KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, February 16, 2014

TAIFA STARS KUWEKA KAMBI UHOLANZI





SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeanza rasmi mikakati ya kuiwezesha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kufuzu kwa Fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani baada ya kupanga mpango wa timu hiyo kuweka kambi nchini Uholanzi.

Kambi hiyo itakuwa ni maalumu kwa timu hiyo kuweza kujiandaa na hatua ya kufuzu kwa fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Morocco na kushirikisha jumla ya mataifa 16 yatakayofuzu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesema endapo Stars itafanikiwa kupita katika hatua ya awali ya mchujo ikiwa itapangwa kwenye hatua hiyo, wamepanga kuweka kambi nchini Uholanzi ya timu hiyo, ili kujiandaa na hatua ya pili ya makundi.

Malinzi alisema wameamua kufanya hivyo ili kurudia historia ya mwaka 1980 ya Stars kufuzu kwa mara ya mwisho michuano ya AFCON, iliyofanyika nchini Nigeria, ambapo Stars iliweka kambi Uholanzi mwaka 1979 na kufanikiwa kufuzu kwa fainali hizo.

“Tumepokea barua ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) inayotueleza kuwa mechi zetu za mchujo zitaanza kati ya mwezi Mei hadi Agosti kutokana na kiwango chetu kuwa chini ya nchi 21 bora za bara hili, hivyo muda si mrefu tunafikiria kurekebisha benchi lote la ufundi kwa pamoja na kuanza mikakati ya timu hiyo.

“Huenda timu yetu ikaanzia hatua ya mchujo kama CAF walivyotuandikia, ikifanikiwa kufuzu katika hatua ya makundi ttumepanga kuweka kambi nje ya nchi katika nchi ya Uholanzi, na huko timu itapata mafunzo ya kisasa ili kufanya vizuri kwenye hatua ya makundi,” alisema Malinzi.

Katika hatua nyingine alisema kwa sasa wameshazungumza na Balozi wa Uholanzi hapa nchini kwa ajili ya mipango yao hiyo, pia wamewataarifu wadhamini wakuu wa Stars, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chao cha Kilimanjaro Premier Lager ili kuandaa bajeti ya ziara hiyo.

No comments:

Post a Comment