WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya klabu bingwa Afrika, Yanga wamefuzu kucheza raundi ya pili ya michuano hiyo baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na APR ya Rwanda.
Sare hiyo iliyopatikana jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, imeiwezesha Yanga kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2, kufuatia kushinda mechi ya awali mjini Bujumbura kwa mabao 2-1.
Kwa ushindi huo, Yanga sasa itakutana na Al Ahly ya Misri katika mechi ya raundi ya tatu.
Al Ahly imetinga hatua hiyo baada ya kuitoa Recreativo do Libolo ya Angola kwa jumla ya mabao 2-0. Katika mechi ya awali, timu hizo zilitoka suluhu mjini Luanda.
APR ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya tatu lililofungwa na Fiston Nkinzingabo aliyefumua shuti kali akimalizia pasi ya Jean Claude Iranzi.
Yanga walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 28 kupitia kwa mshambuliaji wake, Donald Dombo Ngoma, aliyefumua shuti la kitaalamu baada ya pasi nzuri ya kiungo Mzimbabwe mwenzake, Thabani Scara Kamusoko.
Pambano kati ya Yanga na Al Ahly linatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi wa soka nchini, kutoka na timu hiyo ya Tanzania kuwa na rekodi ya kufungwa kila inapokutana na timu za Misri.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana mwaka 2014, katika raundi ya kwanza na Yanga ikatolewa kwa penalti 4-3, baada ya sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
Kwa mujibu wa ratiba, mechi ya kwanza itachezwa Aprili 9, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati marudiano yatakuwa Aprili 19 mjini Cairo.
No comments:
Post a Comment