'
Friday, July 7, 2017
UCHAGUZI TWFA KUFANYIKA DAR ES SALAAM
Uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake (TWFA), sasa utafanyika Dar es Salaam badala ya Dodoma na Morogoro - mikoa iliyotangazwa awali.
Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi ya TWFA, Msomi Wakili George Mushumba, amesema kwamba taratibu zote zimekamilika na kwamba siku ya uchaguzi ni Jumamosi Julai 8, mwaka huu.
Wakili Mushumba ametoa wito kwa wajumbe wote kufika Dar es Salaam Ijumaa Julai 7, mwaka huu kwa ajili ya kufahamu tararibu za awali za uchaguzi.
Tayari Kamati ya Mushumba ilitangaza majina ya wagombea 11 waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu.
Majina ambayo yamepitishwa ni Amina Karuma, Rose Kisiwa, Somoe Ng’itu, Theresia Mung’ong’o, Hilda Masanche, Salma Wajeso, Zena Chande, Triphonia Temba, Mwamvita Kiyogoma, Jasmine Soudy na Chichi Mwidege.
Nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na Wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji.
FOMU ZA KUWANIA UONGOZI TAFCA
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA), Ramadhani Mambosasa ametoa wito wa walimu wa soka kujitokeza kwa wingi kuchukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi - ngazi ya taifa.
Mambosasa ametoa wito huo ikiwa zimebaki siku mbili tu kwa mujibu wa kanuni kukamilisha hatua hiyo. Fomu hizo zinazopatikana ofisi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam, zilianza kutolewa juzi Julai 3, 2017 na mwisho ni Julai 7, mwaka huu.
“Wanaojitokeza wachache. Wengine wanadai hawafahamu zilizo ofisi za DRFA. Tunatoa wito wajitokeze kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali,” amesema Mambosasa.
Nafasi zilizotangazwa kuwaniwa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina ambao fomu zao zinapatikana kwa Sh 200,000 wakati nafasi za wajumbe wa Mkutano Mkuu TFF na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji fomu zao zinapatikana kwa Sh 100,000.
UCHAGUZI CHAMA CHA WATAALAMU WA TIBA ZA MICHEZO
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Wataalamu wa Tiba za Michezo (TASMA), kimetangaza Uchaguzi Mkuu wa chama hicho kwamba utafanyika Agosti 5, mwaka huu katika Ukumbi wa Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.
“Wanachama wote wanakaribishwa kushiriki kwa namna moja au nyingine katika zoezi hili muhimu sana,” amesema Mwenyekiti wa kamati hiyo, Leslie Liunda alipokuwa anatangaza ramani ya mchakato wa uchaguzi huo leo Alhamis Julai 06, 2017.
Amesema: Mwanachama ye yote anayependa kukiongoza chama hiki anaombwa kuchukua fomu katika ofisi za Olimpiki Maalumu, zilizoko jirani na Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwa ajili ya kugombea nafasi anayoona kuwa anaweza kuimudu.”
Nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina ambao fomu zao zinapatikana kwa Sh 200,000 wakati nafasi za wajumbe wa Mkutano Mkuu TFF na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji fomu zao zinapatikana kwa Sh 100,000.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment