KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 11, 2016

MALINZI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI MSIBA WA SIANG’A

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea taarifa za kifo Kocha wa zamani wa Simba, James Aggrey Siang’a. Taarifa kutoka Kenya zinasema amefariki leo Septemba 10, 2016 alfajiri mjini Bungoma baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Siang’a alikuwa ni miongoni mwa makocha walioheshimika Afrika Mashariki hususani Tanzania alipoingoza Simba kufanya vema kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kufika hatua ya timu Nane Bora.

Kutokana na kifo hicho, Rais wa TFF Jamal Malinzi amemtumia salamu za rambirambi kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF), Nick Mwendwa akieleza kwamba ameshtushwa na kifo cha Siang’a.

Rais Malinzi mbali ya kutuma salamu FKF, pia alituma salamu za rambirambi kwa familia ya Marehemu Siang’a kadhalika ndugu, jamaa, majirani na marafiki huku akiwataka kuwa na moyo wa subira wakati huu mgumu wa msiba wa mpendwa wao.

Rais Malinzi amesema kwamba Siang’a ameacha alama ya wadau wa soka kujifunza na kukumbukwa daima baada ya kucheza mpira wa miguu kwa mafanikio makubwa akichezea Klabu za Gor Mahia, Luo Union na timu ya taifa Kenya Harambee Stars kama kipa, pia aliwahi kuwa kocha wa klabu za Simba, Moro United na Express ya Uganda kama kocha.

Kwa mujibu wa historia ya Siang’a aliidakia Kenya katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1972 na pia alikuwa kocha wa Harambee Stars mwaka 1999 na 2000, kabla ya kuhamia Tanzania kufundisha Simba, Mtibwa Sugar, Moro United na timu ya taifa ya Bara kwa muda mfupi mwaka 2002.

Kwa Tanzania, atakumbukwa na familia nzima ya Simba kutokana na kuipa timu taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati visiwani Zanzibar mwaka 2002, kabla ya kuunda kikosi imara cha vijana wadogo kilichokuwa tishio katika soka ya Tanzania miaka 14 iliyopita wakiwamo Steven Mapunda ‘Garincha’, Said Swedi, Ramazani Wasso, Boniface Pawasa, Victor Costa, Lubigisa Madata, Suleiman Matola, Primus Kasonzo, Christopher Alex, Shekhan Rashid, Ulimboka Mwakingwe, Emmanuel Gabriel na Athumani Machuppa.

Vijana hao ndio walioiwezeha Simba SC kuitoa Zamalek ya Misri waliokuwa mabingwa wa Afrika katika hatua ya 16 Bora na kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako awali walizitoa timu za BDF XI ya Botswana, Santos ya Afrika Kusini kabla ya Zamalek. Santos aliitoa kwa penalti 9-8 baada ya sare ya jumla 0-0 na Zamalek pia aliitoa kwa penaliti 3-2, baada ya sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Mzee Siang’a mahala pema peponi

No comments:

Post a Comment