WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya klabu za Afrika, Yanga na Azam jana walijiweka kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya APR ya Rwanda na Bidvest ya Afrika Kusini.
Wakati Yanga iliichapa APR mabao 2-1 katika mechi ya michuano ya klabu bingwa Afrika iliyochezwa mjini Kigali, Azam iliitandika Bidvest mabao 3-0 katika mechi ya michuano ya Kombe iliyochezwa mjini Johannesburg.
Timu hizo nne zinatarajiwa kurudiana wiki mbili zijazo mjini Dar es Salaam, huku Yanga na Azam zikiwa zinahitaji sare ya aina yoyote ili ziweze kusonga mbele.
Beki Juma Abdul na kiungo Thabani Kamusoko ndio walioiwezesha Yanga kutoka uwanjani wakiwa wababe baada ya kuifungia mabao hayo mawili.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na Duncan Lengani, aliyesaidiwa na washika vibendera Clemence Kanduku na Jonizio Luwizi wote wa Malawi, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na Juma Abdul Jaffar dakika ya 20 kwa shuti la mpira wa adhabu ndogo umbali wa mita 30, baada ya Haruna Niyonzima kuangushwa.
Kamusoko aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 74, akimalizia pasi ya mshambuliaji Donald Dombo Ngoma.
APR ilipata bao la kujifariji dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za kawaida lililofungwa na Patrick Sibomana.
Nayo Azam ilijipatia mabao yake matatu kupitia kwa kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dakika ya 51, beki Shomary Kapombe dakika ya 56 na mshambuliaji na Nahodha John Bocco ‘Adebayor’ dakika ya 59.
Wawakilishi wengine wa Tanzania, JKU ya Zanzibar wamefungwa mabao 4-0 na wenyeji SC Villa katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza Kombe la Shirikisho, uliochezwa kwenye Uwanja wa Mandela, Kampala, Uganda.
Mabao ya Villa yalifungwa na Mike Ndera, Mike Serumaga, Umar Kasumba na Godfrey Lwesibawa.
No comments:
Post a Comment