KIU ya Simba kutwaa tena taji la ligi kuu ya Tanzania Bara, imeendelea kujidhihirisha leo baada ya kuichapa Stand United bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Bao hilo la pekee na la ushindi la Simba lilifungwa na kiungo mshambuliaji, Shiza Kichuya kwa njia ya penalti dakika ya 33, baada ya Laudit Mavugo kuangushwa na beki Adeyum Ahmed wa Stand United ndani ya eneo la hatari.
Kutokana na ushindi huo, Simba imeendelea kujichimbia kileleni mwa ligi hiyo ikiwa na pointi 35 baada ya kucheza mechi 13. Stand inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 22 baada ya kucheza mechi 14.
Katika pambano hilo, timu zote mbili zilishambuliana kwa zamu na kupata nafasi kadhaa za kufunga mabao, lakini umaliziaji mbovu wa washambuliaji wake ulikuwa kikwazo.
Wakati huo huo, mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Azam leo wameendelea kufufua matumaini ya kutwaa taji hilo baada ya kuwachapa Toto African bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Bao pekee na la ushindi la Azam lilifungwa na mshambuliaji Shabani Iddi dakika ya 81 baada ya kupokea pasi kutoka kwa John Bocco.
No comments:
Post a Comment