MTUNZI na mwimbaji nyota wa zamani wa bendi ya Mlimani Park Orchestra, Shabani Dede, amesema yuko tayari kulinogesha onyesho la 'Usiku wa Sikinde', litakalofanyika Jumapili ijayo.
Akizungumza na Uhuru, mwishoni mwa wiki iliyopita, Dede alisema anachokihitaji ni kupata baraka kutoka kwa viongozi wake wa bendi ya Msondo Ngoma ili aweze kushiriki kwenye onyesho hilo.
"Sikinde ni bendi yangu, kama nahitajika kushiriki kwenye onyesho hilo, siwezi kuacha kufanya hivyo. Lakini itabidi nipate baraka za viongozi wangu,"alisema.
Mwimbaji huyo mkongwe, ambaye kwa sasa anaitumikia bendi ya Msondo Ngoma, amekuwa mwimbaji wa pili wa zamani wa Sikinde kuthibitisha kushiriki kwenye onyesho hilo. Mwingine ni kiongozi na mwimbaji wa bendi ya Talent, Hussein Jumbe.
Meneja wa Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti alisema hawana tatizo kumruhusu Dede kushiriki kwenye onyesho hilo, isipokuwa ni lazima awajulishe viongozi wenzake.
"Hatuna tatizo kwa hilo, lakini inabidi nikae na viongozi wenzangu kujadili suala hilo kabla ya kutoa ruhusa kwa Dede,"alisema Kibiriti.
Dede ni miongoni mwa watunzi mahiri wa zamani wa Sikinde, akiwa anashika nafasi ya pili kwa kutunga nyimbo nyingi, nyuma ya mkongwe Hassan Bitchuka.
Onyesho la Usiku wa Sikinde, ambalo limelenga kuwakumbusha mashabiki nyimbo za zamani za Mlimani Park Orchestra na mpya, linatarajiwa kufanyika kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.
Dede na Jumbe wanatarajiwa kushiriki kuimba nyimbo mbalimbali za zamani walizowahi kuzitunga na kuziimba walipokuwa Mlimani Park.
Mmoja wa waratibu wa onyesho hilo, Emmanuel Ndege, alisema jana kuwa, maandalizi yanakwenda vizuri, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwasaka wanamuziki wengine nyota wa zamani wa bendi hiyo, akiwemo mpiga gita la solo na rythim, Abdalla Gama.
Ndege alisema wameamua kuliita onyesho hilo kuwa la Usiku wa Sikinde, kwa sababu ni maalumu kwa watu maalumu, lengo likiwa ni kuwakumbusha mashabiki,enzi bendi hiyo ilipokuwa ikitamba kwa miondoko hiyo.
Aidha, Ndege alisema bendi hiyo pia itatumia fursa hiyo kutambulisha baadhi ya nyimbo zake mpya na zile zilizorekodiwa katika albamu ya hivi karibuni, inayojulikana kwa jina la Jinamizi la talaka.
Ndege alisema wakati wa onyesho hilo, kutatolewa zawadi mbalimbali kwa mashabiki watakaovutia kwa mavazi na kujimwayamwaya Kisikinde. Pia, alisema mashabiki watakaoingia ukumbini mapema, watapatiwa zawadi.
Mratibu huyo alisema onyesho hilo limedhaminiwa na Kampuni ya Isere Sports, inayojihusisha na uuzaji wa vifaa mbalimbali vya michezo, gazeti la Burudani na kituo cha Redio Uhuru.
Kiongozi wa bendi hiyo, Abdalla Hemba, aliwahakikishia mashabiki kwamba, watapata burudani murua na adimu, ambayo hawataisahau katika maisha yao.
No comments:
Post a Comment