KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, March 17, 2014

RONALDO AOKOA MAISHA YA MTOTO


 


MADRID, Hispania
MWANASOKA bora wa dunia, Cristiano Ronaldo amedhihirisha kuwa ni mtu mwenye huruma baada ya kujitolea kulipa gharama za upasuaji wa mtoto mwenye umri wa miaka 10.

Mtoto huyo, Erik Ortiz Cruz, anasumbuliwa na matatizo mbalimbali ya kiafya na upasuaji ndio pekee utakaoweza kunusuru maisha yake.

Familia ya mtoto huyo imeshindwa kumudu gharama za matibabu ya mtoto huyo hospitali, ambapo gharama za kila kipimo ni pauni 5,020 za Uingereza na upasuaji ni pauni 50,240.

Kutokana na hali hiyo, Ronaldo ameguswa na jitihada zinazofanywa na familia hiyo kwa ajili ya kukusanya fedha za kulipia matibabu ya mtoto huyo na kuamua kubeba mzigo huo.

Awali, Ronaldo aliombwa kuchangia viatu na fulana ili vipigwe mnada kwa ajili ya kuchangia fedha za matibabu hayo, lakini aliamua kwenda mbali zaidi kwa kulipa gharama hizo.

Mapema mwaka huu, Ronaldo alisherehekea tuzo ya kuwa mwanasoka bora duniani na watoto wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kansa, akitekeleza ahadi aliyoitoa mwaka jana alipohojiwa na kituo cha redio cha Hispania.

Ronaldo alikutana na watoto hao wakati wa kipindi cha redio hiyo cha Partido de la 12 Novemba mwaka jana na kusema, iwapo atashinda tuzo hiyo, atasherehekea nao.

UCHAGUZI MKUU SIMBA MEI 4


UCHAGUZI mkuu wa klabu ya Simba umepangwa kufanyika Mei mwaka huu mjini Dar es Salaam.

Uamuzi wa kupanga tarehe hiyo ulifikiwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya Simba kilichofanyika mjini Dar es Salaam juzi chini ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage.

Katika kikao hicho, kamati hiyo pia ilifanya uteuzi wa wajumbe wa kamati ya kusimamia uchaguzi huo itakayoongozwa na mwanasheria, Damas Ndumbaro.

Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo ni Salum Madenge, katibu ni Issa Batenga, katibu msaidizi ni Khalid Kamguna. Wajumbe wengine ni Kassim Dewji, Juma Simba na Amin Bakhressa.

YANGA, MTIBWA HAKUNA MBABE, AZAM YAIGAGADUA COASTAL UNION


NA FRED MAJALIWA, MOROGORO
MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga jana walishindwa kuonyesha makeke yao mbele ya Mtibwa Sugar, baada ya kulazimishwa kutoka nayo suluhu katika mechi kali na ya kusisimua iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Yanga tangu iliporejea nchini Jumatatu iliyopita kutoka Misri baada ya kutolewa na Al Ahly katika raundi ya pili ya michuano ya klabu bingwa Afrika.

Sare hiyo imeiwezesha Yanga kurejea nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kati yake na Mbeya City, ambayo imeshuka nafasi ya tatu.

Yanga inazo pointi 39 baada ya kucheza mechi 18 sawa na Mbeya City yenye idadi hiyo ya pointi baada ya kucheza mechi 21. Yanga imefunga mabao 41 na kufungwa 12 wakati Mbeya City imefunga mabao 27 na kufungwa 17.

Washindi wa pili wa ligi hiyo, Azam wameendelea kujichimbia kileleni mwa ligi hiyo baada ya kuichapa Coastal Union mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Chamazi ulioko Mbagala, Dar es Salaam. Ushindi huo umeiwezesha Azam kuwa na pointi 43 baada ya kucheza mechi 19.

Yanga ililianza pambano hilo kwa kasi na kulifikia lango la Mtibwa dakika ya kwanza wakati Emmanuel Okwi alipopiga mpira kichwa ukatumbukia ndani ya eneo la hatari na kumkuta Nizar Khalfan, lakini shuti lake lilimlenga kipa Hussein Sharrif.

Katika dakika ya nane na tisa, Mtibwa ilifanya mashambulizi makali kwenye lango la Yanga huku ikishangiliwa na mashabiki wa Simba na kupata kona mbili, lakini hazikuweza kuzaa matunda.

Kiungo Shaaban Nditi alikuwa nyota ya mchezo kwa Mtibwa katika dakika za mwanzo za pambano hilo kutokana na kutawala dimba la kati huku akirudi nyuma kusaidia kuokoa mashambulizi.

Okwi nusura aipatie bao Yanga dakika ya 20 alipounganisha kwa kichwa krosi kutoka pembeni ya uwanja, lakini mpira ulikwenda moja kwa moja mikononi mwa kipa Sharrir.

Dakika moja baadaye, Okwi na Didier Kavumbagu walijichanganya ndani ya eneo la hatari la Mtibwa wakiwa wamebaki ana kwa ana na kipa Sharrif, Okwi akapiga shuti dhaifu lililodakwa na kipa huyo.

Mtibwa ilipata nafasi nzuri dakika ya 26 baada ya mwamuzi Zakaria Jacob kutoka Pwani kuamuru ipigwe adhabu ndogo nje kidogo ya eneo la hatari la Yanga baada ya beki Juma Abdul kucheza rafu, lakini shuti la Shabani Kisiga liliokolewa na kipa Juma Kaseja.

Kipa Sharrif wa Mtibwa alilazimika kufanyakazi ya ziada dakika ya 38 kuokoa mpira mrefu kwa kichwa na kutua kwa Okwi wa Yanga, aliyekuwa akijiandaa kufunga, lakini akaukosa.

Lango la Yanga lilikuwa kwenye kimbembe dakika ya 43 na 45, lakini mabeki wake wakiongozwa na Kelvin Yondan na Nadir Haroub, walisimama imara kuondosha hatari hizo. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.

Kipindi cha pili kilianza kwa kosi kwa Mtibwa baada ya mshambuliaji wake, Abdalla Juma kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Jacob kwa kosa la kumpiga kichwa beki Yondan wa Yanga.

Didier Kavumbagu aliikosesha Yanga bao dakika ya 71 baada ya kushindwa kuunganisha wavuni krosi maridadi iliyopigwa na Okwi kutoka pembeni ya uwanja.

Dakika 10 baadaye, Kavumbagu alishindwa kuukwamisha mpira wavuni baada ya kupenyezewa pasi akiwa ndani ya eneo la hatari huku kipa Sharrif akiwa ametoka langoni. Shuti lake lilipaa juu ya langu.

Hussein Javu, aliyeingia kipindi cha pili badala ya Hamisi Kiiza, angeweza kufunga bao dakika ya 83 alipopewa pasi akiwa nje kidogo ya eneo la hatari, lakini shuti lake lilitoka pembeni ya lango.

Yanga itabidi waijutie nafasi waliyoipata dakika ya 91 baada ya Okwi kuingia na mpira ndani ya 18, lakini shuti lake liligonga mwamba wa goli na mpira kurudi uwanjani, ambako uliokolewa na mabeki wa Mtibwa.

Yanga: Juma Kaseja, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondan, Nadir Haroub, Frank Domayo, Simon Msuva, Nizar Khalfan, Hassan Dilunga, Emmanuel Okwi, Didier Kavumbagu, Hamisi Kiiza/Hussein Javu.

Mtibwa: Hussein Sharrif, Hassan Ramadhani, Paulo Ngelema, Dickson Daudi, Salum Mbonde, Shaabani Nditi, Ally Shomari/Saidi Mkopi, Abdalla Juma, Mohamed Mkopi na Vicent Barnabas/Jamal Mnyate.

Wakati huo huo, mabao yaliyofungwa na Kipre Tcheche na John Bocco jana yaliiwezesha Azam kuinyuka Coastal Union mabao 4-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi.

Tchetche alifunga bao la kwanza dakika ya 23 kabla ya kuongeza la pili dakika ya 38. Bao la tatu lilifungwa na John Bocco dakika ya 64 wakati la nne lilifungwa na Kevin Friday dakika ya 90.

Saturday, March 15, 2014

BALE: HAKUNA KAMA RONALDO



 
MADRID, Hispania
MSHAMBULIAJI Gareth Bale amemwelezea nyota mwenzake wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, kuwa ndiye mchezaji bora duniani kwa sasa na ataiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa Hispania msimu huu.

Licha ya Lionel Messi kuonyesha kiwango cha juu wakati Barcelona ilipomenyana na Manchester City katika mechi ya ligi ya mabingwa wa Ulaya Jumatano iliyopita, Bale amesema ana hakika Ronaldo yupo kwenye kiwango bora zaidi.

"Cristiano ni mchezaji bora duniani kwa sasa na sote tunaelewa jinsi alivyo mzuri,"amesema Bale.

"Huwa inanisaidia sana ninapocheza safu ya ushambuliaji pamoja na Ronaldo na natumaini tutacheza vizuri zaidi na kushinda taji hili msimu huu,"ameongeza.

Bale alikuwa akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa viatu vyake vipya vya Adidas F50 iliyofanyika mjini hapa.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Tottenham ya England alishindwa kujizuia kuzungumzia mafanikio, ambayo Real Madrid inaweza kuyapata mwishoni mwa msimu huu.

Madrid inatarajiwa kumenyana na Barcelona, Machi 23 mwaka huu katika mechi ya ligi ya Hispania, inayotarajiwa kuwa na ushindani mkali na wa aina yake.

"Kuna mechi za kufurahisha kwa mchezaji yeyote. Tuna hamu ya kupambana nao, na kama inawezekana kuwafunga. Mechi ijayo tutacheza dhidi ya Malaga, hivyo tumeelekeza nguvu zetu katika mechi hizo kwa sasa,"alisema Bale.

Nyota huyo wa Real Madrid amesema, lengo la Madrid msimu huu ni kutwaa mataji yote matatu wanayoshindania na kwamba wanayo nafasi kubwa ya kufanya hivyo, lakini wanapaswa kwenda hatua kwa hatua.

Kwa sasa, Madrid inaongoza ligi ya Hispania kwa tofauti ya pointi tatu na Atletico Madrid, inayoshika nafasi ya pili. Timu zote mbili zimesaliwa na michezo 11. Madrid inaongoza kwa kuwa na pointi 67, Atletico inazo pointi 64 wakati Barcelona ni ya tatu ikiwa na pointi 63.

"Ni kweli kwamba tupo kwenye nafasi nzuri,"alisema Bale. "Kama tutaendelea kufanya kazi nzuri na kushinda, hatuna sababu ya kuwa wasiwasi kuhusu timu zingine na tunaweza kutimiza malengo yetu, ambayo ni kutwaa ubingwa wa ligi,"amesema Bale.

Nyota huyo wa Madrid amesema, kwa kipindi cha miezi sita alichoichezea timu hiyo, amekuwa akivutiwa na mbinu za hali ya juu za kisoka katika ligi ya Hispania.

Madrid inatarajiwa kushuka dimbani Alhamisi ijayo kukipiga na Schalke ya Ujerumani katika mechi ya marudiano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya baada ya kuibwaga timu hiyo kwa mabao 6-1. Mabao ya Madrid yalifungwa na Bale, Ronaldo na Karim Benzema, kila mmoja akitupia mawili.

Bale amesema wanayo nafasi nzuri ya kutwaa taji hilo la Ulaya iwapo watavuka hatua za awali na kuwa na bahati.

"Kwa sasa bado zipo timu ngumu katika ligi ya mabingwa. Sidhani kama ipo inayopewa nafasi kubwa zaidi kuliko zingine,"alisema.

'NAPENDA KUOLEWA NA MWANAUME TAJIRI'


LAGOS, Nigeria
MCHEZA sinema mwenye mvuto nchini Nigeria, Lizzy Gold Onuwaje amesema kamwe hawezi kuolewa na mwanaume masikini.

Lizzy, ambaye alitwaa taji la mrembo wa Jimbo la Delta 2006, amesema anapenda kuolewa na mwanaume tajiri na mwenye uwezo mkubwa kipesa.

Mrembo huyo wa filamu, alisema hayo wiki hii alipohojiwa na gazeti la Vanguard la Nigeria.

"Napenda wanaume, ambao wapo tayari kutumia pesa na sio wanaume bahiri,"alisema mrembo huyo mwenye tabasamu mwanana.

"Uhusiano wa kimapenzi kati yangu na mpenzi wangu wa zamani, haukuvunjika kwa sababu ya mimi kuamua kuwa mwigizaji Ukweli ni kwamba hakuwa na pesa, hivyo nikaamua kuachana naye,"alisema mrembo huyo.

"Niliachana naye mwaka jana kwa sababu hakuwa na pesa au kitu chochote, ambacho kingeweza kumuingizia pesa,"aliongeza.

"Napenda mwanaume anayejali. Unapaswa kuwa tajiri, mzuri, unayejali na mwenye mapenzi ya kweli. Baadhi ya wanaume ni matajiri, lakini mabahiri. Kuwa tajiri na uwe tayari kutumia pesa. Iwapo nitakwambia nahitaji kitu chochote, acha nipate ishara. Napenda ishara,"alisema.

Lizzy alisema mwanaume asiye na pesa, asijisumbue kumpigia simu ana kuzipenda picha zake. Alisema anapenda mno pesa na kusisitiza kwamba, kamwe hawezi kuolewa na mwanaume masikini.

"Nahitaji mwanaume tajiri. Pesa zina maana kubwa kwangu. Fedha zinanipa uhai,"alisema mwanadada huyo huku akiangua kicheko.

Lizzy alikwenda mbali zaidi kwa kusema, mwanaume asiye na utajiri, kamwe hawezi kuwa na mvuto kwake.

"Ninaposema tajiri, sina maana ya wanaume aina ya 'Yahoo' kwa sababu sio wachapakazi. Nataka mwanaume, ambaye ni mchapakazi na tajiri. Kwa sasa nimeridhika na mwanaume niliyenayo na sifikirii kuachana naye kwa ajili ya mwanaume mwingine,"aliongeza msisitizo.

SIWEZI KUACHA UIGIZAJI ILI NIOLEWE-ANITA


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu mwenye vituko nchini Nigeria, Anita Joseph, ameamua kuachana na mumewe mtarajiwa, baada ya kumtaka aachane na kazi ya uigizaji.

Anita na mchumba wake huyo, walitarajia kufunga ndoa hivi karibuni, lakini masharti ya mwanaume huyo yalimfanya mwanadada huyo aione ndoa kuwa chungu.

Kuvunjika kwa uchumba wa wapenzi hao, kumezua maswali mengi kuhusu sababu ya kutengana kwao na Anita ameamua kuweka wazi ukweli wa mambo ili kusafisha hali ya hewa.

"Nilikataa ombi lake la kutaka kufunga ndoa na mimi kwa sababu siwezi kuwa mwanamke wa kukaa ndani. Alitaka niache kazi ya uigizaji na kuwa mwanamke wa ndani muda wote,"alisema Anina.

"Mimi si mwanamke wa aina hiyo wa kukaa nyumbani siku nzima. Napenda kufanyakazi. Napenda kuwa bize muda wote,"alisisitiza.

Anita alisema alianza kufahamiana na kijana huyo miaka miwili iliyopita kabla ya kuanzisha naye uhusiano wa kimapenzi uliodumu kwa mwaka mmoja.

"Sitaki kumtambulisha majina yake. Ninachoweza kusema ni kwamba, jina lake ni M. Ni kijana mzuri, lakini anaweza kukudhuru anapopatwa na wivu. Ananielewa nilivyo,"alisema Anita.

Kwa mujibu wa Anita, kijana huyo aliwahi kumuona kwenye televisheni kabla ya kukutana naye na tangu wakati huo, alianza kufuatilia filamu zake.

"Hataki kuniunga mkono katika kazi yangu.Anataka niachane na kazi hiyo baada ya kufunga naye ndoa,"alisema Anita.

"Hataki nitoke nje. Hapendi nijihusishe na filamu za mapenzi. Hataki watu wanitazame na mimi nionekane kwenye filamu za mapenzi. Ninalo wazo la kuolewa, lakini sina haraka ya kufanya hivyo," alisisitiza nyota huyo.

DORIS: NITAKWENDA KOKOTE MUNGU ATAKAKONIONGOZA



LAGOS, Nigeria
IMEPITA miaka miwili tangu ndoa ya mchezaji filamu nyota wa Nigeria, Doris Simon na mumewe, Daniel Ademinokan, ilipovunjika. Tangu wakati huo, Doris ameamua kuishi pweke, japokuwa mtoto wake wa kiume waliyezaa, Daniel anaishi na mzazi mwenzake.

Akihojiwa na mtandao mmoja wa habari nchini Nigeria hivi karibuni, Doris alizungumzia mambo mbalimbali kuhusu kuvunjika kwa ndoa yake.

"Chochote kingeweza kwenda mrama. Chochote kingeweza kusababisha moto mahala kokote. Huwezi kujua nini kinaweza kutokea dakika moja ijayo. Tunajaribu kuweka mambo sawa, lakini Mungu ndiye mwenye uamuzi wa mwisho,"amesema Doris.

"Ni kweli, mambo mengi hutokea maishani na unaweza kuendelea kujiuliza maswali mengi kuhusu kilichotokea na kusababisha jahazi liende mrama. Kama utaendelea kuwa katika hali hiyo, huwezi kusonga mbele kwa sababu kila kitu kinachotokea, Mungu ameweka mkono wake. Kuna sababu kwa nini mambo yanakuwa hivi na imeandikwa kwamba itatokea hivyo,"aliongeza

Doris amesema tangu ndoa yake ilipovunjika, amekuwa akiulizwa maswali mengi. "Watu wananiuliza, 'Doris unadhani utaendeleaje na maisha yako? Utafanya nini ili kusonga mbele'"

"Nimeamua kuyapuuza maswali hayo na kusonga mbele. Ningejikita kujibu maswali hayo, ningechanganyikiwa na kupandwa na hasira,"alisema.

"Wapo watu waliokuwa wakitaka kunicheka, hivyo niliona ni vyema niwaache wabaki na mshangao. Ndio sababu nimeamua kusonga mbele na maisha yangu,"alisisitiza mwanadada huyo mwenye umbo na sura jamali.

Alipoulizwa iwapo atafikiria kuolewa tena, Doria alisema: "Siwezi kuelewa. Lakini siwezi kusema lolote kwa sababu mimi ni binadamu. Ninaweza kujitosa katika penzi jingine. Lakini kwa sasa acha nifanye kile ninachoendelea kukifanya. Popote ambako Mungu ataniongoza, nitakwenda."

MWANAMITINDO AMPASUA KICHWA NYOTA WA ARSENAL




LONDON, England
HATIMAYE mshambuliaji, Olivier Giroud wa klabu ya Arsenal ameamua kuvunja ukimya kwa kujibu tuhuma za kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamitindo, Celia Kay.

Giroud anatuhumiwa kumpeleka Kay kwenye hoteli ya Four Seasons iliyoko Canary Wharf siku moja kabla ya Arsenal kuichapa Crystal Palace katika mechi ya ligi kuu ya England iliyochezwa Februari 2 mwaka huu.

Kocha Mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger, hadi sasa hajaamua kuweka wazi kuhusu hatua zitakazochukuliwa kwa Giroud baada ya kukiri kufanya mapenzi na binti huyo wakati akiwa katika majukumu ya kuitumikia timu yake.

Wenger alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa, suala la mchezaji huyo ni la ndani na litashughulikiwa na uongozi wa klabu.

"Hili ni suala la ndani, sitaki kulizungumza hadharani kwa sababu naheshimu maisha yake binafsi,"alisema Wenger.

Kay alimpiga picha Giroud alipokuwa kwenye chumba cha hoteli hiyo, akiwa amevaa chupi ya ndani na kuisambaza kwenye mitandao, ukiwemo mtandao wa MailOnline.

Awali Giroud, ambaye aliifungia Arsenal mabao mawili ilipoichapa Everton mabao 4-1 katika mechi ya Kombe la FA iliyochezwa wiki iliyopita, alitoa taarifa ya kuomba msamaha kwa mkewe, Jennifer na Wenger.

"Naomba radhi kwa mke wangu, familia yangu, marafiki, kocha, wachezaji wenzangu na mashabiki,"alisema Giroud.

"Napaswa kuipigania familia na klabu yangu na kuomba radhi kwao," alisema mshambuliaji huyo.

"Kuna mambo yaliyokuwa na ukweli, lakini mengine yalikuwa ya uongo. Lakini hayo yamepita kwa sasa,"alisema nyota huyo wa Arsenal, ambaye Juni mwaka jana mkewe alijifungua mtoto wa kiume.

"Kitu ambacho hakiwezi kuniua, kinanifanya niwe jasiri. Nashawishika kuamini kwamba, kina kinachotokea kwangu, kitanifanya niwe na nguvu zaidi,"aliongeza.

Giroud alisema anachopaswa kukifanya kwa sasa ni kuelekeza nguvu na akili yake uwanjani kwa kuitumikia vyema klabu yake na kutunza familia yake.

"Kilikuwa kipindi kigumu. Unapaswa kuwa na ujasiri kichwani kwako. Nilitumia mchezo wa soka kupambana na hili. Mchango wa Kocha Arsene Wenger ulikuwa muhimu. Nilizungumza naye.

"Nataka kusahau kuhusu hili kwa sasa na kuendelea na mambo mengine na kuanza upya,"alisisitiza.
Arsenal ilipanga kumtoza faini ya pauni 230,000 mchezaji huyo, lakini baadaye iliamua kumuunga mkono baada ya kukanusha tuhuma hizo. Wanasheria wa mchezaji huyo nao wameliandikia barua gazeti la Daily Mail kulilaumu kwa kuandika habari hizo.

SEMINA YA WAAMUZI DAR YAANZA


Semina ya siku mbili kwa waamuzi wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na wale wa ngazi ya juu nchini (elite) kwa robo ya kwanza ya mwaka huu inaanza leo (Machi 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Waamuzi na waamuzi wasaidizi 22 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanashiriki katika semina hiyo ambayo pia itahusisha mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test), na itamalizika keshokutwa (Machi 16 mwaka huu).
Baadhi ya waamuzi hao ni Charles Simon kutoka Dodoma, Dalila Jafari (Zanzibar), Ferdinand Chacha (Mwanza), Hamis Chang’walu (Dar es Salaam), Helen Mduma (Dar es Salaam), Israel Mujuni (Dar es Salaam), Issa Vuai (Zanzibar), Janeth Balama (Iringa) na Jesse Erasmo (Morogoro).
John Kanyenye (Mbeya), Jonesia Rukyaa (Bukoba), Josephat Bulali (Zanzibar), Lulu Mushi (Dar es Salaam), Martin Saanya (Morogoro), Mfaume Nassoro (Zanzibar), Mohamed Mkono (Tanga), Mwanahija Makame (Zanzibar), Ngaza Kinduli (Zanzibar), Ramadhan Ibada (Zanzibar) na Waziri Sheha (Zanzibar).

WATANZANIA WATANO WAPATA UKAMISHNA WA CAF

Watanzania watano wameteuliwa kuingia kwenye jopo la makamishna watakaosimamia mechi mbalimbali za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa mwaka 2014 hadi 2016.

Kwa mujibu wa orodha iliyotumwa na CAF kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Watanzania hao ni Alfred Kishongole Rwiza wa Mwanza na Hafidh Ali Tahir wa Zanzibar ambao wamerejeshwa tena kwenye jopo hilo.

Rwiza na Tahir ambao ni waamuzi wastaafu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na wakufunzi wa uamuzi walikuwepo kwenye jopo lililopita la 2012 hadi 2014.

Makamishna wapya kwa upande wa wanawake ni Elizabeth Mwanguku Kalinga wa Mbeya na Isabellah Hussein Kapera wa Dar es Salaam. Kamishna mwingine mpya kwa upande wa wanaume ni Muhsin Ali Rajab kutoka Zanzibar.

Wakati huo huo, CAF imeandaa semina kwa makamishna wanaume itakayofanyika jijini Cairo, Misri kuanzia Aprili 3 hadi 4 mwaka huu.

Watoa mada kwenye semina hiyo ya siku mbili ni Katibu Mkuu wa CAF, Hicham El Amrani, Mkurugenzi wa Mashindano wa CAF, Shereen Arafa na Naibu Mkurugenzi wa Mashindano wa CAF, Khaled Nassar.

Wengine ni Meneja wa Waamuzi wa CAF, Eddy Maillet, Mkurugenzi wa Habari wa CAF, Junior Binyam, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Mawasiliano wa CAF, Tarek el Deeb na Mkurugenzi wa Masoko na Televisheni wa CAF, Amr Shaheen

Friday, March 14, 2014

NGASA, NIYONZIMA KUIKOSA MTIBWA LEO



MSHAMBULIAJI Mrisho Ngassa na kiungo Haruna Niyonzima wa Yanga, wataikosa mechi ya leo ya ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, Ngasa na Niyonzima wataikosa mechi hiyo kutokana na kuwa majeruhi.

Yanga inatarajiwa kushuka dimbani leo kukipiga na Mtibwa Sugar katika mechi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Mabingwa hao watetezi wa Tanzania Bara, walirejea nchini jana saa 12 asubuhi wakitokea Cairo, Misri, ambako walikwenda kurudiana na Al Ahly katika mechi ya raundi ya pili ya michuano ya klabu bingwa Afrika.

Katika mechi hiyo iliyochezwa mjini Alexandria, Yanga ilitolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1, kufuatia Al Ahly kushinda bao 1-0.

Kwa mujibu wa Mkwasa, Ngasa huenda akakaa nje ya uwanja kwa wiki moja kutokana na kupata majeraha makubwa wakati wa mechi hiyo, ambapo alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Athumani Iddi 'Chuji'.

Kwa upande wa Niyonzima, alisema mchezaji huyo bado anasumbuliwa na ugonjwa wa malaria, uliosababisha ashindwe kucheza mechi hiyo ya marudiano dhidi ya Wamisri.

Licha ya kukosekana kwa nyota hao, Mkwasa alisema kikosi chake kipo vizuri na kimejiandaa vyema kushinda mechi yao dhidi ya Mtibwa Sugar.

"Kuanzia sasa, nguvu zetu tumezielekeza kwenye mchezo wa Jumamosi na uongozi utatoa taarifa ni lini timu itakwenda Morogoro kwa ajili ya mchezo huo,"alisema Mkwasa.

Kocha huyo alisema kikosi chake kilitarajiwa kuendelea na mazoezi jana jioni katika uwanja wa Kaunda ulioko makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam na huenda wakaenda Morogoro leo mchana au kesho asubuhi.

"Kiufundi tumejipanga kuhakikisha tunashinda mchezo wetu na Mtibwa ili tujiweke katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu, hasa ikizingatiwa kuwa kwa sasa tupo nafasi ya tatu lakini tunaamini tutarejea kileleni,"alisema Mkwasa.

Yanga inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 38 kutokana na mechi 17 ilizocheza, nyuma ya Mbeya City yenye pointi 39 baada ya kucheza mechi 21. Azam inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na ponti 40.

Mabingwa hao watetezi wanakabiliwa na mechi nyingine ngumu Machi 19 mwaka huu dhidi ya Azam, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

SIMBA YAIFAGILIA YANGA


UONGOZI wa klabu ya Simba, umeipongeza Yanga kwa kuonyesha kiwango cha juu cha soka katika mechi zake mbili za raundi ya pili ya michuano ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamekunwa na kiwango kilichoonyeshwa na watani wao katika mechi hizo na kuongeza kuwa, kutolewa kwao ni kwa bahati mbaya.

"Tunawapongeza sana Yanga kwa kucheza soka ya kiwango cha juu dhidi ya Al Ahly na sasa tunawakaribisha tena kwenye ligi kuu baada ya kutolewa,"alisema.

Yanga ilitolewa katika michuano hiyo baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 na Al Ahly katika mechi ya marudiano iliyochezwa mjini Alexandria. Mshindi ilibidi apatikane kwa njia ya penalti tano tano baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1.

Katika mechi ya awali iliyochezwa mjini Dar es Salaam, Yanga iliishinda Al Ahly bao 1-0 na ziliporudiana mjini Alexandria, Al Ahly nayo ilishinda idadi hiyo ya bao.

Wakati huo huo, Kamwaga amesema mkutano mkuu wa Simba, utakaojadili marekebisho ya katiba, utafanyika Jumapili kama ilivyopangwa.

Kamwaga amewataka wanachama wa klabu hiyo kulipia kadi zao ili waweze kuhudhuria mkutano huo na kuchangia mambo muhimu yanayoihusu Simba.

Alisema ajenda ya mkutano huo itakuwa ni marekebisho ya katiba na wanachama ndio wenye maamuzi ya mwisho.

Katika hatua nyingine, klabu ya Simba imewasilisha malalamiko kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutaka ufanyike uchunguzi kuhusu mapato yanayopatikana katika mechi za ligi kuu kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Kamwaga alisema jana kuwa, klabu yake imebaini kuna mchezo mchafu unaochezwa na wasimamizi wa uwanja huo ndio sababu mapato yanayopatikana yamekuwa kiduchu.

"Tumewaomba TFF washirikiane na polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi ili kubaini tatizo ni nini,"alisema.

Akitoa mfano, Kamwaga alisema mechi kati yao na Prisons iliyochezwa wiki iliyopita, iliingiza sh. milioni 33, lakini idadi ya mashabiki walioingia uwanjani ilikuwa kubwa kuliko kiwango hicho cha mapato.

Alisema mechi kati yao na Mbeya City iliingiza sh. milioni 143 wakati idadi ya mashabiki walioingia uwanjani ilikuwa sawa na ile ya mechi yao na Prisons.

Kamwaga alisema pia kuwa, wameandika barua TFF kupinga kukatwa sh. milioni 25 kutokana na uharibifu wa viti uliofanywa na mashabiki wao wakati wa mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi dhidi ya Kagera Sugar.

Alisema wanataka warejeshewe pesa hizo kwa sababu kuna kesi mahakamani iliyofunguliwa dhidi ya mashabiki wanaodaiwa kuhusika na uharibifu huo, hivyo Simba haikustahili kukatwa pesa hizo.

TAMBWE HAUZWI NG'O-SIMBA



UONGOZI wa klabu ya Simba umesema hauna mpango wa kumuuza mshambuliaji wake nyota, Hamisi Tambwe kwa bei yoyote.

Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, Tambwe ana mkataba wa kuichezea klabu hiyo kwa miaka miwili.

Kamwaga alisema hayo kutokana na baadhi ya magazeti kuripoti jana kuwa, mchezaji huyo yupo tayari kujiunga na Yanga iwapo atalipwa mshahara mnono.

"Tambwe amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili, hivyo hatuwezi kumuuza kwa klabu yoyote kwa sasa,"alisema.

Tambwe, ambaye ni raia wa Burundi, alitia saini mkataba wa kuichezea Simba mwaka jana, mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hanspope na aliyekuwa katibu mkuu, Evodius Mtawala.

Kabla ya kujiunga na Simba, Tambwe alikuwa akiichezea klabu ya Vital'O ya Burundi, ambaye aliiwezesha kutwaa Kombe la Kagame mwaka jana nchini Sudan na kuibuka kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo.

Kwa sasa, Tambwe anaongoza kwa ufungaji mabao katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, akiwa amefunga mabao 19.

Wakati huo huo, uongozi wa Simba umesema, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Zdravko Logarusic, atamaliza mkataba wake wa kuifundisha timu hiyo 31 Mei mwaka huu.

Kamwaga alisema jana kuwa, bado hawajawa na uhakika wa kumuongezea mkataba kocha huyo kwa vile hatima yake itaamuliwa na kamati ya utendaji ya Simba, itakayopitia mwenendo wa timu hiyo katika ligi kuu msimu huu.

Loga alikabidhiwa jukumu la kuinoa Simba baada ya kutimuliwa kwa kocha mkuu wa zamani, Abdalla Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo 'Julio'.

VAN VICKER: SIJACHUKIZWA NA KAULI YA GENEVIEVE



 

VAN Vicker ni mmoja wa wacheza filamu waliojipatia sifa na umaarufu mkubwa barani Afrika kutokana na mwonekano wake wenye mvuto. Mcheza filamu huyo raia wa Ghana, ameoa na ni baba wa watoto watatu. Mkewe anaitwa Adjoa. Aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wacheza filamu wa Kinigeria, Genevieve Nnaji na Chika Ike. Katika makala hii ya ana kwa ana ya gazeti la Tribune la Nigeria, Van Vicker anaelezea kuhusu maisha yake ya usanii.

SWALI: Umekuwa maarufu kutokana na kucheza filamu za mapenzi. Umeupataje mwonekano mzuri ulionao?

JIBU: Sielewi. Siwezi kusema hasa iwapo ni kutoka kwa mama yangu au baba yangu. Naweza kusema ni mchanganyiko wa wote wawili kwa sababu, iwapo mama yangu angeolewa na mwanaume mwingine au baba yangu angeoa mwanamke mwingine, matokeo yangekuwa tofauti.

SWALI : Licha ya kuwepo kwa joto kali nchini Ghana kutokana na ukali wa jua, bado ngozi yako inaonekana kuwa mororo. Je, unatumia mafuta yoyote kuifanya ibaki ilivyo?

JIBU: Ni kweli nimekuwa nikitumia mafuta ya kutunza ngozi, si Ghana pekee, hata ninapokuwa Nigeria. Inategemea na mahali ninapokwenda kupiga picha za filamu. Lakini nakunywa maji mengi na kula mara kwa mara. Ni hivyo tu.

SWALI: Tumesikia uvumi mwingi kuhusu wewe. Unajisikiaje unaposikia uvumi kuhusu wewe binafsi?

JIBU: Mara nyingi huwa sijali uvumi wa aina yoyote kwa sababu naelewa ni mambo ya kutengenezwa. Baadhi ya wakati ninaposikia kujibu, huwa nafanya hivyo kupitia mitandao ya kijamii. Lakini watu hawawezi kuacha kuzungumza mambo ya uvumi, wataendelea kufanya hivyo.

SWALI: Unawezaje kumudu kuwa baba, mume na mwigizaji?

JIBU: Sidhani kama ni jambo kubwa sana. Ninaishi maisha ya kawaida. Nacheza nafasi mbalimbali kwenye filamu kama sehemu ya kazi yangu. Ninapokuwa nyumbani, nakuwa nyumbani na ninapokuwa kazi, sitaki mzaha. Nafanya mambo kama ambavyo baba wa kawaida angefanya. Mtu yeyote aliyeoa, anayefanyakazi na mwenye watoto, atakwenda nyumbani baada ya kazi na kuwa pamoja na familia yake. Hivyo ndivyo ninavyofanya. Hakuna cha ziada kuhusu hilo. Ninapokuwa nyumbani, nacheza na watoto wangu kila ninapopaswa kufanya hivyo.

SWALI: Lakini unapotoka nyumbani kwa siku kadhaa na kwenda kupiga picha za filamu, hauhisi tofauti yoyote? Unafanya nini kwa siku zote hizo unapokuwa mbali na familia yako?

JIBU: Kwa kawaida, kila ninaporudi nyumbani, najaribu kutumia muda mwingi kuwa pamoja nao. Huwa tunakwenda kutembea kwenye fukwe za bahari au kwenye bwawa la kuogelea, kutaza filamu ama kusafiri umbali mrefu au tunabaki nyimbani na kucheza michezo mbalimbali. Huwa najaribu kufanya vitu vingi kwa ajili yao.

SWALI: Ni waigizaji gani wa kike na kiume wanaokuvutia Nigeria?

JIBU: (Kicheko). Huwezi kunitega kwa kuniuliza swali hilo. Nafurahia kufanyakazi na waigizaji wenzangu wote.

SWALI: Kuna wakati Genevieve aliwahi kusema wewe si mwigizaji mzuri. Ulichukua hatua gani kuhusu kauli yake hiyo?

JIBU: Nilisoma habari hiyo, lakini haikukisumbua kichwa changu kwa sababu hayo yalikuwa maoni yake na ana uwezo wa kusema hivyo. Kamwe sikujibu kitu na sifikirii kufanya hivyo. Sina hisia mbaya kuhusu yeye.

Kwa sasa, iwe mtazamo wake umebadilika ama uko vilevile, hauwezi kuleta tofauti yoyote kwangu kwa sababu mimi ni mwigizaji babu kubwa na ninafanya kile ninachopaswa kukifanya. Nafurahia kazi yangu na ninafanya kilicho bora kadri ya uwezo wangu.

Japokuwa amesema hivyo, kama nitapewa kazi ya kufanya ikimuhusisha yeye (Genevieve), nitafanya kazi hiyo. Siwezi kusema kwa sababu alisema maneno hayo, siwezi kufanya kazi hiyo.

SWALI: Iwapo utapata nafasi ya kukutana naye, utamuuliza jambo hilo?

JIBU: Iwapo nitakutana naye kwenye shughuli yoyote au kucheza naye filamu, nitamuuliza, lakini siwezi kufanya hivyo kupitia kwenye vyombo vya habari. Baadhi ya vitu hivi, ambavyo watu wanaviandika kwenye magazeti au blogu si vya kweli. Inawezekana walibadili maneno yake.

Siku zote wamekuwa wakifanya hivyo kwangu, hivyo inawezekana wamefanya hivyo kwake. Lakini nitakapokutana naye ana kwa ana, nitamuuliza iwapo alisema maneno hayo. Na kama ni kweli, majadiliano yataendelea kati yetu juu ya kwa nini alisema hivyo na alisema maneno gani.

SWALI: Asili yako hasa ni wapi?

JIBU: Mimi ni mchanganyiko wa Kidachi, Kiliberia na Kighana.

SWALI: Ulikulia wapi?

JIBU: Nimelelewa na wanawake wawili katika maisha yangu, mama na dada yangu na siku zote tulikuwa tukihama kutoka sehemu moja hadi nyingine. Baba yangu alifariki nikiwa na umri wa miaka sita, hivyo sikuwahi kuwa na baba yangu muda wote. Mama yangu alinifundisha jinsi ya kuwa imara, kufanya vitu sahihi na alihakikisha nakuwa mtu mzuri, tofauti na watu wengi wanavyosema kwa mtu aliyechanganya uzao kama mimi.

SWALI: Watu wanasema nini kuhusu waliochanganya uzao (machotara)?

JIBU: Unaelewa wanavyosema, sihitaji kukueleza.

SWALI: Sielewi wanavyosema. Mimi pia ni chotara, nieleze?

JIBU: Ok, siku zote watu wanasema machotara ni watu wabaya?

SWALI: Wewe si mtu mbaya?

JIBU: Hapana.

SWALI: Ulifunga ndoa ukiwa bado kijana. Unamudu vipi kupambana na majaribu kutoka kwa rafiki zako wa karibu wa kike na washirika wako?

JIBU: Kama nilivyosema awali, ni mtazamo wa akili yangu na kufanya mambo kwa umakini. Najaribu kuwa makini kadri inavyowezekana na unaelewa baadhi ya wakati, unapaswa kucheza filamu za mapenzi na waigizaji wa kike na bado ukaendelea kuwa makini kwa sababu huo ndio uzuri wa kazi. Unaweza kuigiza mapenzi na watazamaji wakadhani upo kwenye mapenzi ya dhati na mwigizaji unayecheza naye, lakini wakati huo huo baada ya filamu kumalizika, hauwi tena na hisia kuhusu yeye.

SWALI: Umewahi kuvutiwa na mwigizaji yeyote wa kike mkiwa kwenye harakati za kucheza naye filamu?

JIBU: Haijawahi kutokea hivyo. Mwanamke pekee, ambaye nilisoma habari zake ni wakati walipoandika kwamba nimevunja ndoa ya Chika Ike. Sioni iwapo habari hiyo ilikuwa na maana yoyote, lakini walisema nilisababisha ndoa yake kuvunjika.

SWALI: Vipi kuhusu mashabiki wako wa kike? Wamekuwa wakikusumbua?

JIBU: Unamaanisha nini kwa kusema kunisumbua?

SWALI: Umekuwa ukipokea mara ngapi simu, barua pepe na meseji kupitia twitter kutoka kwa mashabiki wako wa kike?

JIBU: Siwezi kuita huo ni usumbufu. Ni watu wanaoifurahia kazi yangu na wanataka kunifahamu mimi binafsi. Ni kweli, napokea simu mara kwa mara, lakini najaribu kutenga muda. Siwezi kuwasiliana nao muda wote, hivyo baadhi ya wakati nawapuuza, wakati mwingine najaribu kujibu maswali yao.

ISERE KUFUNGUA MADUKA YA VIFAA VYA MICHEZO MIKOANI


KAMPUNI ya Isere Sports imesema itaendelea kufungua maduka ya vifaa vya michezo katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kujenga mazingira ya kuwafanya vijana wapende kushiriki kwenye michezo.

Mkurugenzi wa Masoko wa Isere Sports, Abbas Isere, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, tayari ameshafungua duka lingine la vifaa hivyo katika mkoa wa Dodoma.

Isere alisema duka lake la kwanza lipo mtaa wa Mchikichi, Dar es Salaam, na limekuwa likiuza vifaa vya michezo ya aina mbalimbali.

Mbali na kuuza vifaa vya michezo, Isere alisema kampuni yake imekuwa ikitoa msaada wa vifaa hivyo kwa shule za msingi, sekondari na kwa timu zinazoshiriki katika ligi mbalimbali za soka nchini.

Alisema hivi karibuni alitoa msaada wa vifaa hivyo kwa shule ya sekondari ya Kerezange iliyoko Majohe mkoani Dar es Salaam na kwa timu ya Fresh Niga inayoshiriki michuano ya ligi daraja la tatu Kilwa Masoko mkoani Lindi.

"Lengo langu katika kutoa misaada ya aina hii ni kukuza vipaji vya vijana katika soka na kuwaendeleza katika mchezo huo,"alisema Isere.

Aliongeza kuwa mbali na michezo kutoa ajira, pia imekuwa ikiwasaidia vijana kuimarisha afya zao na kuwaepusha na vitendo viovu kama vile uvutaji dawa za kulevya, ulevi na uhuni.

Kwa mujibu wa Isere, maduka yake yanauza vifaa vya michezo mbalimbali, ikiwemo soka, netiboli, ngumi, riadha, mpira wa kikapu na mingineyo.

Alisema kwa sasa, soko lake kubwa ni fulana za michezo zenye nembo za klabu mbalimbali maarufu duniani, lakini anazouza zaidi ni za timu za Barcelona, Real Madrid, Manchester United, Chelsea na Liverpool.

"Vifaa vyangu vyote ninavyouza ni orijino na vya kiwango cha juu ndio sababu bei zake zipo juu kidogo. Siuzi vifaa feki. Nauza vifaa orijino kwa lengo la kuimarisha biashara yangu na ninaviuza kwa bei ya jumla na rejareja," alisema Isere.

Mkurugenzi huyo amesema pia kuwa, fulana za Simba na Yanga na zile zenye nembo na rangi ya Taifa Stars, ndizo zinazoongoza kwa mauzo, hasa timu hizo zinapofanya vizuri katika michuano ya ligi na kimataifa.

Ameongeza kuwa, amekuwa akiuza jezi kwa bei ya sh. 500,000 kwa seti moja na kuongeza kuwa, bei ya fulana ni kati ya sh. 20,000 na sh. 15,000 kwa kutegemea ubora wake.

Tuesday, March 11, 2014

MTIHANI WA MAWAKALA WA WACHEZAJI APRILI 3


Mtihani kwa ajili ya watu wanaotaka kuwa mawakala wa wachezaji wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utafanyika Aprili 3 mwaka huu saa 4 kamili asubuhi ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (FIFA).
Kwa wanaotaka uwakala huo wanatakiwa kujisajili ambapo watapewa kanuni mbalimbali za FIFA na TFF ili waweze kujiandaa kikamilifu kwa mtihani huo utakaokuwa na sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ya mtihani huo ni maswali kutoka FIFA wakati nyingine ni kutoka TFF.
Tanzania ina mawakala watatu tu wa wachezaji wanaotambuliwa na FIFA. Mawakala hao ni Ally Saleh, John Ndumbaro na Mehdi Remtulla

RATIBA YA LIGI KUU YAPANGULIWA, SIMBA NA COASTAL UNION SASA KUCHEZA MACHI 23 BADALA YA LEO

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeifanyia marekebisho ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ambapo sasa itamalizika Aprili 19 mwaka huu badala ya Aprili 27 mwaka huu.

Marekebisho hayo yamefanyika ili kutoa fursa kwa timu ya Taifa 9Taifa Stars) kujiandaa kwa mechi za mchujo la Kombe la Afrika 2015 ambapo itacheza raundi ya awali Mei mwaka huu.

Kutokana na marekebisho hayo, Yanga itacheza na Prisons (Uwanja wa Taifa) Machi 26 mwaka huu katika mechi ya raundi ya 17 wakati Machi 19 mwaka huu kwenye uwanja huo huo ni Yanga na Azam.

Machi 15 mwaka huu kutakuwa na mechi mbili; Azam na Coastal (Azam Complex), na Mtibwa Sugar itacheza na Yanga (Jamhuri). Mgambo na Azam zitacheza Machi 26 mwaka huu Mkwakwani, na Aprili 9 mwaka huu Yanga itaialika Kagera Sugar (Taifa).

Raundi ya 22 itaanza Machi 22 mwaka huu kwa mechi kati ya Kagera vs Prisons (Kaitaba), JKT Ruvu vs Mbeya City (Azam Complex), na Rhino vs Yanga (Ali Hassan Mwinyi). Machi 23 mwaka huu ni Simba vs Coastal (Taifa), Mgambo vs Mtibwa (Mkwakwani), Ruvu Shooting vs Ashanti (Mabatini) na Azam vs Oljoro (Azam Complex).

Machi 29 mwaka huu itaanza raundi ya 23 kwa mechi kati ya Ashanti vs Oljoro (Azam Complex) wakati Machi 30 ni Mbeya City vs Prisons (Sokoine), Kagera vs Ruvu Shooting (Kaitaba), Mtibwa vs Coastal (Manungu), JKT Ruvu vs Rhino (Azam Complex), Azam vs Simba (Taifa), na Mgambo vs Yanga (Mkwakwani).

Raundi ya 24 inaanza Aprili 5 mwaka huu kwa Kagera vs Simba (Kaitaba), Ashanti vs Mbeya City (Azam Complex). Aprili 6 mwaka huu ni Coastal vs Mgambo (Mkwakwani), Oljoro vs Prisons (Sheikh Kaluta Amri Abeid), Rhino vs Mtibwa (Ali Hassan Mwinyi), Ruvu Shooting vs Azam (Mabatini) na Yanga vs JKT Ruvu (Taifa).

Aprili 12 mwaka huu inaanza raundi ya 25 kwa Mtibwa vs Ruvu Shooting (Mabatini), Coastal vs JKT Ruvu (Mkwakwani), Prisons vs Rhino (Sokoine). Aprili 13 mwaka huu ni Mgambo vs Kagera (Mkwakwani), Simba vs Ashanti (Taifa), Mbeya City vs Azam (Sokoine) na Oljoro vs Yanga (Sheikh Kaluta Amri Abeid).

Raundi ya 26 ni Aprili 19 mwaka huu kwa Rhino vs Ruvu Shooting (Ali Hassan Mwinyi), Mbeya City vs Mgambo (Sokoine), Prisons vs Ashanti (Jamhuri, Morogoro), JKT Ruvu vs Azam (Azam Complex), Oljoro vs Mtibwa (Sheikh Kaluta Amri Abeid), Coastal vs Kagera (Mkwakwani) na Yanga vs Simba (Taifa).

WAAMUZI 22 KUSHIRIKI SEMINA DAR


Waamuzi na waamuzi wasaidizi 22 wameteuliwa kushiriki semina na mtihani wa utimamu wa mwili kwa robo ya kwanza ya mwaka huu itakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Machi 14 hadi 16.

Semina hiyo inashirikisha waamuzi wote wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na wale wa ngazi ya juu (elite) kutoka Tanzania Bara za Zanzibar.

Waamuzi hao ni Charles Simon (Dodoma), Dalila Jafari (Zanzibar), Ferdinand Chacha (Mwanza), Hamis Chang’walu (Dar es Salaam), Helen Mduma (Dar es Salaam), Israel Mujuni (Dar es Salaam), Issa Vuai (Zanzibar), Janeth Balama (Iringa), Jesse Erasmo (Morogoro), John Kanyenye (Mbeya) na Jonesia Rukyaa (Bukoba).

Josephat Bulali (Zanzibar), Lulu Mushi (Dar es Salaam), Martin Saanya (Morogoro), Mfaume Nassoro (Zanzibar), Mohamed Mkono (Tanga), Mwanahija Makame (Zanzibar), Ngaza Kinduli (Zanzibar), Oden Mbaga (Dar es Salaam), Ramadhan Ibada (Zanzibar), Samwel Mpenzu (Arusha) na Waziri Sheha (Zanzibar).

Wakufunzi wa semina hiyo ambao wanatambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ni Joan Minja na Riziki Majala.

WATAKAOVUNJA VITI UWANJA WA TAIFA KUKIONA



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunalaani vikali fujo na uhabirifu wa mali unaofanywa na washabiki viwanjani wakati mechi mbalimbali zikiwemo zile za kimataifa na ligi za hapa nchini.

Tunaiomba radhi Serikali kwa uharibifu wa viti uliotokea kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga ya Tanzania na Al Ahly ya Misri iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Uharibifu huo wa viti umesababisha hasara ya sh. milioni 15 kwa wamiliki wa uwanja huo ambao ni Serikali. TFF tutalipa fedha hizo kwa Serikali kutokana na uharibifu huo.

Tunaendelea kuchunguza tukio hilo, huku tukijiandaa kutoa adhabu kwa klabu na washabiki husika kulingana na kanuni zetu. Adhabu itakuwa kali ili iwe fundisho kwa wengine.

Kwa mujibu wa Serikali, viti kumi viling’olewa na kutupwa ovyo ovyo uwanjani wakati vingine 40 viliathirika kutokana na vurugu za watazamaji hao.

Tumebeba dhamana ya kulipa uharibifu huo kwa vile TFF ndiyo wenye dhamana ya kusimamia mechi za kimataifa, na ndiyo tulioomba idhidi ya kutumia uwanja huo.

Kwa vile sasa baadhi ya washabiki, wapenzi na wanachama wa klabu mbalimbali nchini wanataka kufanya suala la uharibifu kuwa la kawaida na mazoea, Serikali inakusudia kuchukua mapato yote ya mchezo husika endapo kutatokea uharibifu.

Pia kuruhusu uwanja kutumiwa bila watazamaji kwa baadhi ya mechi, na kutoruhusu uwanja huo kutotumika kabisa kwa baadhi ya mechi.

Sunday, March 9, 2014

YANGA YAFAN KIUME, YATOLEWA NA AL AHLY KWA PENALTI


YANGA SC imetolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya jumla ya kufungana bao 1-1 na Al Ahly katika mechi mbili za Dar es Salaam na Alexandria.


Yanga SC iliyoshinda 1-0 wiki iliyopita Dar es Salaam, leo imefungwa 1-0 baada ya dakika 90 kwenye mchezo wa marudiano Uwanja wa Border Guard mjini Alexandria.

Kipa Deo Munishi ‘Dida’ alipangua penalti mbili mfululizo ya nne na ya tano, lakini Yanga SC nao wakakosa penalti mbili mfululizo ya nne na ya tano.

Oscar Joshua alipiga penalti nzuri ikaguswa na kipa Sherif Ekramy Ahmed na kugonga mwamba na kurudi uwanjani, wakati Said Bahanuzi akapiga nje upande wa kushoto wa lango.

Sherif Ekramy Ahmed alipangua penalti ya mwisho ya Yanga SC iliyopigwa na Mbuyu Twite na kuwavusha Hatua ya 16 Bora mabingwa hao wa Afrika.

Waliofunga penalti za Yanga SC ni Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Didier Kavumbangu na Emmanuel Okwi.

Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao, Yanga SC wakicheza mchezo wa kujihami na mashambulizi ya kushitukiza.

Mrisho Ngassa alicheza vyema katika safu ya kiungo mchezeshaji akiwapa pasi nzuri washambuliaji Emmanuel Okwi, Simon Msuva, Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza.

Kiungo mkabaji Frank Domayo alishirikiana vizuri na mabeki wa kati Kevin Yondan na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wakati mabeki wa pembeni Mbuyu Twite kulia na Oscar Joshua kushoto walifanya kazi nzuri ya kuzuia na kusaidia mashambulizi

Kipa Deo Munishi ‘Dida’ alifanya kazi nzuri ya kulinda lango na kuwapanga mabeki wake, pia akianzisha haraka mashambulizi kila alipodaka mpira.

Dakika ya 21 mshambuliaji hatari wa Ahly, Amr Gamal alipata pasi nzuri ndani ya 18 akapiga nje kabisa kulia mwa lango.

Dakika ya 23 Abdallah Said alipiga shuti kali akiwa nje ya 18 likatoka nje sentimita chache kushoto mwa lango na Yanga SC iliwashitua kwa mara ya kwanza Ahly dakika ya 29 baada ya winga Simon Msuva kushindwa kuumiliki vyema mpira mrefu akiwa anatazamana na kipa ukamgonga na kutoka nje kulia mwa lango.

Mabeki wa Ahly waliwadhibiti washambuliaji wa Yanga dakika zote 45 za kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili, Yanga SC walikianza vizuri wakiwabana Al Ahly na kudhibiti mashambulizi yao, huku wao wakiendelea kushambulia kwa kushitukiza.

Dakika ya 55 Simon Msuva almanusra aipatie bao Yanga SC baada ya kupiga shuti akiwa ndani ya 18, lakini likatoka nje sentimita chache upande wa kushoto wa lango akiwa upande wa kulia amebanwa na mabeki wawili wa Ahly.

Ahly wakajibu shambulizi hilo haraka na kupata mpira wa dhabu ambao ulipopigwa dakika hiyo hiyo ya 55 ukasababisha kizaazaa langoni mwa Yanga, lakini Cannavaro akaokoa.

Yanga SC ilipata pigo dakika ya 65 baada ya nyota wake, Mrisho Ngassa kuumia na kutolewa nje nafasi yake ikizibwa na Athumani Iddi ‘Chuji’ dakika ya 66.

Ahly ilipata bao lake dakika ya 71, mfungaji Said Abdulwahed.

Baada ya bao, Ahly walikuwa wanashambulia mfululizo, sifa zimuendee kipa Dida aliyeokoa michomo kadhaa na mingine kutoka nje.

Baada ya dakika 90 kumalizika Ahly ikishinda 1-0, mchezo ulihamia kwenye mikwaju ya penalti na ndipo, safari ya Yanga ilipofikia tamati michuano ya Afrika, wakiendeleza utamaduni wao wa kutolewa mapema.

Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Deogratius Munishi 'Dida', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Mrisho Ngassa/Athumani Iddi ‘Chuji’ dk66, Didier Kavumbagu, Hamisi Kiiza/Said Bahanuzi dk85 na Emmanuel Okwi.