KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 25, 2014

NYOTA WATANO WA KIGENI SIMBA WAPIGWA MARUFUKU KUCHEZA LIGI KUU, HAWANA VIBALI VYA KUFANYAKAZI, HATARINI KUIKOSA YANGA OKTOBA 12




Mshambuliaji wa Simba raia wa Uganda, Emmanuel Okwi na wenzake wanne wanaweza kuwa wameiingiza klabu hiyo kwenye mgogoro mkubwa; hawana kibali cha kufanya kazi nchinilicha ya kutumiwa kwenye mechi za ufunguzi wa Ligi Kuu mwishoni mwa wiki.

Idara ya Uhamiaji ilisema jana kuwa Okwi, Joseph Owino, Pierre Kwizera, Amis Tambwe na Raphael Kiongera hawana kibali cha kufanya kazi nchini, ambacho ni moja ya masharti makubwa ya kupata leseni ya kusakata soka.

Mbali na wachezaji hao, kocha Patrick Phiri pia haruhusiwi kukaa kwenye benchi la ufundi kwa kuwa naye hana kibali cha kufanya kazi nchini.

Akizungumza na gazeti hili jana, naibu kamishna wa Uhamiaji ambaye pia ni msemaji wa Idara hiyo, Abbas Mussa Irovya alisema nyota hao wa kigeni wa Simba hawaruhusiwi kuingia uwanjani wala kufanya mazoezi mahali popote hapa nchini na watakapoonekana wakifanya kazi kuanzia leo, watakamatwa.

“Tayari idara imemuagiza Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwakamata kuanzia kesho (leo) endapo wataonekana uwanjani aidha kwenye mechi au kwenye mazoezi na sheria itachukua mkondo wake,” alisema Irovya.

“Hatujapokea ombi lolote la klabu ya Simba kumuombea kibali mchezaji wala kocha wao wa kigeni ili afanye kazi hapa nchini na uwepo wao katika majukumu ya mazoezi au mechi ni kinyume cha sheria,” aliongeza msemaji huyo na kueleza kushangazwa na kitendo cha TFF kuwaachia waendelee kucheza wakati ikijua fika kuwa hawana kibali.

Okwi alikuwa na kibali cha kufanya kazi nchini alichoombewa na Yanga mwaka jana na baada ya kuidhinishwa Simba, klabu hiyo inatakiwa kumuombea kibali kipya.

“Tunamtambua Okwi kama muajiriwa wa klabu ya Yanga kwa kuwa ana kibali cha kufanya kazi hapa nchini chenye namba 1027397 kinachokwisha Machi 3, 2016 kilichoombwa na Yanga na siyo Simba alipo sasa,” alisema.

“Inachokifanya Simba ni kinyume cha sheria za nchi na za Idara ya Uhamiaji... kumwajiri mtu ambaye ana kibali cha kufanya kazi Yanga bila kutoa taarifa uhamiaji ni kukiuka taarifa za uhamiaji.”

Kwa mujibu wa kifungu cha 43 cha Kanuni za Ligi, mchezaji hawezi kupewa leseni ya kucheza soka nchini hadi atimize masharti mawili; kufanikiwa katika vipimo vya afya na kuwa na kibali cha kufanya kazi.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, kaimu katibu mkuu wa TFF, Boniface Wambura alijibu: “Wewe umeongea na Simba, wanasemaje?” na baadaye kumtaka mwandishi kuwasiliana na katibu mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa ambaye hakupatikana.

Kwa mujibu wa Irovya, Yanga ilishapeleka maombi ya vibali vya wachezaji wake kutoka Brazil, Genilson Santos ‘Jaja’ na Andrey Coutinho na makocha wao wawili kutoka nchi hiyo pia, Marcio Maximo na Leonardo Neiva na wako kwenye utaratibu wa kupata vibali hivyo

No comments:

Post a Comment