KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, February 27, 2015

NGASA AIPAISHA YANGA KOMBE LA SHIRIKISHO




BAO lililofungwa na mshambuliaji Mrisho Ngasa jana liliiwezesha Yanga kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Afrika baada ya kuitoa BDF ya Sudan.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa Lobatse, BDF iliichapa Yanga mabao 2-1.

Pamoja na kupata kipigo hicho, Yanga imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2 kufuatia kushinda mechi ya awali wiki mbili zilizopita kwa mabao 2-0.

Timu hizo zilikwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Ngasa dakika ya 30, akiunganisha wavuni kwa kichwa pasi kutoka kwa Amis Tambwe.

BDF ilikianza kipindi cha pili kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 49 kupitia kwa Mosimanyana, aliyemalizia pasi kutoka kwa Lerore.

Yanga ilipata pigo dakika ya 72 baada ya mshambuliaji wake Danny Mrwanda kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Madziba.

Bao la pili la BDF lilifungwa na Kumbulani Madziba dakika ya 85, aliyewatoka mabeki wa Yanga na kufumua shuti lililompita kipa Ally Mustafa Barthez.

Wakati huo huo, wawakilishi  wa Tanzania katika michuano ya klabu bingwa Afrika, Azam leo wanashuka dimbani mjini Khartoum kurudiana na El Merreikh.

Katika mechi hiyo, Azam inahitaji sare ya aina yoyote ili iweze kusonga mbele kufuatia kushinda mechi ya awali mjini Dar es Salaam kwa mabao 2-0.

No comments:

Post a Comment