KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, February 12, 2012

BURIANI WHITNEY HOUSTON!






MWANAMUZIKI nyota wa Marekani na mcheza filamu nguli wa Holywood, Whitney Houston amefariki dunia ndani ya chumba cha hoteli ya Beverly Hilton mjini Los Angeles.

Mwili wa Houston (48) ulikutwa bafuni ndani ya chumba alichopanga na kuna habari kuwa, kabla ya kifo chake, alitumia dawa za kulevya na pombe. Mwanamuziki huyo alifariki saa 9.55 alasiri.

Hadi sasa, chanzo cha kifo cha mwanamuziki huyo hakijafahamika japokuwa Ijumaa jioni, alikuwa na baadhi ya rafiki zake wakinywa pombe katika baa ya hoteli hiyo.

Whitney alipangwa kutumbuiza katika sherehe za utoaji wa tuzo za Grammy, lakini mauti yalimkumba saa chache kabla ya sherehe hizo kuanza.

Gari la polisi liliwasili katika hoteli hiyo dakika chache baada ya muhudumu kupiga simu akieleza kwamba kuna mtu amekufa kwenye moja ya vyumba vilivyomo ghorofa ya nne.

Whitney alikuwa gwiji wa muziki wa pop na ndiye mwanamuziki anayetajwa kwamba, alikuwa na sauti nzuri. Baadhi ya nyimbo zake zilizompatia umaarufu mkubwa ni pamoja na I will always love you na Saving all my love for you.

Whitney alianza kujihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya baada ya kufunga ndoa na mwanamuziki mwingine nyota wa nchi hiyo, Bob Brown, aliyezaa naye mtoto mmoja wa kike, Bobbi Kristina.

Polisi wa Los Angeles wamesema inaweza kuchukua wiki sita hadi nane kuweza kubaini chanzo cha kifo cha mwanamuziki huyo.

Zambia mabingwa Afrika














LIBREVILLE, Gabon
TIMU ya soka ya taifa ya Zambia, Chipolopolo juzi iliweka historia ya aina yake baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kuibwaga Ivory Coast kwa penalti 8-7 katika mechi kali na ya kusisimua ya fainali iliyochezwa mjini hapa.
Mshindi wa pambano hilo ilibidi apatikane kwa njia ya penalti tano tano baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa suluhu.
Katika kupigiana penalti tano tano, wachezaji nyota wa Ivory Coast, Didier Drogba, Yaya Toure na Gervinho walipoteza.
Zambia imetwaa kombe hilo miaka 19 tangu wanasoka na viongozi wake 18 walipofariki katika ajali ya ndege iliyotokea mwaka 1993 nchini Gabon. Zambia ilirejea Gabon kwa lengo la kuweka historia ya kuwaenzi wanasoka hao.
Drogba ndiye aliyeikosesha Ivory Coast ushindi baada ya kupoteza penalti yake ndani ya dakika 90 baada ya shuti lake kupaa juu ya lango.
Zambia: Mweene,Musonda (Nyambe Mulenga 11), Sunzu, Himonde, Nkausu, Sinkala, Lungu, Chansa, Christopher Katongo, Kalaba, Mayuka, Nyambe Mulenga (Felix Katongo 74).
Subs Not Used: Kalililo, Kasonde, Mbesuma, Chamanga, Chivuta, Chintu, Kangwa, Sakuwaha, Titima.
Booked: Nyambe Mulenga.
Ivory Coast: Barry, Tiene, Toure, Bamba, Gosso, Zokora (Konan 75), Tiote, Toure Yaya (Bony 86), Gervinho, Kalou (Gradel 63), Drogba.
Subs Not Used: Yeboah, Boka, Doumbia, Coulibaly, Keita, Lolo, Eboue,Gnanahouan.Booked: Tiote, Bamba.
Referee: Badara Diatta (Senegal).

Waamuzi, kamishna wafungiwa ligi kuu




Waamuzi watatu na kamishna mmoja wameondolewa kuchezesha na kusimamia mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kutokana na kuonesha upungufu katika uchezeshaji na usimamizi.
Uamuzi huo ulifanywa na Kamati ya Ligi iliyokutana jana (Februari 11 mwaka huu) ambapo pamoja na mambo mengine ilipitia taarifa za waamuzi na makamishna wa VPL ambayo leo (Februari 12 mwaka huu) inaendelea katika raundi ya 17.
Peter Mujaya wa Mwanza aliyechezesha mechi namba 101 kati ya JKT Ruvu Stars na Yanga amefungiwa kwa miezi 12 kwa mujibu wa Kanuni ya 26(a) ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa kushindwa kumudu mchezo huo, hivyo kupata alama za chini.
Naye Isihaka Shirikisho wa Tanga ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa VPL msimu huu kwa kushindwa kumudu mchezo namba 105 kati ya Simba na JKT Oljoro. Moja ya udhaifu alioonesha ni kushindwa kumuadhibu mchezaji Patrick Mafisango ambaye alimsukuma baada ya kumuonesha kadi nyekundu Haruna Moshi wa Simba.
Mwamuzi mwingine aliyefungiwa kwa miezi 12 kwa mujibu wa Kanuni ya 26(a) ni Kennedy Mapunda wa Dar es Salaam aliyechezesha mechi namba 107 kati ya Villa Squad na Simba. Moja ya udhaifu wa Mapunda ni kushindwa kumpa kadi nyekundu Fred Cosmas wa Villa Squad baada ya kumuonesha kadi ya pili ya njano.
Pia waamuzi wasaidizi Michael Mkongwa wa Iringa na Kudura Omary wa Tanga waliochezesha mechi namba 112 kati ya Yanga na Mtibwa Sugar wameondolewa katika mechi zilizobaki za VPL kwa kutokuwa makini. Mwamuzi wa mechi hiyo Ibrahim Kidiwa amepewa onyo. Waamuzi wengine waliopewa onyo na kutakuwa kujirekebisha ni Hashim Abdallah wa Dar es Salaam aliyechezesha mechi namba 92 kati ya Moro United na Yanga, na mwamuzi msaidizi wa mechi ya Simba na Coastal Union, Issa Malimali wa Ruvuma.
Kamishna wa mechi namba 112 kati ya Yanga na Mtibwa Sugar, Mohamed Nyange ameondolewa katika orodha ya makamishna kwa mechi zilizobaki za VPL kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu.
MAFISANGO AONYWA, SIMBA YAPIGWA FAINI
Kamati ya Ligi imeagiza mchezaji Patrick Mafisango wa Simba aandikiwe barua ya onyo kutokana na kumsukuma mwamuzi Isihaka Shirikisho baada ya kumuonesha kadi nyekundu mchezaji mwenzake Haruna Moshi kwenye mechi kati ya Simba na JKT Oljoro.
Nayo klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya washabiki wake kurusha makopo ya soda na chupa za maji wakipinga uamuzi wa mwamuzi Shirikisho kumtoa kwa kadi nyekundu Haruna Moshi.
Wachezaji waliopigwa faini ya sh. 500,000 kila mmoja baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kutokana na kupiga ambapo pia wanakosa mechi tatu za ligi kwa mujibu wa Kanuni ya 25 ni nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa na Cyprian Lukindo wa Villa Squad.
SIMBA, AZAM ZAINGIZA MIL 67/-
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Azam lililochezwa Februari 11 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 67,548,000. Jumla ya watazamaji 19,257 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 117 kwa kiingilio cha sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 15,000 kwa VIP A.
Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 10,303,932.20 kila timu ilipata sh. 13,182,800.34, uwanja sh. 4,394,266.78. Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,757,706.78, TFF sh. 4,394,266.78, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,197,133.39, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 439,426.78 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni sh. 4,394,266.78.
Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000. wamuzi wa akiba sh. 30,000, tiketi sh. 4,350,000, maandalizi ya uwanja (pitch) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000.
Gharama nyingine ni Jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi; kila klabu ilipata sh. 1,347,990,280 wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata sh. 1,555,420. Powered by Sorecson : Creation de site internetBoniface WamburaOfisa HabariShirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Thursday, February 9, 2012

UNAWAFAHAMU WATU HAWA?

Hawa ni wacheza filamu wawili maarufu duniani. Wamecheza filamu nyingi za kivita na kibabe na kujipatia umaarufu mkubwa. Wote wawili ni Wamarekani. Ni miongoni mwa matajiri wa Hollywood. Je, unawatambua ni akina nani? Na mahali walipo ni wapi na walikuwa wanafanya nini? Nakaribisha majibu yenu-Mmiliki wa blogu, Zahor.

Zambia kucheza fainali na Ivory Coast

Wachezaji wa Zambia wakipongezana baada ya timu hiyo kuifunga Ghana bao 1-0 jana

Wachezaji wa Ivory Coast wakimpongeza mchezaji mwenzao, Gervinho baada ya kuifungia bao pekee dhidi ya Mali jana.

LIBREVILLE, Gabon
IVORY Coast na Zambia jana zilifuzu kucheza fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Mali na Ghana.
Katika mechi hizo zilizokuwa na ushindani mkali, Ivory Coast iliichapa Mali bao 1-0 wakati Zambia nayo iliipiga Ghana mweleka wa idadi hiyo ya bao.
Bao pekee la Ivory Coast lilifungwa na mshambuliaji Gervinho katika kipindi cha kwanza, kufuatia uzembe wa mabeki wa Mali.
Katika mechi hiyo, Ivory Coast ilitawala vipindi vyote viwili huku washambuliaji wake, Didier Drogba na Yaya Toure walikosa nafasi kadhaa za kufunga mabao.
Nayo Zambia ilijipatia bao lake la pekee dakika ya 78 kupitia kwa mshambuliaji wake, Emmanuel Mayuka, aliyetokea benki.
Hii ni mara ya kwanza kwa Zambia kufuzu kucheza fainali ya michuano hiyo katika kipindi cha miaka 18 iliyopita na sasa itakutana na Ivory Coast katika mechi ya kutafuta bingwa, itakayochezwa Jumapili.
Ghana ilifanikiwa kupata penalti dakika ya nane iliyopigwa na Asamoah Gyan, lakini iliokolewa na kipa Kennedy Mweene wa Zambia.
Waghana walilazimika kumaliza mechi hiyo wakiwa na wachezaji 10 baada ya Derek Boateng kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika za mwisho.

KILIMANJARO MUSIC AWARDS
























Wednesday, February 8, 2012

Asha Baraka aichachafya Mashujaa Band


MKURUGENZI wa Kampuni ya African Stars Entertainment (ASET), Asha Baraka amesema kamwe bendi yake ya Twanga Pepeta International haiwezi kutetereka hata kama wataondoka wanamuziki watano kwa mpigo.
Asha amesema Twanga Pepeta ni chuo cha sanaa na kwamba ataendelea kufanyakazi ya kuwaendeleza wasanii wa Tanzania bila hofu yoyote hadi pale atakapoamua kustaafu kazi hiyo kwa ridhaa yake mwenyewe.
Mkurugenzi huyo wa ASET alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akijibu swali kuhusu sababu za kuishusha jukwaani bendi ya Mashujaa, ilipokuwa ikitumbuiza kwenye viwanja vya Leaders vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam.
Asha alisema aliamua kuishusha jukwaani bendi hiyo kwa sababu steji iliyokuwa ikiitumia ni mali yake, hivyo wamiliki wake walipaswa kuomba kuitumia badala ya kutumia ubabe ama kumdharau kwa sababu ya jinsia yake.
"Ile steji ni mali yangu, nimeitengeneza kwa pesa zangu, unapotaka kuitumia ni lazima uombe ili utumie bure ama uikodishe. Isiwe una pesa nyingi ukadhani nitakuogopa, sikuogopi, vinginevyo tengeneza chako,"alisema.
"Unachotakiwa kukifanya ni kuomba, lakini ukichukulia tu kwamba mimi ni mwanamke, atanifanya nini? Au mimi nina pesa nyingi hawezi kunifanya lolote, hapo umechemsha," aliongeza mwanamama huyo, ambaye ni mwanamke wa kwanza nchini kumiliki bendi ya muziki wa dansi.
Asha alisema iwapo kuna mfanyabiashara yoyote anayetaka kununua wanamuziki wote wa Twanga Pepeta, anaweza kufanya hivyo, lakini kamwe hawezi kubadili lolote katika maisha yake.
Mwanamama huyo alisema Twanga Pepeta inaundwa na wanamuziki wengi na kwamba bendi nyingi zilizoundwa miaka ya hivi karibuni kama vile Mapacha Watatu, Mchinga Sound, Extra Bongo na Mashujaa zimetokana na bendi yake.
"ASET inazalisha wanamuziki na tutaendelea kufanya hivyo. Tunao waimbaji 12 na kwa bendi ni wengi sana. Kwa bendi nzima, tunao wanamuziki 34. Hivi karibuni wanamuziki 13 walikwenda Uingereza kwa ajili ya maonyesho ya miaka 50 ya uhuru, lakini hatukusimamisha maonyesho yetu,"alisema.
"Walibaki wanamuziki 20 na waliendelea na maonyesho katika kumbi za Mango Garden, TCC na Leaders. Na wengine walikwenda mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya sherehe kama hizo," aliongeza mwanamama huyo.
"Sisi ni kiwanda cha sanaa, tutaendelea kuwepo na mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi, waendelee kutuunga mkono na kufurika kwa wingi kwenye maonyesho yetu kama ilivyokuwa wiki iliyopita,"alisema mwanamama huyo.
Akizungumzia tukio hilo, kiongozi wa bendi ya Mashujaa, Yohana Mlawa alisema, hawapendi kuingia kwenye malumbano na bendi ya Twanga Pepeta kwa sababu wanamheshimu mmiliki wake, Asha Baraka kama mdau aliyesaidia kwa kiasi kikubwa kukua kwa sanaa ya muziki wa dansi nchini.
Hata hivyo, Yohana alisema mwanamuziki kutoka bendi moja hadi nyingine ni si jambo la ajabu na halikuanza kwa mwimbaji Charles Baba, aliyekuwa Twanga Pepeta na kujiunga na Mashujaa na kwamba lengo kubwa huwa ni kutafuta maslahi mazuri zaidi.
"Ukishuka kutoka namba moja hadi mbili, usichukie, jipange upya ili urejee kule ulikotoka,"alisema.
Kiongozi huyo alisema Mashujaa haikumchukua Charles Baba kwa lengo la kuikomoa Twanga Pepeta, bali walifanya hivyo baada ya mwanamuziki huyo kuwaeleza kwamba, hakuwa na mkataba na bendi hiyo.
"Haya yote ni maisha, leo hii yupo Mashujaa, mkataba wake ukimalizika, anaweza kuamua kubaki Mashujaa ama kurudi Twanga Pepeta,"alisema.
Alisema si vizuri kwa wamiliki wa bendi za muziki ama vikundi vya sanaa kuwekeana visasi na kufanyiana vitendo vya kudhalilishana, badala yake wanapaswa kujiuliza chanzo cha tatizo na kulitafutia ufumbuzi.

SMZ yazipiga jeki Mafunzo na Jamhuri



SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeamua kuzipiga jeki timu za soka za Mafunzo na Jamhuri kwa kuzipatia sh. milioni 15 kila moja.
Msaada huo umelenga kuziwezesha timu hizo zishiriki vyema katika michuano ya klabu za Afrika, inayotarajiwa kuanza wiki ijayo.
Mafunzo inatarajiwa kushiriki katika michuano ya klabu bingwa Afrika wakati Jamhuri itashiriki katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Kwa mujibu wa ratiba, Jamhuri imepangwa kumenyana na Hwange ya Zimbabwe katika mechi itakayopigwa Februari 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba wakati Mafunzo itacheza na Muculamana de Maputo ya Msumbiji katika mechi itakayopigwa Februari 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Uamuzi huo wa serikali kuzipiga jeki timu hizo umekuja siku chache baada ya kuunda kamati maalumu ya kuendeleza michezo Zanzibar (KUMIZA).
Msemaji wa kamati hiyo, Ali Saleh alisema wiki hii mjini hapa kuwa, timu hizo mbili zinahitaji msaada mkubwa ili kufanikisha ushiriki wao katika michuano hiyo.
Mbali ya kutoa kiasi hicho cha pesa, serikali pia imetoa dola 9,000 za Marekani (sh. milioni 13.5) kwa ajili ya kuwagharamia waamuzi watakaochezesha mechi ya Mafunzo na Hwange.
Saleh alisema serikali haijatoa pesa hizo kwa Jamhuri kwa vile timu hiyo imesema inao uwezo wa kumudu gharama za waamuzi.
Kamati hiyo iliyoundwa na serikali inaongozwa na Sharifa Khamis, katibu wake ni Suleiman Mahmoud Jabir na wajumbe ni Khamis Abdalla, Ali Khalil Mirza na Saleh.
Serikali imesema kamati hiyo imeundwa kwa lengo la kusaidia michezo yote visiwani Zanzibar badala ya mchezo wa soka pekee.

Barnaba kurekodi na Fally Ipupa mwezi ujao


MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Barnaba anatarajiwa kuondoka nchini Machi 28 mwaka huu kwenda Ufaransa kurekodi wimbo wake mpya.
Barnaba atarekodi wimbo huo, unaojulikana kwa jina la ‘Tuachane kwa wema’ kwa kushirikiana na mwanamuziki nyota, Fally Ipupa wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Msanii huyo kutoka katika kundi la THT amesema, maandalizi yote kwa ajili ya safari hiyo yamekamilika, ikiwa ni pamoja na kupata viza ya kuingia nchini humo.
Barnaba alisema pia kuwa, ameshapangiwa siku ya kurekodi wimbo huo katika moja ya studio maarufu katika Jiji la Paris.
Kwa mujibu wa Barnaba, wimbo huo utakuwa miongoni mwa nyimbo zake mpya, zitakazokuwamo katika albam yake itakayokuwa na nyimbo 10. Albamu hiyo inatarajiwa kukamilika Juni mwaka huu.
''Katika ndoto zangu za kimuziki, nimekuwa nikitamani sana kurekodi na mastaa wa ukweli duniani na Fally Ipupa ni mwanzo tu kwani wapo wengine, ambao tayari nimeshawasiliana nao na tayari wamenithibitishia kunipa shavu,”alisema.
Msanii huyo alisema hata Fally Ipupa alikuwa akipenda kurekodi naye baada ya kumpagawisha wakati wa moja ya maonyesho yake aliyoyafanya hapa nchini.
Mbali na kurekodi wimbo huo Ufaransa, pia alisema atarekodi video yake nchini humo na anatarajia itakuwa babu kubwa.
Alizitaja nyimbo zingine zitakazokuwemo kwenye albamu hiyo kuwa ni Gubegube, Sidhani kama na Roho si moyo, ambazo zimerekodiwa katika studio za THT.

MWANAHAWA AJIENGUA T-MOTTO, AREJEA EAST AFRICAN MELODY


MWIMBAJI mkongwe wa muziki wa taarab nchini, Mwanahawa Ally amesema katika maisha yake ya usanii, hajawahi kutunga wimbo wa taarab.
Mwanahawa (61) amesema hajawahi kufanya hivyo kwa sababu utunzi wa nyimbo za taarab ni kazi ngumu na inahitaji kuwa na kipaji cha aina yake.
Mkongwe huyo wa taarab alisema hayo wiki hii alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Raha Zetu kilichorushwa hewani na kituo cha redio cha Clouds.
“Kutunga wimbo ni kazi ngumu, tofauti na watu wanavyofikiria kwani nyimbo nzuri ni lazima iwe na mashairi yenye vina vinavyolingana,”alisema mwanamama huyo.
“Tangu nianze kuimba taarab huu ni mwaka wa 45 na sijawahi kutunga nyimbo yangu mimi mwenyewe. Natungiwa tu na watu wengine, siwezi hata kujaribu, mashairi yana kazi ngumu,” aliongeza.
Mwanahawa, ambaye kwa sasa anafanyakazi katika kikundi cha East African Melody, amesema amerejea kikundi hicho baada ya kushindwa kuelewana na uongozi wa T Motto.
Alisema ameamua kujiondoa T Motto kwa hiari yake baada ya kuona mkurugenzi wake, Amin Salmin ameshindwa kukiendesha kwa mafanikio.
“Wakati waliponifuata, walinieleza kwamba nitalipwa shilingi milioni mbili na kusaini mkataba wa mwaka mmoja, lakini hadi sasa sijui kama huo mkataba uliandikwa na sijawahi kulipwa mshahara wowote,”alisema.
“Nasikia tu matangazo ya redio na televisheni yakieleza kwamba nipo T Motto, lakini sijawahi kumuona mkurugenzi wake hata siku moja na sidhani kama anafahamu nina shida gani,”aliongeza.
Mwanahawa alisema, anahisi kundi hilo lilitaka kuleta ushindani katika muziki wa taarab, lakini halikuwa limeandaliwa vyema ama kujipanga vizuri.
Alisema tangu aliporekodi wimbo mmoja na kundi hilo na kushiriki kwenye uzinduzi, hajawahi kuitwa kwenye onyesho lolote na haelewi iwapo bado lipo ama limekufa.
Mkongwe huyo amewahi kuimbia vikundi mbalimbali vya taarab kama vile Jahazi, Five Stars, Zanzibar Stars na East African Melody.

Barakat, Aboutrika, Motaeb wajiuzulu kuichezea Al-Ahly

Aboutrika

Emad Motaeb

Barakat


CAIRO, Misri
WACHEZAJI nyota watatu wa kimataifa wa Misri, wametangaza kustaafu kucheza soka baada ya kushuhudia mapigano yaliyotokea wiki iliyopita na kusababisha vifo vya mashabiki 74 katika mji wa Port Said.
Viungo Mohamed Barakat, Mohamed Aboutrika na mshambuliaji, Emad Motaeb wa Al-Ahly wamekieleza kituo cha televisheni cha Misri kuhusu uamuzi wao huo mara baada ya vurugu hizo.
Hata hivyo, Barakat alishindwa kuweka wazi iwapo hatarudi tena uwanjani. Alisema anaweza kurudi uwanjani iwapo tu mashabiki waliofariki katika vurugu hizo watalipwa fidia.
Vurugu hizo zilitokea wiki iliyopita mara baada ya kumalizika kwa mechi ya ligi kati ya Al-Ahly na Al-Masry iliyochezwa mjini Port Said. Katika mechi hiyo, Al-Masry iliibwaga Al-Ahly mabao 3-1.
Chanzo cha vurugu hizo ni mashabiki wa Al-Masry kuvamia ndani ya uwanja baada ya mchezo huo kumalizika na kuwashambulia wachezaji na mashabiki wa Al-Ahly. Katika vurugu hizo, zaidi ya mashabiki 800 walijeruhiwa.
Barakat, Aboutrika na Motaeb ni miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Misri kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika mara tatu mfululizo.
Aboutrika na Barakat walikuwemo kwenye kikosi cha Al-Ahly kilichocheza dhidi ya Al-Masry wakati Motaeb aliingizwa kipindi cha pili.
Kwa mujibu wa ripoti, mashabiki wengi walifariki dunia kutokana na kunasa kwenye njia za kutokea kwenye uwanja huo wakati walipokuwa wakikimbia mapigano.
Motaeb alikuwa amerejea uwanjani baada ya kuwa majeruhi kwa wiki kadhaa, akisumbuliwa na maumivu ya mgongo wakati Barakat naye alikuwa amerejea uwanjani baada ya kukosa mechi nne za ligi kutokana na maumivu ya misuli.
Baada ya kushuhudia vurugu hizo, wanasoka hao watatu wamesema hawawezi kuendelea kucheza soka katika klabu hiyo wakati nchi yao ikiwa katika mazingira hayo.
“Watu wanakufa na hakuna anayefanya lolote. Ni kama vita,”alisema Aboutrika alipohojiwa na kituo cha televisheni cha Al-Ahly. “Hivi maisha ni rahisi kiasi hiki?”
Aboutrika na mshindi wa zamani wa tuzo ya mwanasoka bora wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na kwa kushirikiana na Barakat na Motaeb, wameiwezesha Al-Ahly kupata mafanikio makubwa katika soka barani Afrika.
Al-Ahly imewahi kutwaa ubingwa wa ligi ya Misrimara 36 na pia kutwaa taji la ligi ya mabingwa Afrika mara sita.
Wakati nyota hao watatu wakiamua kustaafu kuichezea Al-Ahly, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Manuel Jose ameamua kureja kwao Ureno na kuitaka klabu hiyo ivunje mkataba wake.
Jose ameelezea jinsi alivyopigwa kwa fimbo na mijeredi na pia kushuhudia mashabiki wakiuawa wakati wa vurugu hizo, zilizosababisha vifo vya mashabiki 74.
“Nilipigwa kwa fimbo na mijeredi shingoni, kichwani na miguuni,”alisema Jose.
“Niliwashuhudia mashabiki wetu wakiuawa mbele yetu na hatukuwa na uwezo wa kufanya chochote,”aliongeza kocha huyo.
Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo walisema, polisi waliokuwepo uwanjani hawakufanya jitihada kubwa katika kukabiliana na vurugu hizo.
Kocha Msaidizi wa Al-Ahly, Pedro Barny alisema: “Kilichotokea ni vigumu kukielezea.”
“Tangu mwanzo wa mchezo, mashabiki wa timu pinzani waliruhusiwa kuingia uwanjani na fataki na waliturushia mawe bila kuchukuliwa hatua yoyote,” alisema Pedro.
“Mwishoni, vurugu zilikuwa kubwa bila ya maofisa wa usalama kuchukua hatua. Tulijitahidi kuokoa maisha ya baadhi ya mashabiki, lakini wengi walikufa mbele ya macho yetu,”aliongeza.
Jose (65) amewahi kuichezea na kuifundisha timu ya Benfica ya Ureno kwa miaka mingi, lakini alisema tukio hilo la Misri limebadili maisha yake.
“Hakuna kilichotokea kwa mchezaji yeyote, lakini tunajisikia kuwa na majonzi makubwa na nilirejea Ureno kimya kimya, nikiwapa heshima mashabiki wetu waliopoteza maisha,”alisema kocha huyo.
“Napaswa kufikiria maisha yangu tofauti hivi sasa. Japokuwa kila mmoja ananipenda hapa Misri, uzoefu huu umebadili kabisa mwelekeo wa maisha yangu,” alisisitiza.
Shirikisho la Soka la Misri (EFF) limetangaza kusimamisha mechi zote za ligi nchini humo na kutangaza siku tatu za maombolezo kwa ajili ya kuwakumbuka mashabiki waliopoteza maisha yao.
Wakati EFF imetangaza kusimamisha ligi, serikali ya kijeshi ya nchi hiyo imeutimua madarakani uongozi wa shirikisho hilo kutokana na vurugu hizo.
Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) limetaka lipatiwe maelezo kutoka EFF kuhusiana na vurugu hizo na limeitaka serikali ya kijeshi ya nchi hiyo, kuurejesha mara moja madarakani uongozi wa shirikisho hilo.
Kwa mujibu wa katiba ya FIFA, serikali za nchi zilizo wanachama wake, haziruhusiwi kuingilia kati masuala ya soka, vinginevyo nchi husika husimamishwa uanachama.
Iwapo FIFA itachukua hatua hiyo kwa Misri, klabu za Zamalek, Al-Ahly na Ismailia zitaondolewa kwenye michuano ya klabu za Afrika na kutoa nafasi kwa wapinzani wao kusonga mbele.

Ini edo, Rita wakacha kikao cha kuwapatanisha


LAGOS, Nigeria
WACHEZA filamu wa kike wenye mvuto nchini Nigeria, Ini Edo na Rita Dominic wamekacha kuhudhuria kikao kilichoitishwa kwa lengo la kuwasuluhisha.
Kikao hicho kilichoitishwa wiki iliyopita, kililenga kumaliza bifu la muda mrefu kati ya wacheza filamu hao, ambao ni miongoni mwa matajiri watano wa Nollywood.
Habari kutoka kwa watu walio karibu na wacheza filamu hao zimeeleza kuwa, wote wawili walikwepa kuhudhuria kikao hicho kwa visingizio mbalimbali.
Baadhi ya marafiki wa Ini na Rita ndio walioitisha kikao hicho, kilichopangwa kufanyika kwenye hoteli moja mjini Lagos.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, Rita alitoa udhuru akidai kuwa, alikuwa bize katika kutayarisha filamu yake mpya ya The Meeting wakati Ini alidai kuwa, alikwenda kuhudhuria shughuli muhimu.
Kwa muda mrefu sasa, akina dada hao wenye sura na maumbo yenye mvuto, wamekuwa hawaelewani huku kila mmoja akijigamba kuwa ni zaidi ya mwenzake.
Baadhi ya marafiki wa wacheza filamu hao, wamekuwa hawaifurahii hali hiyo na uadui uliopo kati yao na ndio sababu walipanga kuwakutanisha ili kumaliza tofauti zao.
Hata hivyo, marafiki hao wameonekana kukata tamaa baada ya Ini na Rita kushindwa kuhudhuria kikao hicho cha kuwapatisha.
Akinadada hao walianza kuwa na bifu mwaka jana baada ya Rita kuuponda utaratibu wa kuwateua washindi wa tuzo za mwigizaji bora, kupitia mtandao wa twitter.
Takwimu zinaonyesha kuwa, Ini ndiye anayeshika namba moja kwa utajiri miongoni mwa wacheza filamu wa kike nchini Nigeria. Mwanadada huyo anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Naira milioni 130.
Licha ya kukumbwa na vikwazo vingi, mafanikio aliyoyapata Ini hadi sasa ni makubwa, ikiwa ni pamoja na kutayarisha filamu zake mwenyewe na ni mwigizaji pekee wa kike anayecheza filamu nyingi zaidi kwa mwaka.
Kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, picha zake zimekuwa zikitumika kwenye matangazo ya Globacom, Noble Hair na kumwingizia Naira milioni 90. Anamiliki vitega uchumi vingi pamoja na maduka ya nguo na mitindo.
Naye Rita anashika nafasi ya tatu kwa utajiri nchini Nigeria ambapo mapato yake yanakadiriwa kufika Naira milioni 100. Ni mwigizaji wa kike mwenye mvuto zaidi Nollywood, ambaye amekuwa akiingia mikataba ya matangazo na kampuni mbalimbali kama vile Nokia, Globacom na Arik Air.Kwa sasa, anaandaa filamu yake, ambayo inatarajiwa kuanza kuonyeshwa hivi karibuni nchini Nigeria.

Ndoa ya Aki yajibu mapigo




LAGOS, Nigeria
NDOA ya mcheza filamu nyota wa Nigeria, Chinedu Ikedieze na mkewe, Nneoma imejibu mapigo baada ya kuelezwa kuwa, tayari mwanadada huyo amepata uja uzito.
Chinedu, maarufu kwa jina la Aki, alifunga ndoa na Nneoma mwishoni mwa mwaka jana na kuhudhuriwa na watu mbalimbali maarufu nchini Nigeria, akiwemo Rais wa nchi hiyo, Goodluck Jonathan.
Mmoja wa watu walio karibu na Aki ameueleza mtandao wa Nigeriafilms kuwa, kwa sasa mwili wa Nneoma umeongezeka uzito na ameanza kunenepa katika kila sehemu ya mwili wake.
Alipoulizwa iwapo taarifa hizo ni za kweli, Aki aling’aka na kuvitaka vyombo vya habari viache kufuatilia maisha yake na mkewe.
“Mimba? Hapana! Mnapaswa kutuacha kama tulivyo. Tunapaswa kuweka mambo yetu sawa kwanza kabla ya kuzaa watoto,”alisema Aki.
“Tafadhali tuacheni tufurahie maisha yetu ya ndoa,”aliongeza msanii huyo, aliyeanza kujipatia umaarufu mkubwa kupitia filamu ya Aki na Ukwa, aliyoicheza kwa kushirikiana na swahiba wake mkubwa, Osita Iheme ‘Ukwa’.
Siku chache baada ya kufunga ndoa, Aki alikaririwa akisema kuwa, yeye na mkewe wangependa kuwa na watoto wawili au watatu bila kujali jinsia yao.
Aki na mkewe walirejea nchini Nigeria mwishoni mwa mwezi uliopita, wakitokea Abu Dhabi, Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) walikokwenda kwa mapumziko.
Wanandoa hao walikaa Abu Dhabi kwa siku saba kwa ajili ya mapumziko maalumu ‘honeymoon’ na wanatarajia kuondoka tena Nigeria wiki ijayo kwenda Marekani.
Kwa mujibu wa mtandao wa Nigeriafilms, Aki na mkewe wamepanga kwenda Marekani kwa ajili ya sherehe ya siku ya wapendanao (Valentine Day).
Akizungumza na mtandao huo, Aki aliyaelezea mapumziko yao huko Abu Dhabi kuwa yalikuwa ya aina yake na kwamba walipata nafasi ya kutembelea sehemu mbalimbali zenye vivutio vya kitalii.
Inakadiriwa kuwa, Aki alitumia Naira milioni tano za Nigeria kwa ajili ya matembezi hayo, ambapo walipanga kwenye hoteli ya nyota nne ya Sheraton.

Monalisa aziponda tuzo za Min Ziff Red Carpet


MCHEZA filamu maarufu wa kike nchini, Yvonne Cherry ‘Monalisa’ ameziponda tuzo za Min Ziff Red Carpet kwa madai kuwa, hazina hadhi.
Monalisa amesema tuzo hizo zilizotolewa hivi karibuni kwa wachezaji filamu nchini, zilikuwa za ubabaishaji na maandalizi yake yalikuwa ya zimamoto.
Mwanadada huyo alisema hayo wiki iliyopita kupitia mtandao wa filamucentre baada ya kuulizwa mtazamo wake kuhusu utoaji wa tuzo hizo.
“Kusema ukweli, tuzo zilizotolewa hazikuwa na hadhi ya tuzo kutokana na maandalizi yake,”alisema msanii huyo wa zamani wa kundi la Mambo Hayo.
Mbali na tuzo zilizotolewa kutokuwa na hadhi, Monalisa alisema maandalizi ya utoaji wake yalikuwa ya zimamoto kutokana na kushindwa kufanyika kwa wakati uliopangwa.
Alisema ratiba iliyotolewa na waandaaji wa tuzo hizo ilionyesha kuwa, shughuli ingeanza saa mbili usiku, lakini badala yake ilianza usiku wa manane.
“Ni kweli wasanii tunahitaji tuzo au motisha kutoka kwa wadau wetu, wanaoguswa na kazi zetu, lakini jambo hili linahitaji maandalizi na tukio zima kupewa hadhi inayotakiwa,”alisema.
“Kwangu mimi, hafla ya utoaji wa tuzo hizo niliiona kama tamasha tu, ambalo halina tofauti na matamasha mengine yanayoandaliwa kila kukicha,”aliongeza. Monalisa amezishauri mamlaka zinazohusika na utoaji wa vibali kwa waandaaji wa tuzo mbalimbali, kuwa makini kwa kutowapa vibali hivyo watu wasiokuwa na sifa na uwezo.
Alisema wapo watu makini na wenye sifa za kuandaa tuzo hizo, lakini mamlaka husika zimekuwa zikiwanyima vibali kwa kisingizio cha kuwepo kwa watu maalumu wenye haki hiyo.

STEVE: Tutamkumbuka JK akiondoka madarakani



MSANII nyota wa vichekesho nchini, Steve Mengere ‘Nyerere’ amesema haijawahi kutokea na haitatokea kwa kiongozi wa nchi kupenda sanaa kama ilivyo kwa Rais Jakaya Kikwete.
Steve alisema hayo wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Mkasi, kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha East Africa.
Msanii huyo mahiri kwa kuigiza sauti ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere alisema, binafsi amepata mafanikio makubwa kiusanii baada ya kuingia madarakani Rais Kikwete.
“Mimi nasema Rais Kikwete akiondoka madarakani, wasanii watamkumbuka sana kwa sababu haijawahi kutokea na haitatokea kiongozi wa nchi anayependa sanaa kama JK,”alisema.
Aliitaja faida nyingine aliyoipata kiusanii tangu JK alipoingia madarakani kuwa ni kupata nafasi ya kukaa naye karibu na pia kula naye chakula.
“Lakini kikubwa zaidi ni Rais Kikwete kujua kwamba kuna mtu anaitwa Steve Nyerere,”alisema msanii huyo mwenye vituko na makeke.
Steve alisema kwa sasa maisha yanamwendea vizuri kwa sababu pesa ndogo ndogo hazimpigi chenga. Alisema filamu yake mpya ya Mr. President, iliyozinduliwa hivi karibuni imemweka kwenye chati ya juu zaidi.
Msanii huyo alikiri kuwa, sanaa ya vichekesho pia imemwezesha kutembelea mikoa mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na kufikisha ujumbe kwa njia ya vichekesho.
Steve alisema moja ya malengo makubwa aliyonayo katika siku zijazo ni kuwa mwanasiasa. Alisema anavutiwa sana na mambo ya siasa na anapenda siku moja awe mbunge ama kiongozi wa chama.
Hata hivyo, Steve alikiri kuwa ni vigumu kwa wasanii nchini kupata mafanikio makubwa kiusanii kutokana na kutokuwa na umoja. Alisema sababu kubwa inayowafanya wasanii wasiwe na msimamo ni njaa.
“Wasanii hatuna viwango maalumu vya malipo kwa kazi tunazozifanya. Wewe ukikataa malipo ya shilingi 500,000 kwa kuona ni kiwango kidogo, mwenzako atapokea. Na ukitaka ulipwe shilingi milioni moja, utakufa na njaa,”alisema.

Chaneta kuandaa fainali za Afrika


CHAMA cha Netiboli cha Afrika (NA) kimekipa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) nafasi ya kuandaa michuano ijayo ya netiboli ya Afrika.
Kaimu Katibu Mkuu wa CHANETA, Rose Mkisi alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano mkuu wa NA uliofanyika hivi karibuni mjini Windhoek.
Rose alisema michuano hiyo, ambayo itafanyika nchini kwa mara ya kwanza, imepangwa kufanyika kati ya Mei 8 na 18 mwaka huu Dar es Salaam.
"Hakika hii ni faraja kubwa kwetu na kwa wadau na mashabiki wa mchezo wa netiboli, ambao umeonekana kukua kila kukicha na kuiletea sifa kubwa nchi yetu katika michuano ya kimataifa," alisema.
Rose alisema hivi sasa uongozi wake unajipanga kusaka fedha na wadhamini ili kufanikisha michuano hiyo. Alisema chama chake kinahitaji sh. milioni 187 ili kiweze kuandaa michuano hiyo kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa Rose, tayari chama chake kimeshaanza kuwasiliana na kampuni, taasisi na wadau mbalimbali ili kuwashawishi wajitokeze kudhamini michuano hiyo.
Rose alisema nchi 18 zilizo wanachama wa NA zinatarajiwa kushiriki katika michuano hiyo. Alizitaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini, Lesotho, Namibia na Uganda. Zingine ni Kenya, Malawi, Botswana, Rwanda, Burundi, Sudan, Ethiopia na wenyeji Tanzania.
Wakati huo huo, CHANETA inatarajia kuendesha semina yenye lengo la kukuza na kuboresha viwango vya makocha na waamuzi wa mchezo huo kati ya Machi 12 na 13 mwaka huu mkoani Dar es Salaam.
Rose alisema semina hiyo itaendeshwa na wakufunzi wawili, ambapo alisema mmoja atakuwa wa ndani na mwingine atatoka nje ya nchi.

Diamond, Kiba, Mashauzi kuwania tuzo nyingi

Isha Mashauzi

Diamond

Ali Kiba


KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) imetangaza majina ya wasanii watakaowania tuzo za wanamuziki bora nchini za mwaka 2011.
Katika tuzo hizo, vipengele 22 vitashindaniwa na washindi watatangazwa katika sherehe zitakazofanyika Aprili 14 mwaka huu kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Wasanii Isha Ramadhani ’Mashauzi’, Nassib Abdul ’Diamond’, Ally Kiba na Khadija Kopa ndio wanaoongoza kwa kuteuliwa kushiriki kwenye tuzo nyingi zaidi kuliko wengine.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, wasanii walioteuliwa kuwania tuzo hizo, wamepitia katika hatua mbalimbali.
Alisema baada ya wasanii kupita katika hatua tofauti, ikiwemo ya mchujo, majaji walikaa chini na kupata wasanii waliopata kura nyingi kabla ya kuhesabiwa na kupata washindi, ambao wameteuliwa kuwania tuzo hizo.
Kavishe alisema jumla ya tuzo 21 zitawaniwa. Alizitaja tuzo hizo kuwa ni mtumbuizaji bora wa kike, mtumbuizaji bora wa kiume, mwimbaji bora wa kiume, mwimbaji bora wa kike, wimbo bora wa taarabu, wimbo bora wa mwaka, wimbo bora wa kiswahili wa bendi, wimbo bora wa R&B, wimbo bora wa hip hop, wimbo bora wa raga na wimbo bora wa dancehall.
Alizitaja tuzo zingine kuwa ni ya rapa bora wa mwaka wa bendi, msanii bora wa hip hop, wimbo bora wa Afrika Mashariki, mtunzi bora wa mwaka, mtayarishaji bora wa nyimbo wa mwaka, video bora ya muziki wa mwaka, wimbo bora wa Afro Pop, wimbo bora wa zouk rhumba, wimbo bora wenye vionjo vya kiswahili na msanii bora anayechipukia.
Aliwataja wasanii walioteuliwa kuwania tuzo hizo kuwa ni Khadija Kopa, Isha Mashauzi, Queen Darleen, Dayna na Shaa (mtumbuizaji bora wa kike), Diamond, Ally Kiba, Bob Junior, Dully Sykes na Mzee Yusuf (mtumbuizaji bora wa kiume). Tuzo ya mwimbaji bora wa kiume inawaniwa na Ally Kiba, Diamond, Barnaba, Belle 9 na Mzee Yusuf.
Tuzo ya mwimbaji bora wa kike inawaniawa na Lady Jay Dee, Khadija Kopa, Isha Mashauzi, Dayna na Lina wakati tuzo ya wimbo bora wa taarab inawaniwa na Full Stop (Khadija Kopa), Mamaa Mashauzi (Isha Mashauzi), Hakuna Mkamilifu (Jahazi), Nani kama Mama (Isha Mashauzi) na Nilijua Mtasema (Jahazi).
Tuzo ya wimbo bora wa mwaka inawaniwa na Hakunaga (Suma Lee), Dushelele (Ally Kiba), Moyo Wangu (Diamond), Mathematics (Roma), Nilipe Nisepe (Belle 9) na Riz one (Izzo B). Tuzo ya wimbo bora wa Kiswahili wa bendi ni Dunia Daraja (Africans Stars), Hukumu ya Mnafiki (Mashujaa Band), Falsafa ya Mapenzi (Extra Bongo), Usia wa Babu (Mapacha Watatu) na Mtenda (Extra Bongo).

Bakhresa ajitosa kutetea kiti chake DRFA


WAGOMBEA watatu zaidi wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania uenyekiti katika uchaguzi wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA).
Miongoni mwa wagombea hao ni pamoja na Amin Bakhresa, ambaye anatetea nafasi hiyo. Wagombea wengine ni Salum Mkemi na Salum Mwaking'anda.
Mratibu wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA, Harudiki Kabunju alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, uchukuaji wa fomu ulitarajiwa kuhitimishwa saa 10 jioni.
Alimtaja mgombea mwingine aliyejitokeza kuchukua fomu jana kuwa ni Benny Kisaka, anayewania nafasi ya kuziwakilisha klabu katika mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Uchaguzi mkuu wa DRFA, ambao umekuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, umepangwa kufanyika Machi 18 mwaka huu.
Akizungumza uamuzi wake kutetea nafasi ya uenyekiti, Bakhresa alisema umetokana na malengo aliyojiwekea ya kukuza na kuendeleza soka katika mkoa wa Dar es Salaam.
Bakhresa alisema changamoto bado ni nyingi na ili atimize malengo yake, ameona ni vyema aendelee kukiongeza chama hicho.
Wagombea wengine waliochukua fomu ni Gungulungu Tambaza na Khamisi Kisiwa (makamu mwenyekiti), Selemani Salim Kigodi (ujumbe wa kamati ya utendaji),Ramadhani Kampira na Mohammed Bhinda (ujumbe wa klabu) na Ally Hassan (mweka hazina).
Wengine, nafasi wanazowania zikiwa kwenye mabano ni Muhsin Balhabou (ujumbe wa TFF), Kanuti Daudi (ujumbe wa kamati ya utendaji), Msanifu Kondo (katibu mkuu), Abeid Mziba, Hamisi Mkwama (ujumbe) na Lameck Nyambaya (ujumbe wa klabu).

Dewji aizawadia Chipolopolo sh. mil 22


MWANAMICHEZO na mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji amekunwa na mafanikio ya timu ya soka ya Taifa ya Zambia `Chipolopolo’ na amethibitisha furaha yake hiyo kwa kumpatia kila mchezaji wa timu hiyo kitita cha dola 500 za Kimarekani (sh. 750,000).
Kutokana na kiwango hicho cha fedha, Dewji amelazimika kutoka zaidi ya dola 13,000 (sh milioni 22.1 ) kwa ajili ya wachezaji 23 na viongozi wa timu hiyo waliopo Gabon, moja ya nchi mbili zilizoandaa michuano hiyo mikubwa barani Afrika. Nyingine ni Guinea ya Ikweta.
Dewji, aliyeiwezesha Simba kucheza fainali za Kombe la CAF mwaka 1993, alikabidhi kiasi hicho cha fedha kwa Rais wa Shirikisho la Soka Zambia (FAZ), Kalusha Bwalya katika ghafla fupi iliyofanyika jana Lusaka, Zambia.
Akikabidhi fedha hizo kwa Bwalya, Dewji ambaye yuko nchini humo kwa shughuli za biashara, alisema ameguswa na mafanikio ya Zambia katika michuano hiyo, ambayo yamerejesha heshima ya soka kwa nchi za kusini mwa bara la Afrika.
“Zambia ni majirani zetu, tunapakana nao. Lazima tujivunie mafanikio haya kwa sababu si ya Zambia peke yao, bali ya ukanda huu wote,” alisema Dewji na kuongeza kuwa, Zambia ni ndugu wa kweli na waliwahi kuwa wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ambalo Tanzania ni miongoni mwa wanachama wake.
Mbali na kuizawadia Zambia, Dewji alisema atakuwa tayari kufanya hivyo kwa timu yoyote itakayofanya vizuri, ikiwamo timu ya soka ya Tanzania, `Taifa Stars’.
“Kama timu inatoka ukanda huu, sitabagua, nitawatuza kwa heshima wanayoileta. Hata Twiga Stars wamefanya vizuri hivi karibuni nimewazawadia, lakini si busara kutangaza kila kitu, hata kwa vitu vidogo," alisema.
Dewji ameahidi kumwaga fedha zaidi kwa Zambia iwapo wataifumua Ghana katika mchezo wa nusu fainali. Mchezo huo ulitarajiwa kufanyika jana usiku.
“Nitawapa fedha zaidi na pia nitawakumbuka kwa zawadi maalumu wajane wa wachezaji waliokufa katika ajali ya ndege iliyotokea Pwani ya Gabon mwaka 1993,” alisema Dewji, Mkurugenzi wa kampuni ya Simba Trailers inayounda bodi za magari makubwa, yakiwemo ya mizigo na ya abiria.
Zambia iliyopo Gabon chini ya nahodha Christopher Katongo, ilitua katika fainali za mwaka huu kwa kiapo cha kuwafuta machozi Wazambia ambao miaka 19 iliyopita walipoteza kikosi chote cha kwanza kilichokuwa gumzo wakati huo barani Afrika.
Wachezaji waliokufa katika ajali hiyo ni Efford Chabala, John Soko, Whiteson Changwe, Robert Watiyakeni, Eston Mulenga, Derby Makinka, Moses Chikwalakwala, Wisdom Mumba Chansa, Kelvin "Malaza" Mutale, Timothy Mwitwa, Numba Mwila, Richard Mwanza, Samuel, Moses Masuwa, Kenan Simambe, Godfrey Kangwa, Winter Mumba na Patrick "Bomber".

Yanga yatwaa uongozi ligi kuu

MSHAMBULIAJI Kenneth Asamoah (kulia) wa Yanga akiwania mpira na Salvatory Ntebe (kushoto) wa Mtibwa timu hizo zilipomenyana jana katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. (Picha na Emmanuel Ndege).


MABAO yaliyofungwa na washambuliaji Kenneth Asamoah,Hamisi Kiiza na Shamte Ally jana yaliiwezesha Yanga kuiengua Simba katika uongozi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Mtibwa Sugar mabao 3-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilijipatia mabao hayo matatu katika kipindi cha pili baada ya timu hizo kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza zikiwa suluhu.
Ushindi huo uliiwezesha Yanga kutwaa uongozi wa ligi hiyo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kati yake na watani wao wa jadi Simba, kufuatia kila moja kuwa na pointi 34 baada ya kucheza mechi 16.
Yanga sasa imefunga mabao 28 na kufungwa mabao 13 wakati Simba imefunga mabao 25 na kufungwa 10. Azam imeshuka hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 32, ikiwa imefunga mabao 18 na kufungwa sita.
Mtibwa ililazimika kumaliza mechi hiyo ikiwa na wachezaji 10 baada ya Saidi Mkopo kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 33 na mwamuzi Ibrahim Kidiwa kutoka Tanga kwa kosa la kucheza rafu mbaya Stephano Mwasika wa Yanga.
Mtibwa ilikuwa ya kwanza kubisha hodi kwenye lango la Yanga dakika ya tano wakati Vicent Barnabas alipowatoka mabeki wawili wa timu hiyo, lakini wakati akijiandaa kufunga, kipa Shabani Kado alitokea na kuokoa hatari.
Yanga ilijibu mapigo dakika ya saba wakati Davis Mwape alipofumua shuti kali akiwa ndani ya 18, lakini mpira uligonga mwamba kabla ya kuokolewa na mabeki wa Mtibwa.
Katika dakika ya 14, Saidi Rashid wa Mtibwa Sugar alimtoka beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga na kufumua shuti kali, lakini lilitoka nje ya lango.
Dakika mbili baadaye, Mwape alifanikiwa kumtoka beki Salvatory Ntebe na kufumua shuti kali, lakini liligonga mwamba wa juu wa goli na kutoka nje.
Mwape alipata nafasi nyingine nzuri ya kufunga bao dakika ya 22 alipomtoka beki Salum Sued, lakini shuti lake lilitoka nje.
Rashid aliikosesha Mtibwa nafasi zingine nzuri za kufunga mabao dakika ya 30 na 32 baada ya kupewa pasi na Barnabas na Issa Rashid, kufuatia mashuti yake kutoka nje ya lango.
Kenneth Asamoah angeweza kuifungia Yanga bao dakika ya 45 alipopewa pasi akiwa ndani ya eneo la hatari la Mtibwa, lakini shuti lake lilitoka nje. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.
Licha ya kucheza ikiwa na wachezaji pungufu, Mtibwa ililisakama lango la Yanga mara kwa mara kipindi cha pili, lakini washambuliaji wake, Javu na Barnabas hawakuwa makini.
Uzembe wa beki Mwasika wa Yanga nusura uipatie bao Mtibwa dakika ya 64 baada ya kupokonywa mpira na Javu ndani ya eneo la hatari, lakini wakati akijiandaa kufunga, kipa Kado alitokea na kuokoa.
Yanga ilihesabu bao lake la kwanza dakika ya 73 kupitia kwa Asamoah. Alifunga bao hilo kwa shuti kali lililogonga mwamba wa goli na kutinga wavuni.
Kiiza aliiongezea Yanga bao la pili dakika ya 80 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mwasika kabla ya Shamte kuongeza la tatu dakika ya 86 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Haruna Niyonzima. Bao la kujifariji la Mtibwa lilifungwa na Issa Rashid dakika ya 89.
Yanga: Shaaban Kado, Godfrey Taita/Shamte Ally, Stephano Mwasika, Nadir Haroub, Athuman Idd, Salum Telela/Juma Seif, Omega Seme, Haruna Niyonzima, Davis Mwape, Hamisi Kiiza, Kenneth Asamoah.
Mtibwa Sugar: Deogratius Munisi, Juma Jaffar, Issa Rashid, Salvantory Ntebe, Salum Sued, Shaaban Nditi, Saidi Mkopi, Awadh Issa, Saidi Rashid, Thomas Mourice/ Hussein Javu na Vincent Barnabas/ Zuberi Katwila.