KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, July 16, 2017

SIMBA YAENDA KUWEKA KAMBI AFRIKA KUSINI


TIMU ya soka ya Simba inatarajiwa kuondoka nchini Jumanne kwenda Afrika Kusini kwa ziara ya wiki mbili, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara.

Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo kwa vyombo vya habari jana ilisema kuwa, kikosi kitakachoondoka Jumanne hakitakuwa na wachezaji waliomo kwenye timu ya Taifa ya Tanzania Bara.

Wachezaji hao bado wapo kwenye kikosi cha Tanzania Bara, wakijiandaa na mchezo wa marudiano wa michuano ya Kombe la CHAN dhidi ya Rwanda, Jumamosi ijayo. Katika mechi ya awali iliyochezwa jana mjini Mwanza, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wachezaji hao, kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe, Salim Mbonde, viungo Muzamil Yassin, Said Ndemla na Shiza Kichuya na mshambuliaji John Bocco, wataungana na Simba baada ya mchezo huo wa marudiano dhidi ya Rwanda.

Ikiwa Afrika Kusini, mbali ya kufanya mazoezi chini ya kocha wake, Joseph Omog, Simba itacheza mechi kadhaa za kujipima nguvu.

Baada ya ziara hiyo ya Afrika Kusini, Simba itarejea nchini kwa ajili ya tamasha lake la kila mwaka la Simba Day, litakalofanyika Agosti 8, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba imekuwa ikilitumia tamasha hilo kutambulisha wachezaji wake wapya na pia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya timu kutoka nje ya nchi.


No comments:

Post a Comment