'
Thursday, November 17, 2016
SIKINDE YAWAANDALIA MASHABIKI ONYESHO MAALUMU NOVEMBA 27, NI LA USIKU WA VITU ADIMU, LITAFANYIKA DDC KARIAKOO
BENDI ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra, imewaandalia mashabiki wake onyesho maalumu litakalojulikana kwa jina la 'Usiku wa Sikinde'.
Onyesho hilo, ambalo limelenga kuwakumbusha mashabiki nyimbo za zamani za bendi hiyo na mpya, linatarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu, kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.
Akizungumza mjini Dar es Salaam, jana, Mratibu wa onyesho hilo, Rashid Zahor, alisema maandalizi yote muhimu yanakwenda vizuri, ikiwa ni pamoja na bendi hiyo kuzifanyia mazoezi ya nguvu baadhi ya nyimbo za zamani.
"Hili ni onyesho maalumu kwa watu maalumu, ndio sababu tumelipa jina la 'Usiku wa Sikinde', kwa sababu tunataka kuwakumbusha mashabiki, zile enzi bendi ilipokuwa ikitamba kwa miondoko hiyo,"alisema Zahor.
Alizitaja baadhi ya nyimbo adimu zitakazopigwa kuwa ni pamoja na Celina, Maudhi, Taraka rejea, Clara, Christina Bundala, Hiba, Barua kutoka kwa mama, Chenga ya mwili, Dua la kuku, Sitokubali kuwa mtumwa, Mtoto akililia wembe, Cenjesta, Epuka jambo lisilokuhusu na nyinginezo.
Aidha, Zahor alisema bendi hiyo pia itatumia fursa hiyo kutambulisha baadhi ya nyimbo zake mpya na zile zilizorekodiwa katika albamu ya hivi karibuni, inayojulikana kwa jina la Jinamizi la talaka.
Nyimbo hizo ni Jinamizi la Talaka, Za mkwezi mbili, Nikipata nitalipa,
Kibogoyo, Dole gumba, Ng'ombe haelemewi, Nundu, Tabasamu, Supu umeitia nazi na Wali nazi.
Kwa mujibu wa Zahor, wakati wa onyesho hilo, mashabiki wataruhusiwa kuomba nyimbo watakazotaka kupigiwa na pia kutatolewa zawadi mbalimbali kwa watakaovutia kwa mavazi na kujimwayamwaya vizuri.
Mratibu huyo alisema onyesho hilo limedhaminiwa na Kampuni ya Isere Sports, inayojihusisha na uuzaji wa vifaa mbalimbali vya michezo, gazeti la Burudani na kituo cha Redio Uhuru.
Kwa upande wake, kiongozi wa bendi hiyo, Abdalla Hemba, aliwahakikishia mashabiki kwamba, watapata burudani murua na adimu, ambayo hawataisahau katika maisha yao.
Alisema wameshaanza kuzifanyia mazoezi baadhi ya nyimbo za zamani ili kuwapa mashabiki ladha halisi na kwamba, hakutakuwa na tofauti
licha ya wanamuziki wengi wa zamani kutokuwepo kwenye bendi hiyo kwa sasa.
Hemba amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenye onyesho hilo ili kuiunga mkono bendi yao, ambayo imekuwa mstari wa mbele kukuza na kuendeleza muziki wa dansi wa miondoko ya asili.
Aidha, kiongozi huyo wa Sikinde alisema watalitumia onyesho hilo kumkaribisha tena jukwaani mwimbaji nyota nchini, Hassan Bicthuka, ambaye alipumzika kutokana na kuwa mgonjwa.
Mlimani Park Orchestra ilianzishwa 1978 na lililokuwa Shirika la Usafiri na Huduma za Taksi (TTTS), kwa lengo la kutoa burudani kwa mashabiki. Shirika hili lilikuwa mali ya serikali.
TTTS iliacha kuiendesha bendi hiyo mwaka 1982, ikachukuliwa na Shirika la Uchumi na Maendeleo la Mkoa wa Dar es Salaam (DDC). Kuanzia wakati huo, bendi ilibadilishwa jina la kuitwa DDC Mlimani Park Orchestra.
Mwaka 2010, uongozi wa DDC uliamua kujitoa kuiendesha bendi hii na kukabidhi vyombo kwa wanamuziki ili waweze kujiendesha. Tangu wakati huo, bendi hii imekuwa ikiendeshwa na wanamuziki wenyewe na kuchagua viongozi kila baada ya miaka miwili.
Baadhi ya wanamuziki waliowahi kuiongoza bendi hii ni marehemu Michael Enock, Muhidin Gurumo, Bennovilla Anthony, marehemu Nasir Lubua, Shabani Dede, Hussein Jumbe, Habibu Abbas 'Jeff' na Hemba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment