'
Thursday, September 25, 2014
KATIBA MPYA KUWATAMBUA WASANII
Msanii wa filamu nchini Tanzania maarufu kama Mzee Chilo akiwa katika picha ya pamoja na mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Angellah Kairuki jana katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Kiongozi wa msafara wa wasanii waliofika katika Bunge Maalumu la Katiba,Simon Mwakifwamba akiwa katika picha ya pamoja na mjumbe wa bunge hilo, Angellah Kairuki katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Baadhi ya Wasanii wakijadiliana jambo mara baada ya kutoka nje ya Bunge Maalumu la Katiba jana mjini Dodoma.
Baadhi ya wasanii wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Fenella Mukangara (wa pili toka kushoto) wakati alipokutana nao maeneo ya viwanja vya bunge hilo.
Wasanii wakiendelea kumsikiliza Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Fenella Mukangara wakati alipokutana nao maeneo ya viwanja vya bunge hilo jana mjini Dodoma.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Fenella Mukangara akiwa katika picha ya pamoja na wasanii maeneo ya viwanja vya bunge hilo jana mjini Dodoma.
Na Happiness Mtweve, Dodoma
HATIMAYE Bunge Maalumu la Katiba, limeridhia mapendekezo ya kuboresha Rasimu kuhusu kuanzishwa kwa Ibara mpya inayohusu uhuru wa taaluma, ubunifu na ugunduzi.
Akiwasilisha Rasimu ya Katiba Mpya iliyopendekezwa na Bunge hilo mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge, alisema hayo ni moja ya mapendekezo kutoka makundi mbalimbali yaliyoridhiwa.
“Kamati ya Uandishi, imekubaliana na pendekezo hilo na imeanzisha Ibara mpya ya 48 A inayohusu uhuru wa taaluma, ubunifu na ugunduzi ili kutoa fursa ya mtu kujifunza, kufundisha, kutafiti na kueneza matumizi ya matokeo ya utafiti kulingana na kanuni za kitaaluma na za kiutafiti,” alisema Chenge.
Aidha, alisema serikali imepewa mamlaka ya kulinda hakimiliki za ugunduzi na ubunifu, ikiwa ni pamoja na haki za wabunifu na watafiti nchini kwa manufaa ya Taifa.
Mwenyekiti huyo pia alisema Kamati ya Uandishi imependekeza kuongezwa kwa aya mpya ya (f) inayoweka masharti kwa serikali kukuza na kuendeleza utafiti inayoeleza: “Mambo mengine yanayohusu ubunifu, ugunduzi na utafiti.”
Hatua hiyo ni mwanzo wa mafanikio kwa wasanii wa fani mbalimbali nchini, ambapo sasa wataweza kunufaika kutokana na kulindwa na kutambulika kwa kazi zao.
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Martha Mlata, akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge jana, alieleza kufurahishwa na Katiba Inayopendekezwa, kuwatambua wasanii kwa kuwa kilikuwa kilio chake cha muda mrefu ndani na nje ya Bunge.
Alisema kwa muda mrefu wasanii nchini wamekuwa wakipambana kufanya kazi kwa ajili ya kuinuka kiuchumi, lakini wamekuwa wakikwamishwa kutokana na kunyonywa, hivyo kutopata kile wanachostahili, jambo ambalo kwa sasa limeangaliwa kwa umakini.
"Nimefarijika mno kuwepo kwa mapendekezo ya kutambua wasanii na kazi zao za sanaa...ni muda mrefu sana nimekuwa nikililia hili kwa manufaa ya wasanii wote nchini. Nawaomba wasanii waungane kuhakikisha wanatetea na kuipigia kura katiba hii ili kuhakikisha inapita," alisema Martha, ambaye amekuwa mstari wa mbele kutetea haki za wasanii nchini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment