KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 14, 2014

YANGA, AZAM KAZI IPO LEO NGAO YA JAMII



PAZIA la Ligi Kuu ya Tanzania Bara litafunguliwa leo kwa mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii kati ya mabingwa wa msimu uliopita, Azam na washindi wa pili, Yanga utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni.

Yanga itaingia uwanjani huku ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii msimu uliopita. Bao hilo la pekee lilifungwa na Salum Telela.

Kocha Mkuu wa Yanga, Marcio Maximo, ambaye atakuwa akiongoza Yanga kwa mara ya kwanza katika ligi, amesema vijana wake wote wapo katika hali nzuri, jambo linalompa wigo mpana wa kuchagua nani amtumie katika mchezo huo.

Mpaka sasa Maximo ameiongoza Yanga katika michezo minne ya kirafiki, akifanikiwa kushinda michezo yote, ambapo aliibuka na ushindi 1-0 (Chipukizi FC), 2-0 (Shagani FC), 2-0 (KMKM) na 1-0 (Thika United) kutoka nchini Kenya.

Katika mazoezi ya mwisho yaliyofanyika jana asubuhi katika uwanja wa shule ya Sekondari Loyola, mchezaji pekee ambaye hakuweza kufanya mazoezi ni Jerson Tegete, anayesumbuliwa na nyonga wakati Andrey Coutinho alifanya mazoezi mepesi chini ya usimamizi wa daktari wa timu, Suphian Juma.

Jumla ya wachezaji 26 wa Yanga wameendelea kuwepo kambini kujiandaa na mchezo huo katika Hoteli ya Tansoma iliyoko eneo la Gerezani, Kariakoo, Dar es Salaal.

Wachezaji hao ni walinda mlango: Juma Kaseja, Ally Mustafa "Barthez" na Deo Munish "Dida"
Walinzi wa Pembeni: Juma Abdul, Salum Telela, Oscar Joshua, Edward Charles na Amos Abel
Walinzi wa kati: Kelvin Yondani, Rajab Zahir, Pato Ngonyani na Nadir Haroub "Cannavaro"
Viungo: Mbuyu Twite, Hassan Dilunga, Omega Seme, Hamis Thabit, Nizar Khalfani, Haruna Niyonzima na Said Juma "Makapu"
Washambuliaji: Saimon Msuva, Mrisho Ngasa, Huseesin Javu, Said Bahauzi, Andrey Coutinho, Geilson Santana "Jaja" na Hamis Kizza "Diego"

Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Azam, Joseph Marius Omog amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa leo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga SC.

Omog amesema japokuwa atamkosa nahodha wake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’, lakini anaamini wachezaji waliobaki wana uwezo wa kuiwezesha Azam FC kutwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya kwanza.

“Tuko tayari, vijana wapo katika hali nzuri kuelekea mchezo huo muhimu wa mwanzo wa msimu. Nitamkosa nahodha John (Bocco), lakini nina imani kubwa na wachezaji waliopo,”amesema Mcameroon huyo.

Bocco anasumbuliwa na maumivu ya nyama aliyoyapata katika mchezo wa robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwezi uliopita mjini Kigali, Rwanda.

Akiwazungumzia wapinzani wao, Omog amesema anaiheshimu Yanga SC ni timu kongwe na yenye historia katika soka ya Tanzania na anatarajia mchezo utakuwa mgumu, lakini wamejiandaa kikamilifu kushinda.

Tayari TFF ilishatangaza viingilio vya mchezo huo kuwa ni Tshs 30,000 (VIP A) Tshs 20,000 (VIP B & C) Tshs 10,000 (Rangi ya Chungwa) na Tshs 5,000 (Bluu & Kijani).

No comments:

Post a Comment