'
Tuesday, July 18, 2017
SIKINDE KUFANYA MAONYESHO KENYA WIKI IJAYO
BENDI ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra (Sikinde), inatarajiwa kuondoka nchini wiki ijayo kwenda Nairobi, Kenya kwa ziara ya maonyesho mawili ya muziki.
Kiongozi wa bendi hiyo, Abdalla Hemba, alisema mjini Dar es Salaam, jana kuwa, bendi hiyo itakwenda Kenya kwa mwaliko uongozi wa Hoteli ya Deepwest Resort.
Hemba alisema bendi hiyo itaondoka nchini Jumatatu ijayo kwa basi, ikiwa na kundi la wanamuziki 14, ambao hakuwa tayari kutaja majina yao kwa madai kuwa ni mapema kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa Hemba, onyesho la kwanza la bendi hiyo limepangwa kufanyika Julai 28 wakati onyesho la pili litafanyika Julai 29, mwaka huu, kwenye ukumbi wa hoteli hiyo.
Hemba alisema kutokana na maelezo waliyopatiwa na mratibu wa onyesho hilo, Abuu Omar, ukumbi wa Deepwest Resort upo jirani na jengo la T-Mall, barabara ya Lang'ata, Jijini Nairobi.
Tayari baadhi ya vyombo vya habari nchini Kenya, vimeshaanza kuitangaza ziara hiyo, ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa muziki nchini humo.
Baadhi ya vyombo hivyo vya habari, likiwemo gazeti la Daily Nation, vimeielezea bendi hiyo kuwa ni miongoni mwa zilizotamba kimuziki katika ukanda wa Afrika Mashariki miaka ya 1980.
Ziara hiyo itakuwa ya tatu kwa Mlimani Park Orchestra nchini Kenya. Ilikwenda huko kwa mara ya kwanza mwaka 1988, ambako ilirekodi albamu ya Kisonoko na kutumbuiza kwenye sherehe za maadhimisho ya kutimiza miaka 10 madarakani, Rais wa zamani wa nchi hiyo, Daniel Arap Moi.
Sikinde ilikwenda tena Kenya mwaka 2006, ambapo ilifanya maonyesho mawili katika ukumbi wa Carnivores ulioko mjini Nairobi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment