'
Sunday, February 22, 2015
MTIBWA SUGAR SASA CHOKA MBAYA
MABINGWA wa zamani wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wameendelea kufanya vibaya licha ya kuanza msimu kwa kishindo, baada ya leo kufungwa bao 1-0 na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Matokeo hayo, yanaifanya Mgambo itimize pointi 20 baada ya kucheza mechi 15 na kupanda hadi nafasi ya sita kutoka ya 11, wakati Mtibwa inabaki na pointi zake 19 za mechi 16.
Bao pekee la Mgambo JKT jioni ya leo limefungwa na Balimi Busungu dakika ya 27, akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Salim Kapinga.
Wakati huo huo, Kagera Sugar wamepanda hadi nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa bao 1-0 jioni ya leo dhidi ya Polisi Moro Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Kagera wanafikisha pointi 27 baada ya kucheza mechi 17, wakiwashushia nafasi ya tatu mabingwa watetezi, Azam FC wenye pointi 26 za mechi 14. Yanga SC yenye pointi 28 za mechi 14, inaongoza Ligi Kuu.
Bao pekee Kagera leo limefungwa na mshambuliaji wa ‘Taifa Stars Maboresho’, Rashid Mandawa.
Katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, wenyeji Ndanda wameshinda 1-0 dhidi ya Coastal Union, bao pekee la Nassor Kapama
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment