MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Yanga leo wametepweta mbele ya Stand United, baada ya kuchapwa bao 1-0 katika mechi ya ligi kuu iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Bao pekee na la ushindi la Stand United lilipachikwa wavunu na mshambuliaji Pastory Athanas na hivyo kuiwezesha kutoka uwanjani na pointi zote tatu.
Kutokana na ushindi huo, Stand United, ambayo imekuwa ikikabiliwa na mgogoro wa uongozi kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, imefikisha pointi 12 baada ya kucheza mechi sita, ikiwa nyuma ya vinara Simba, wenye pointi 16.
Kwa upande wa Yanga, imeendelea kubaki na pointi 10 baada ya kucheza mechi sita.
Licha ya kushambuliana kwa zamu muda wote wa dakika 45 za kipindi cha kwanza, Yanga na Stand United zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.
Athanas aliifungia Stand bao hilo la pekee dakika ya 58 baada ya kuwatoka mabeki Haji Mwinyi na Vincent Bossou kabla ya kufumua shuti katikati yao, lililompita ubavuni kipa Ally Mustapha na mpira kutinga wavuni.
Japokuwa Stand United imekuwa ikikabiliwa na mgogoro wa uongozi, haijapoteza mechi hata moja tangu ligi hiyo ilipoanza msimu huu, ikiwa imeshinda mechi tatu na kutoka sare mechi tatu.
No comments:
Post a Comment