiti mwezi bila kumuona Mercy akicheza filamu zisizopungua mbili katika mwezi mmoja na hivyo kuwa mwigizaji aliye bize kuliko wenzake.
Uchunguzi wa mtandao huo pia umebaini kuwa, watayarishaji wa filamu nchini Nigeria wamekuwa wakiandaa filamu zao huku wakipanga jinsi ya kumshirikisha na hivyo kumuongezea sifa, umaarufu na utajiri.
"Hali imekuwa hivyo kwa muda mrefu sasa. Hata alipokuwa na uja uzito, alikuwa akifanyakazi bila kusimama, ikiwa ni pamoja na kwenda kupiga picha za filamu nchini Marekani akiwa na tumbo kubwa," umeripoti mtandao huo.
Baadhi ya filamu za hivi karibuni, ambazo zimemfanya mwanadada huyo mwenye mtoto mmoja awe tajiri na maarufu ni pamoja na Obioma The Slave Girl, Sleeping Walker, Heart of A Twin 1 & 2, Mud of Hardship, Dumebi and Bitterleaf Cyhtia, There are also Daniella, First Experience na Endless Agony.
Zingine ni Immaculate Heart, Painful Soul, Tears of Madness, Weeping Kingdom, Troubled King, Baby Oku in America, Dumebi in School, Somma The Local Champion, Ebute The Only Girl, Leave My Tears 1 & 2, Mary The Hunter, Cry of A Widow na Voice of A Mother.
Kutokana na utajiri alionao sasa, Mercy amewapiku wacheza filamu wengine nyota wa Nigeria kama vile Genevieve Nnaji, Patience Ozokwor 'Mama G', Omotola Jalade na Ini Edo.
Mercy amefunga ndoa na Odianosen Okojie, ambaye wamezaa mtoto mmoja wa kike, anayeitwa
Purity. Mercy ni mtoto wa nne katika familia yenye watoto saba.
Alizaliwa Agosti 28, 1984. Alijitosa kwenye fani ya filamu kutokana na kuvutiwa na Genevieve. Filamu yake ya kwanza ilimwingizia Naira 50,000.
No comments:
Post a Comment