'
Monday, February 2, 2015
FRANCIS CHEKA AFUNGWA JELA
NA LATIFA GANZEL, MOROGORO,
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, imemhukumu bondia nguli nchini, Francis Cheka, kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la shambulio na kudhuru mwili.
Cheka alihukumiwa kifungo hicho jana baada ya Hakimu Mkazi, Said Msuya, kumtia hatiani kwa kosa la kumshambulia na kumdhuru mwili aliyekuwa Meneja wa baa yake, Bahati Kabanda.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Cheka anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 2, mwaka jana, katika eneo la kata ya Uwanja wa Taifa, Manispaa ya Morogoro.
Bondia huyo anadaiwa kumpiga aliyekuwa meneja wa baa yake ilijulikanayo kwa jina la Vijana Social Hall na kusababisha kumdhuru sehemu mbalimbali za mwili.
Akisoma hukumu hiyo, Hakima Msuya alisema mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela na baada ya kumaliza kutumikia adhabu hiyo, atatakiwa kumlipa mlalamikaji gharama ya sh. milioni moja ya matibabu alizojitibia baada ya kupigwa na bondia huyo.
Akizungumza baada ya kupewa adhabu hiyo, Cheka alidai kuna mkono wa watu wenye lengo la kutaka kuchafua jina lake na maisha yake .
Cheka alidai kushangazwa kusomewa kuwa alikiri kosa la kumpiga mlalamikaji wakati yeye katika maelezo yake alikana shitaka.
"Ni wazi kesi yangu ilipangwa kuvurugwa ili nifungwe na kunipoteza katika ulimwengu wa masumbwi," alidai.
Kocha wa bondia huyo, Abdallah Komando, alidai kuwa kifungo cha bondia wake kimemtia simanzi kubwa, kwa kuwa kesi hiyo ingeweza kumalizika mezani.
Komando alisema kifungo cha bondia wake ni matokeo ya fitna za kimichezo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment