KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, November 20, 2016

HUSSEIN JUMBE KUPAMBA ONYESHO LA USIKU WA SIKINDE

MWIMBAJI nyota wa muziki wa dansi nchini, Hussein Jumbe, amethibitisha kushiriki katika onyesho maalumu la 'Usiku wa Sikinde', lililopangwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.

Jumbe, ambaye kwa sasa anamiliki bendi ya Talent, alisema jana kuwa, atashiriki onyesho hilo kwa sababu bendi ya Mlimani Park Orchestra ni nyumbani kwake.

Onyesho hilo, ambalo limelenga kuwakumbusha mashabiki nyimbo za zamani za Mlimani Park na mpya, linatarajiwa kufanyika kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.

Jumbe alisema katika onyesho hilo, atashiriki kuimba nyimbo mbalimbali za zamani alizowahi kuzitunga na kuziimba alipokuwa bendi ya Mlimani Park.

Alizitaja baadhi ya nyimbo hizo kuwa ni Isaya mrithi wangu, Nachechemea, Hisia za Mwanadamu na Nuru ya Upendo.

Kwa upande wake, Mratibu wa onyesho hilo, Rashid Zahor, alisema maandalizi yote muhimu yanakwenda vizuri, ikiwa ni pamoja na bendi hiyo kuzifanyia mazoezi ya nguvu baadhi ya nyimbo za zamani.

"Hili ni onyesho maalumu kwa watu maalumu, ndio sababu tumelipa jina la 'Usiku wa Sikinde', kwa sababu tunataka kuwakumbusha mashabiki, zile enzi bendi ilipokuwa ikitamba kwa miondoko hiyo,"alisema Zahor.

Alizitaja baadhi ya nyimbo adimu zitakazopigwa kuwa ni pamoja na Celina, Maudhi, Taraka rejea, Clara, Christina Bundala, Hiba, Barua kutoka kwa mama, Chenga ya mwili, Dua la kuku, Sitokubali kuwa mtumwa, Mtoto akililia wembe, Cenjesta, Epuka jambo lisilokuhusu na nyinginezo.

Aidha, Zahor alisema bendi hiyo pia itatumia fursa hiyo kutambulisha baadhi ya nyimbo zake mpya na zile zilizorekodiwa katika albamu ya hivi karibuni, inayojulikana kwa jina la Jinamizi la talaka.

Nyimbo hizo ni Jinamizi la Talaka, Za mkwezi mbili, Nikipata nitalipa,Kibogoyo, Dole gumba, Ng'ombe haelemewi nundu, Tabasamu, Supu umeitia nazi na Wali nazi.

Kwa mujibu wa Zahor, wakati wa onyesho hilo, mashabiki wataruhusiwa kuomba nyimbo watakazotaka kupigiwa na pia kutatolewa zawadi mbalimbali kwa watakaovutia kwa mavazi na kujimwayamwaya vizuri. Pia, alisema mashabiki watakaoingia ukumbini mapema, watapatiwa zawadi ya bia moja bure.

Mratibu huyo alisema onyesho hilo limedhaminiwa na Kampuni ya Isere Sports, inayojihusisha na uuzaji wa vifaa mbalimbali vya michezo, gazeti la Burudani na kituo cha Redio Uhuru.

Kiongozi wa bendi hiyo, Abdalla Hemba, aliwahakikishia mashabiki kwamba, watapata burudani murua na adimu, ambayo hawataisahau katika maisha yao.

Alisema wameshaanza kuzifanyia mazoezi baadhi ya nyimbo za zamani ili kuwapa mashabiki ladha halisi na kwamba, hakutakuwa na tofauti
licha ya wanamuziki wengi wa zamani kutokuwepo kwenye bendi hiyo kwa sasa.

Hemba amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenye onyesho hilo ili kuiunga mkono bendi yao, ambayo imekuwa mstari wa mbele kukuza na kuendeleza muziki wa dansi wa miondoko ya asili.

Aidha, kiongozi huyo wa Sikinde alisema watalitumia onyesho hilo kumkaribisha tena jukwaani mwimbaji nyota nchini, Hassan Bicthuka, ambaye alipumzika kutokana na kuwa mgonjwa.

No comments:

Post a Comment