'
Wednesday, November 9, 2016
SIMBA YAPIGWA 2-1 NA PRISONS
TIMU kongwe ya soka ya Simba, jana, iliendelea kupunguzwa kasi ya kuwania taji la ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Prisons.
Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Simba ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipigo hicho ni cha pili mfululizo kwa Simba katika kipindi cha wiki moja. Mwishoni mwa wiki iliyopita, Simba ilichapwa bao 1-0 na African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pamoja na kupokea kipigo hicho, Simba imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi 35, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 30 na Azam yenye pointi 25.
Iliwachukua Simba dakika 43 kuhesabu bao lililofungwa na Jamal Mnyate baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa mpira wa krosi kutoka kwa Shizza Kichuya.
Prisons ilisawazisha dakika ya 47 kwa bao lililofungwa na Victor Hangaya baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa krosi kutoka kwa Salum Bosco.
Bao la pili la Prisons lilifungwa na Hangaya tena dakika ya 63 baada ya kuunganisha wavuni mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Mohammed Samatta.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment