Mtangazaji wa Televisheni ya Everton, Darren Griffiths akizungumza katika hafla hiyo iliyowakutanisha wagonjwa waliotibiwa na wanaotibiwa ugonjwa wa Matende na Mabusha na baadhi ya wachezaji wa timu ya Everton ambayo imekuwa ikifadhili matibabu hayo kushoto ni Graham Stuart na Leon Osman wachezaji wa zamani wa Everton.
NA WAMJW-DAR ES SALAAM
UONGOZI wa timu ya mpira wa miguu ya Everton kutoka nchini Uingereza imeridhishwa na huduma inayotolewa kwa wagonjwa wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ikiwemo mabusha na matende hapa nchini.
Hayo yamezungumzwa na mmoja wa viongozi wa Everton Bw. Darren Griffiths ambao ni washiriki katika kuchangia huduma ya magonjwa hayo hapa nchini ambaye ameongozana na timu yake ili kucheza mechi ya kirafiki na timu ya Gor Mahia kutoka chini Kenya.
“Tunayo furaha kuona wagonjwa wengi waliokuwa wanaumwa mabusha na metende nchini Tanzania kwa sasa wamepona kabisa na tunahaidi kuwa na Wizara ya afya bega kwa bega katika kutokomeza magonjwa haya” alisema Bw. Darren Griffiths
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Huduma za Kinga Wizara ya Afya Dkt. Vida Mmbaga amesema kuwa kutokana na ushiriki wa Everton katika kuchangia utoaji wa Huduma ya kutibu ugonjwa huo wamefanikiwa kupata ujuzi wa upasuaji hasa kwa wagonjwa wa mabusha na matende hapa nchini.
Aidha Dkt. Vida amesema kuwa Serikali ikishirikiana vyema na wananchi na mashirika mbalimbali ya afya magonjwa hayo yatatokomea kwa kiasi kikubwa hapa nchini mpaka kufikia mwaka 2025.
Mbali na Hayo Dkt. Vida amesema kuwa anawashukuru watu wa Everton kwa kupitia ushirikiano wao katika sekta ya afya kwa kutoa huduma pamoja na mafunzo kwa wataalamu ambapo imesaidia kuwafanyia upasuaji wagonjwa elfu moja.
Kwa upande wake Bw. Yahya Ally Kidege mkazi wa pugu stesheni amesema kuwa anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwajali wananchi wake kwani amepata upasuaji wa ugonjwa wake wa busha na amepona kabisa kwan alikua na ugonjwa huo takribani miaka 20.
No comments:
Post a Comment