'
Wednesday, September 3, 2014
SIMBA KUJIPIMA KWA GOR MAHIA NA APR, YANGA USO KWA USO NA THIKA UNITED LEO
TIMU kongwe ya soka nchini, Simba mwishoni mwa wiki hii itacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Gor Mahia ya Kenya. Mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, maandalizi ya mechi hiyo yanaendelea vizuri, timu ikiwa kambini Zanzibar, chini ya Kocha wake mzoefu, Patrick Phiri kutoka Zambia.
Kwa mujibu wa habari hizo, Simba huenda ikacheza mechi nyingine ya kirafiki ya kimataifa wiki ijayo kwa kumenyana na APR ya Rwanda.
Mechi dhidi ya Gor Mahia itapigwa Jumamosi wakati mechi dhidi ya APR itapigwa Jumatano ijayo kwenye uwanja huo.
Wakati huo huo, Yanga leo inacheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa ya kirafiki kwa kumenyana na Thika United ya Kenya.
Mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Taifa na itakuwa ya kwanza kwa Kocha mpya wa Yanga, Marcio Maximo kutoka Brazil tangu alipoanza kuinoa timu hiyo.
Mechi hiyo itakuwa kipimo kizuri kwa Yanga, ambayo imeshacheza mechi tatu za kirafiki dhidi ya Chipukizi, Shangani na KMKM za Zanzibar na kuibuka na ushindi.
Mechi hiyo itachezwa kuanzia saa 11:00 jioni kwa saaa za Afrika Mashariki ili kutoa fursa kwa wafanyakazi wa maofisini na taasisi mbalimbali waweze kuwahi na kushuhudia mchezo huo.
Viingilio vya mchezo huo ni:
VIP A Tshs 30,000/=
VIP B & C Tshs 20,000/=
Orange Tshs 10,000/=
Bluu & Kijanni Tshs 5,000/=
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment