'
Monday, February 2, 2015
DRFA YAIFAGILIA TEMEKE KUTWAA KOMBE LA TAIFA LA WANAWAKE
Chama cha kandanda mkoa wa Dar es salaam DRFA, kimeipongeza timu ya Temeke kwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Taifa la Wanawake,baada ya kuifunga Pwani kwa bao 1-0,kwenye mchezo wa fainali uliopigwa Jumapili iliyopita kwenye uwanja wa Azam Complez, Chamazi.
Katika fainali hiyo iliyohudhuriwa na Waziri mwenye dhamana ya michezo Dk.Fenella Mukangara,Temeke ilijipatia bao lake dakika ya 66 kupitia kwa mchezaji wao Neema Paul.
Temeke walifanikiwa kutinga hatua ya fainali baada ya kuwafunga ndugu zao Ilala kwa mabao 4-0,huku Pwani wakitinga hatua hiyo kwa kuifunga Kigoma mabao 3-2.
Mshindi amejinyakulia kitita cha shilingi milioni tatu, makamu bingwa sh. milioni mbili, wakati mshindi wa tatu ameondoka na sh. milioni moja.
Mbali na Temeke kubeba ubingwa,pia imefanikiwa kutoa mlinda mlango bora, Belina Julius aliyezawadiwa kitita cha shilingi 500,000/-.
Mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu uliwakutanisha, Ilala dhidi ya Kigoma, ambapo Ilala ilifanikiwa kuchukua nafasi ya tatu baada ya kushinda mabao 3-0.
Uongozi wa DRFA,unatoa shukurani kwa mashabiki wa mkoa wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani,ambao wamejitokeza kwa wingi kushuhudia michuano hiyo na kuwaomba waendelee kuwa na moyo huo ili kuongeza hamasa kwa wachezaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment