KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, February 7, 2014

OKWI, CHUJI KUWAKOSA WACOMORO


UONGOZI wa klabu ya Yanga, umesema hauna uwezo wa kumtumia mshambuliaji, Emmanuel Okwi, licha ya Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), kutoa leseni ya kucheza michuano ya klabu bingwa mwaka huu.

Akizungumza jana na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya klabu hiyo mjini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema hadi jana walikuwa wakifuatilia kwenye mtandao wa CAF kuona iwapo kuna pingamizi lolote kwa mchezaji huyo.

Yanga inatarajiwa kushuka dimbani keshokutwa kumenyana na Komorozine de Domoni kutoka Comoro katika mechi ya awali ya michuano ya klabu bingwa Afrika itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kizuguto, alisema kwenye mfumo wa usajili wa Okwi, wamegundua hakuna dosari yoyote kwa vile walifuata taratibu zote, ikiwemo kuzungumza na mchezaji na kisha klabu ya Villa ya Uganda, ambayo imetoa ruhusa ya kusajiliwa kwa mchezaji huyo.

Hata hivyo, Kizuguto alisema wanaendelea kusubiri taarifa kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kama litatoa baraka zake kwa mchezaji huyo kuichezea Yanga katika michuano hiyo na ligi kuu msimu huu.

Okwi alisajiliwa na Yanga mwaka jana kutoka SC Villa baada ya kugoma kuendelea kuichezea Etoile du Sahel ya Tunisia, iliyomsajili kwa mkataba wa miaka minne kuanzia Januari mwaka juzi kutoka Simba SC ya Tanzania.

Nyota huyo wa Uganda, alifungua kesi Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), akilalamika kutolipwa mishahara ya miezi mitatu na Etoile, ndipo akaruhusiwa kujiunga na SC Villa ya Uganda, ambayo baadae ilimuuza kwa Yanga.

Hata hivyo, baada ya Villa kumuuza Yanga ikidai ina haki zote, TFF imeandika barua FIFA kutaka ufafanuzi kama inaweza kumuidhinisha Mganda huyo kucheza timu ya Jangwani na wakati huo huo imeizuia klabu hiyo kumtumia hadi majibu yapatikane.

Hadi sasa Etoile haijailipa Simba SC dola za Marekani 300,000 za manunuzi ya mchezaji huyo na Wekundu hao wa Msimbazi nao wamefungua kesi FIFA.    

"Sheria inasema kabla ya kumsajili mchezaji inabidi mkubaliane, tulifanya hivyo na kisha tukazungumza na viongozi wa Villa na kisha tukatuma jina na mambo muhimu CAF, usajili wake umekamilika, kama kungekuwa na pingamizi tusingeweza kupata system na password," alisema Kizuguto.

Amesema baada ya kipindi cha pingamizi kupita, Okwi aliwekewa pingamizi baada ya siku 37 kwenye Shirikisho la Soka nchini, kitu ambacho nina imani CAF hawana taarifa nacho.

Kauli ya kiongozi huyo, imekuja siku chache baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, kusimamisha usajili wa mshambuliaji huyo Yanga hadi FIFA itakapotoa ufafanuzi.

Shirikisho hilo, limechukua uamuzi huo, baada ya kubaini kuwa Okwi, aliruhusiwa kuichezea SC Villa ya Uganda kwa kibali maalumu cha miezi sita kutoka FIFA.

FIFA inazo kesi tatu mkononi za mchezaji huyo, ikiwemo ya kuishitaki Etoile  kwa kutomlipa mshahara wakati Etoile nayo imemshitaki mchezaji huyo kwa utoro.
Simba nayo imeishitaki Etoile wa kushindwa kuilipa ada ya mauzo ya mchezaji huyo ambayo ni dola za Marekani 300,000 (sh. milioni 480).

ATHUMAN IDD 'CHUJI'
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, amesema kiungo wao mahiri, Athuman Idd 'Chuji' ataukosa mchezo wa keshokutwa dhidi ya Wacomoro kutokana na kukabiliwa na adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa katika mchezo kati ya Yanga na Zamalek ya Misri.

Kizuguto alisema jana kuwa, wamepokea taarifa kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika(CAF), likiwakumbusha kuacha kumtumia nyota huyo kwenye mchezo huo kwa vile alipewa kadi nyekundu.

Yanga ilishiriki na kutolewa raundi ya kwanza katika michuano ya klabu bingwa Afrika
mwaka 2012 baada ya kufungwa na Zamalek ya Misri. Katika mechi ya kwanza,
walilazimishwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na katika mechi ya marudiano walifungwa bao 1 – 0 mjini  Cairo.

SEIF AHMED'MAGARI'
Mwenyekiti wa mashindano ya kimataifa wa klabu ya Yanga, Seif Ahmed 'Magari', amesema wana imani na kikosi chao dhidi ya Komorozine de Domoni.

Magari alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, tayari wameshagawa kazi kwa kamati yake, ambapo wakimaliza mchezo wa marudiano, watahakikisha wanaanza kuifuatilia timu ya Al Ahly ya Misri ili kujua mbinu zao zote.

Kiongozi huyo alisema wamejipanga kuweka historia barani Afrika mwaka huu kwa vile kikosi chao kimekamilika kila idara baada ya kufanya usajili kwa umakini mkubwa.

Ameongeza kuwa, lengo lao ni kuona Yanga inavuka vikwazo vya timu za Misri na kusonga mbele katika michuano hiyo.

"Tunajua wazi kwamba waarabu wanajua mbinu za kusaka ushindi nje ya mchezo, lakini tutatuma watu kufahamu mbinu zao na mahali ambapo Yanga ikienda Misri itafikia,"alisema.

WAAMUZI
Shirikisho la Soka Barani Afrika( CAF), limeteua waamuzi kutoka Somalia kuchezesha mechi kati ya Yanga na Wacomoro itakayofanyika keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwamuzi wa kati atakuwa Hassan Mohamed Hagi wakati wasaidizi wake ni Hamza Hagi Abdi, Bashir Abdi Suleiman na Bashir Olab Arab. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Eugene Musoke kutoka Uganda.

VIINGILIO
Uongozi wa Yanga umetangaza viingilio vya mechi ya klabu bingwa Afrika itakayoikutanisha Yanga na Comorozine de Domoni ya Comoro, ambapo kiingilio cha chini kitakuwa sh. 5,000.

Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kiingilio cha juu katika mechi hiyo ni VIP A sh.30,000, VIP B na C Sh. 20,000, viti vya rangi ya chungwa sh. 10,000 na viti vya kijani sh.5,000.

Alisema Klabu ya Yanga imetengeneza tiketi 45,000 ambapo katika VIP A kuna tiketi 500, VIP B na C tiketi 4,500, viti vya rangi ya chungwa tiketi 7,000 na viti vya kijani tiketi 33,000.

Alisema tiketi hizo, zitapatikana katika vituo 10 ikiwemo makao makuu ya klabu hiyo Jangwani, Olicom Buguruni, Stears, Oilcom Ubungo, Kimara Mwisho, Uwanja wa Uhuru, Shule ya Benjamin Mkapa pamoja na Uwanja wa Taifa.
 
Tiketi hizo, zitaanza kuuzwa kesho asubuhi na siku ya mchezo, ambapo zitapatikana mpaka saa tano asubuhi.Kizuguto amewataka mashabiki wa Yanga kufika kwa wingi uwanjani kuishangilia timu hiyo ambayo mechi hiyo itakuwa muhimu kushinda.

No comments:

Post a Comment