KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, July 2, 2017

MCHAKATO WA UCHAGUZI MKUU TFF WASIMAMISHWA

KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imetangaza kusimamisha mchakato wa uchaguzi wa shirikisho hilo hadi itakapotangazwa baadaye.

Uamuzi huo umetangazwa leo na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Wakili Revocatus Kuuli, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF, zilizoko Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Kuuli amesema amefikia uamuzi huo baada ya kutokea hali ya kutokuelewana kati ya wajumbe wa kamati hiyo, kuhusu wagombea waliofikishwa mahakama kwa tuhuma za utakatishaji fedha.

Kwa mujibu wa Kuuli, baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walitaka wagombea hao kupitishwa moja kwa moja bila kufanyiwa usaili wakati wengine walipinga.

Kutokana na tofauti hizo, Wakili Kuuli alisema wameamua kwa kauli moja kusitisha mchakato huo ili kufikia mwafaka wa jambo hilo.

Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, ambaye pia ni Mkurugenzi wa shirikisho hilo, Salum Madadi, amethibitisha kusimamishwa kwa uchaguzi huo.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Alfred Lucas, alisema uchaguzi huo utafanyika kama ilivyopangwa, isipokuwa mchakato wake umesimamishwa kwa muda ili kutafuta suluhu ya tofauti zilizojitokeza.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi, Katibu wake, Celestine Mwesigwa na Mhasibu, Nsiande Isawafo Mwanga,  walifikishwa mahakamani wiki iliyopita kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi, ikiwemo tuhuma za utakatishaji wa fedha. Watuhumiwa hao wapo rumande hadi kesho.

No comments:

Post a Comment