YANGA imeendelea kung'ara katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Majimaji mabao 3-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mshambuliaji Amis Tambwe aliibuka shujaa wa Yanga baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matatu. Bao lingine lilifungwa na kiungo Deus Kaseke.
Kwa ushindi huo, Yanga sasa imefikisha pointi saba baada ya kucheza mechi tatu, ambapo imeshinda mbili, imetoka sare moja, kama ilivyo kwa timu kongwe ya Simba.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Azam ilitoka uwanjani na ushindi baada ya kuibugiza Mbeya City mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Ushindi huo uliiwezesha Azam kushinda mechi zote mbili ilizocheza Mbeya baada ya wiki iliyopita kuilaza Prisons bao 1-0 kwenye uwanja huo.
Kutokana na ushindi huo, Azam imeendelea kujikita kileleni mwa ligi hiyo, ikiwa na pointi 10 baada ya kucheza mechi nne wakati Mbeya City inazo pointi saba.
Mabao ya Azam yalifungwa na Khamis Mcha na Gonazo Thomas. Bao la Mbeya City lilifungwa na Rafael Daudi.
Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa juzi, Ruvu Shooting iliwalaza maafande wenzao wa JKT kwa bao 1-0, Mwadui ilitoka sare ya mabao 2-2 na majirani zao wa Stand United wakati Ndanda FC na Kagera Sugar zilitoka suluhu.
No comments:
Post a Comment