YANGA jana ilianza vibaya kampeni ya kuwania ubingwa wa michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar.
Katika mechi hiyo iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, mshambuliaji Genilson Jaja aliikosesha Yanga bao baada ya kupoteza penalti katika kipindi cha kwanza.
Mtibwa ilipata bao la kuongoza dakika ya 15 kupitia kwa mshambuliaji wake, Mussa Hassan 'Mgosi' baada ya kupokea pasi kutoka kwa Shaaban Nditi.
Yanga ilipata penalti dakika ya 46 baada ya Mrisho Ngasa kumnawisha mpira beki Saidi Mbonde wa Mtibwa. Hata hivyo, shuti la jaja liliokolewa kwa mguu na kipa Saidi Mohamed kabla ya mabeki wake kuuondosha kwenye hatari.
Zikiwa zimesalia dakika tano pambano hilo kumalizika, jahazi la Yanga lilizidi kuzama baada ya Ali kuifungia Mtibwa bao la pili kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Nditi.
Wakati huo huo, mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Azam jana walianza vyema kutetea taji lao baada ya kuichapa Polisi Moro mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mabao yaliyoiwezesha Azam kutoka uwanjani na ushindi huo mnene yalipachikwa wavuni na Didier Kavumbagu, aliyefunga mawili na Aggrey Morris.
Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa juzi, Ndanda FC iliibamiza Stand United mabao 4-1, Mgambo JKT iliichapa Kagera Sugar bao 1-0, Ruvu Shooting ilipigwa mweleka wa mabao 2-0 na Prisons wakati Mbeya City ilitoka suluhu na JKT Ruvu.
No comments:
Post a Comment