KAMA ilivyotarajiwa, Simba SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 3-0 jioni ya leo dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shukrani kwao, wafungaji wa mabao hayo, kiungo Mwinyi Kazimoto Mwitula kipindi cha kwanza na mshambuliaji Mganda, Hamisi Friday Kiiza mawili kipindi cha pili.
Simba SC sasa inafikisha pointi 51 baada ya kucheza mechi 22 na kuwashushia nafasi ya pili, mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 50 za mechi 21.
Simba walipata bao lao la kwanza dakika ya 35, baada ya Kazimoto kutuliza vizuri krosi ya Ibrahim Hajib iliyowapita kipa wa Ndanda, Jeremiah Kisubi na mabeki wake na kufumua shuti la kiufundi la juu lililotinga nyavuni.
Mshambuliaji wa Uganda, Kiiza akaipatia Simba bao la pili dakika ya 57 kwa kichwa akimalizia kona ya Hajib, hilo likiwa bao lake la 17 msimu huu katika Ligi Kuu na kumfikia mshambuliaji wa Yanga, Mrundi Amissi Joselyn Tambwe aliyekuwa anaongoza.
Kiiza akafunga bao lake la 18 msimu huu wa Ligi Kuu dakika ya 73 na kumpiku Tambwe, akimalizia pasi ya mshambuliaji Danny Lyanga aliyeuwahi mpira uliotemwa na kipa Jeremiah Kisubi kufuatia shuti kali la mpira wa dhabu la kiungo Mzimbabwe, Justive Majabvi.
Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, Mbeya City
Imeifunga 2-0 Stand United Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, mabao ya Raphael Daudi na Haruna Shamte.
CHANZO CHA HABARI: BLOGU YA BINZUBEIRY
No comments:
Post a Comment