KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, December 1, 2016

SAKATA LA HASSAN KESSY LAZIDI KUIUMIZA KICHWA TFF



Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ilikutana jana Jumapili Novemba 27, 2016 kwenye Ukumbi wa Mikutano ya Bodi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia mashauri manane.

Shauri la 1. Klabu ya Simba dhidi ya Young Africans na mchezaji Hassan Hamis Ramadhani Kessy

Shauri hili sasa limerudi rasmi kwenye meza ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji. Kamati iliyoketi chini ya Makamu Mwenyekiti, Mwanasheria Raymond Wawa imekubali shauri hilo kurejea kwenye Kamati yake na imeahidi kutoa maamuzi ndani ya wiki hii.

Shauri la 2. Malalamiko ya Ayoub Nyenzi na wenzake

Shauri hili pia limepangwa kusikilizwa mwishoni mwa wiki hii. Uongozi wa Young Africans, umeagizwa kuleta nyaraka/kesi inayodai kuwa viongozi hao waliofukuzwa uanachama na Mkutano Mkuu wa dharura ama walishiriki au walifungua shauri mahakamani.

Uongozi wa Young Africans, chini ya Kaimu Katibu Mkuu Baraka Deusdedit ulikubali kuwasilisha nyaraka hizo kabla ya kikao kijacho kinachotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii. Wenzake na Nyenzi ni Hashim Abdallah na Salum Mkemi.

Shauri la 3. Klabu ya Simba na Kocha Amatre Richard

Kamati ilijikita kwenye hukumu yake na kuitaka Sekretarieti ya TFF kuandikia Simba kuhusu msimamo wa hukumu iliyotolewa kwa Simba kumlipa kocha huyo.

Shauri la 4. Malalamiko ya Young Africans dhidi ya Kagera Sugar

Wahusika kwenye shauri hili, wameamuliwa kwenda Dar es Salaam mbele ya kikao kitakachoitishwa mwishoni mwa wiki ili kujieleza. Wahusika hao ni Young Africans waliowasilisha malalamiko, Panone FC ya Kilimanjaro, Kagera Sugar pamoja na mchezaji husika ili hatua stahiki zichukuliwe mara baada ya kuwasikiliza.

Shauri la 6. Malipo ya wachezaji Jerry Tegete, Omega Seme na Thabit Mohammed

Kamati iliamua utekelezwa ufanyike kwa Klabu ya Young Africans kuwalipa wachezaji hao kama uamuzi ulivyokwisha kutoka hapo awali. TFF iandikie barua Young Africans kuhakikisha inawalipa.

Shauri la 7. Madai ya Mchezaji Said Bahanuzi dhidi ya Young Africans.

Suala la Bahanuzi limesogezwa mbele basi kwa kwa kuwa halikujadiliwa.

Shauri la 8. Mchezaji Said Hussein Morald

 Mchezaji huyo kwa sasa ni huru baada ya yeye na Klabu ya Singida Unitedf kufikia mwafaka kwa barua ambazo waliwasilisha mbele ya kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji.

KAMATI YA NIDHAMU YAIFUTIA ADHABU KIMONDO



Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limefuta adhabu iliyotolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya Saa 72) kwa viongozi na wachezaji wa Kimondo.

Kamati ya Saa 72, ilifanya tathmini ya mchezo huo Na. 23 kati ya Kurugenzi na Kimondo ambako iliamua kuwafungia viongozi wa Kimondo, Eric Ambakisye, Selestine Mashenzi, na Mussa Minga kwa miezi sita na kupigwa faini ya Sh. 500,000 kila mmoja.

Walidaiwa kuwafuata waamuzi hotelini baada ya mechi ambapo walimpiga Mwamuzi Mussa Gabriel na kumjeruhi wakishirikiana na baadhi ya wachezaji ambao waliohusika katika tukio hilo wamefungiwa mechi sita na faini ya sh. 500,000 kila mmoja.

Wachezaji waliotajwa ni January Daraja Mwamlima, Daniel Douglas Silvalwe, Abiud Kizengo na Monte Stefano Mwanamtwa. Adhabu zote ni kwa mujibu wa Kanuni ya 24(6) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Hata hivyo, katika kikao chake Jumapili iliyopita, Kamati ya Nidhamu ya TFF, chini ya Mwenyekiti Tarimba Abbas ilikubaliana na hoja ya wapinga adhabu waliowasilisha malalamiko yao TFF mara baada ya kuadhibiwa na Kamati ya Saa 72.

Hoja za viongozi wa Kimondo ni kuwa hakuwahi kuitwa mbele ya Kamati hiyo kuhusiana na jambo hilo kwa ajili ya kutoa utetezi wake na kuwa na shaka na kamati hiyo juu ya kutoa adhabu hiyo.

Kamati ya Nidhamu ilikubaliana na hoja hizo na hivyo kufuta adhabu hizo na kuagiza kamati ya saa 72 ya Bodi ya Ligi Kuu kuandikia kamati ya Nidhamu kuhusu makosa hayo ili kusikilizwa upya.

MWANSASU AITA 12 KUIVAA UGANDA DESEMBA 9

Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu unaochezwa ufukweni (Beach Soccer), John Mwansasu ameita kikosi cha wachezaji 12 kati ya 13 wanaotarajiwa kuivaa Uganda katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Desemba 9, 2016 utakaofanyika Dar es Salaam.

Mwansasu ambaye hivi karibuni kikosi chake kilicheza na Ivory Coast katika michezo miwili ya  kuwania nafasi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa soka la ufukweni bila mafanikio ni makipa  ambao ni  Rajab Galla na Khalifa Mgaya.

Mabeki ni Roland Revocatus, Juma Ibrahim, Kashiru Salum na Mohammed Rajab wakati Viungo ni Mwalimu Akida, Ahmada Ali na Samwel John huku washambuliaji wengine wakiwa ni Kassim Kilungo na Talib Ally pamoja na Ally Rabbi ambaye ni Nahodha na Mshambulaji wa timu hiyo.

Kocha John Mwansasu bado anafuatilia viwango vya wachezaji mbalimbali ili kujaza nafasi moja ya kipa kabla ya Desemba mosi, 2016 baada ya Kipa Juma Kaseja kutoa taarifa kuwa atakuwa na udhuru wakati nyota mwingine, Mohammed Banka aliyeripotiwa kuwa safarini nchini Afrika Kusini.

TFF YAKANA KUANZISHA MASHINDANO MAPYA MWEZI HUU



Zimekuweko taarifa mbalimbali kwenye vyombo vya habari na mitandao kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeandaa shindano maalum mwezi Desemba.

Mwezi Desemba hakuna shindano lolote jipya  litakalaondaliwa na TFF zaidi ya mashindano yake ya kawaida ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara (VPL) na Azam Sports Federation Cup  (ASFC).

Michuano mingine inayosimamiwa na TFF ni Ligi Kuu ya Taifa ya Wanawake (TWPL), Ligi Kuu ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 (TFFU20L), Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Ligi Daraja la Pili (SDL) na Ligi ya Mabingwa wa  Mikoa (RCL).

Ikumbukwe tu kwamba kwa sasa, timu za VPL ziko likizo na ni wakati wa Klabu kufanya mchakato wa usajili wa Dirisha Dogo. Duru la pili lenye mizunguko 15 inatarajiwa kuanza Desemba 17, 2016 kama ilivyopangwa hapo awali.

USIKU WA SIKINDE HAIJAPATA KUTOKEA








BENDI ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra, juzi iliwapa mashabiki wake burudani murua na adhimu wakati ilipofanya onyesho maalumu la Usiku wa Sikinde.

Katika onyesho hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam, kuanzia saa moja hadi saa sita usiku, mashabiki lukuki waliofurika kwenye ukumbi huo walirejea nyumbani wakiwa roho kwatu kutokana na kupata burudani ya vitu adimu.

Ikiongozwa na mwimbaji mkongwe, Abdalla Hemba, akisaidiwa na Karama Regesu, Hassan Kunyata na Musemba wa Minyigu, bendi hiyo kongwe ilianza onyesho hilo kwa kuporomosha vibao vyake vilivyowahi kutamba mwishoni mwa miaka ya 1970.

Kutokuwepo kwa mtunzi na mwimbaji mkongwe, Hassan Bitchuka, ambaye alikuwa mgonjwa, kulizua maswali mengi, lakini pengo lake lilizibwa vyema na Karama na Musemba.

Vibao vilivyotia fora na kuwakuna mashabiki ni pamoja na Taksi driver, Maudhi maudhi na Neema, ambavyo viliwafanya mashabiki wakumbuke mbali, ikiwa ni pamoja na kuwakumbuka watunzi na waimbaji halisi wa nyimbo hizo, ambao kwa sasa hawapo katika bendi hiyo.

Safu ya magita iliongozwa vyema na Ramadhani Mapesa, Mjusi Shemboza na Karama Tony wakati kwenye drums walikuwepo Habibu Abbas, Juma Choka huku tumba ikikongotwa vilivyo na Ally Jamwaka.

Katika saxaphone na trumphet walikuwepo Hamisi Milambo, Mbaraka Othman na Shabani Lendi, ambao walizipuliza ala hizo kwa umahiri wa aina yake.

Onyesho hilo lilihudhuriwa na mashabiki wa rika tofauti, ambapo wengi ilikuwa mara yao ya kwanza kufika kwenye ukumbi huo,lakini walivutiwa na matangazo yaliyokuwa yakitolewa kuhusu onyesho hilo.

Baadhi ya wanamuziki wakongwe waliohudhuria onyesho hilo na kuelezea furaha yao kutokana na uamuzi wa Sikinde kuandaa onyesho hilo ni pamoja na Abuu Omar na Juma Kakere.

Abuu, ambaye anamiliki bendi ya Tanzanites, yenye maskani yake Falme za Kiarabu, alisema alifarijika kwa muziki wa Sikinde, hasa ilipopiga vibao vyake vya zamani.

"Kwa kweli tumepata burudani ya kutosha na pia nimepata nafasi ya kukutana na watu wengi, ambao nilipoteana nao,"alisema mkongwe huyo.

Akizungumzia onyesho hilo, mmoja wa mashabiki aliyejitambulisha kwa jina la Kaniki Hassan, alisema lilikuwa uzuri, lakini lilichelewa kuanza kwa muda ulioangwa.

"Siku nyingine Sikinde wakipanga kuanza onyesho saa 12 jioni, basi iwe muda huo, sio wafanya kama leo wameanza saa moja,"alisema.

Mratibu wa onyesho hilo, Rashid Zahor, alisema kutokana na maombi mengi waliyoyapata kutoka kwa mashabiki, wameanga kuandaa lingine mwishoni mwa Desemba, mwaka huu.

Mwakilishi wa Kampuni ya Isere Sports, iliyodhamini onyesho hilo, Damas Omwigamba, alisema wamefurahia mwitikio wa mashabiki katika onyesho hilo na kwamba wataendelea kuidhamini bendi hiyo kwa sare za muziki.

Kiongozi wa bendi hiyo, Abdalla Hemba, alisema hawakutarajia kupata mashabiki wengi kama ilivyokuwa na kuongeza kuwa, huo ni uthibitisho wa wazi kwamba muziki wa dansi bado unapendwa.

Friday, November 25, 2016

ISERE SORTS KUNOGESHA USIKU WA SIKINDE


MKURUGENZI wa duka la kuuza vifaa vya michezo la Isere Sports, Abbas Isere (kulia), akimkabidhi moja ya fulana 30, Mratibu wa onyesho la Usiku wa Sikinde, Rashid Zahor, kwa ajili onyesho hilo, litakalofanyika kesho katika ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam. (Picha na Jumanne Gude).

KAMPUNI ya Isere Sports, inayojihusisha na utengenezaji na usambazaji wa vifaa vya michezo, imejitokeza kulinogesha onyesho la 'Usiku wa Sikinde' kwa kutoa zawadi maalumu ya fulana.

Onyesho hilo, ambalo limelenga kuwakumbusha mashabiki nyimbo za zamani na mpya za bendi ya Mlimani Park Orchestra, linatarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu, kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo,  Abbas Isere, alikabidhi fulana hizo jana, kwa Mratibu wa onyesho hilo, Rashid Zahor, katika hafla iliyofanyika ofisini kwake mjini Dar es Salaam.

Abbas alisema ameamua kutoa zawadi hiyo ya fulana ili kuiunga mkono bendi hiyo katika jitihada zake za kukuza na kuinua muziki wa dansi nchini.

"Mimi nimeishi sana mitaa ya Kariakoo na ni miongoni mwa mashabiki wakubwa wa Sikinde, nilikuwa sikosekani kwenye kumbi, ambazo bendi hii ilikuwa ikitumbuiza, hivyo nimetoa fulana hizi kwa lengo la kuiunga mkono pamoja na nyinyi waratibu,"alisema.

Mbali na kutoa zawadi hiyo ya fulana, Abbas alisema atakuwa miongoni mwa mashabiki watakaohudhuria onyesho hilo, ambalo amebashiri kuwa litakuwa la aina yake kwa sababu litakuwa kwa ajili ya watu maalumu.

Akipokea fulana hizo, Zahor alimshukuru Abbas kwa msaada huo, ambao alisema utalifanya onyesho hilo liwe na mvuto wa aina yake kwa sababu baadhi zitatolewa kwa mashabiki.

Alisema wakati wa onyesho hilo, mashabiki watakaopendeza kwa mavazi, kucheza vizuri na kujibu vyema maswali yanayohusu Sikinde, watapatiwa zawadi hizo za fulana.

Baadhi ya nyimbo adimu zitakazopigwa kwenye onyesho hilo ni pamoja na Celina, Maudhi, Taraka rejea, Clara, Christina Bundala, Hiba, Barua kutoka kwa mama, Chenga ya mwili, Dua la kuku, Sitokubali kuwa mtumwa, Mtoto akililia wembe, Cenjesta na Epuka jambo lisilokuhusu.

Kiongozi wa bendi hiyo, Abdalla Hemba, aliwahakikishia mashabiki kwamba, watapata burudani murua na adimu, ambayo hawataisahau katika maisha yao.

TFF YAOMBOLEZA KIFO CHA AHMAD KILUVIA WA YANGA




“Nimeshtushwa,” ni neno moja tu la Rais wa  Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania  (TFF), Jamal Malinzi mara baada ya kupata taarifa za kifo cha Hamad Kiluvia ambaye ni mmoja wa viongozi wa Young Africans Sports Club.

Hamad Kilivua amefariki dunia leo alfajiri Novemba 23, 2016 jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku ambayo Makamu Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Isaac Shekiondo ‘Clinton’ amezikwa kwao Korogwe mkoani Tanga.

Kilichomshitua Rais Malinzi ni kifo cha Kiluvia akisema kinakwenda sambamba na cha Shekiondo aliyefariki dunia Novemba 20, mwaka huu kwenye Hospitali ya Amana, Ilala  jijini Dar es Salaam.

Leo amepata taarifa za kifo cha Kiluvia ambaye alikuwa mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Young Africans. Enzi za uhai wake, Kiluvia akiwa Mjumbe wa bodi hiyo alishirikiana na Malinzi wakati huo wakiwa viongozi wa juu wa Klabu hiyo ambayo Makuu yake yako kwenye makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, Kariakoo, Dar es Salaam.

Rais Malinzi amesema amepokea kwa masikitiko kifo cha Kiluvia kwa kuwa anafahamu vema utendaji wakati huo akiwa Kiongozi wa Young Africans Sports Club. Alikuwa ni mtu mpole, mwenye kusikiliza na kutatua changamoto za klabu aliyependa mpira wa miguu na kutoa misaada na fedha na mawazo kadiri ya uwezo wake.

Kadhalika Rais Malinzi alituma salamu hizo kwa familia ya marehemu Kiluvia ndugu, jamaa na marafiki ambayo kwa muda walikuwa wakimuuguza mpendwa wao na hivyo kutokana na kifo hicho, amewataka kuwa watulivu kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao.

Msiba wa Kiluvia uko nyumbani kwake, Mikocheni Regent Estate jirani na Ofisi za Baraza la Mazingira (NEMC) ambako taratibu za mazishi zinafanyika.

RAUNDI YA PILI AZAM SPORTS FEDERATION CUP 2016/2017


Wakati Baruti ya Mara ikiifunga Ambassador ya Simiyu mabao 3-1 katika mchezo wa raundi ya pili  ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), ndani ya Uwanja wa  Halmashauri Kahama,  michezo mingine inatarajiwa kuendelea Novemba 27, mwaka huu kwenye viwanja mbalimbali kwa mujibu wa ratiba.

Hatua ya pili itakutanisha timu zlizopenya hatua ya kwanza iliyofanyika wikiendi iliyopita. Mechi zinazotarajiwa kucheza hatua inayofuata ni Tomato dhidi ya Jangwani katika mchezo utakaofanyika mkoani Njombe.

Mbuga FC ya Mtwara itacheza na Muheza United huko Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara huku Kabela City ya Kahama itakuwa mwenyeji wa Firestone ya Kiteto mkoani Manyara.

 Raundi ya tatu itafanyika Desemba 3, 2016 kwa kukutanisha timu za Mtwivila ambayo itasubiri mshindi kati ya Tomato na Jangwani wakati Stand Bagamoyo itasubiri mshindi kati ya Mbuga na Muheza United ya Tanga huku Stand Misuna inasubiri mshindi wa mchezo kati ya Kabela City na Firestone ya Manyara ilihali Mrusagamba ya Kagera sasa inasubiri kucheza na Baruti ya Mara.

Kufika hapo Tomato iliing’oa Mkali ya Ruvuma kwa ushindi wa penalti 6-5; Jangwani iliifumua Nyundo 2-0; Mtwivila iliilaza Sido kwa mabao 7-4; Mbuga iliifunga Makumbusho mabao 5-4; wakati Muheza ilishinda 2-1 dhidi ya Sifa Politan ya Temeke.

Timu ya Stendi FC ililala kwa Kabela City kwa mabao 5-3; wakati Stand Misuna iliifunga Veyula mabao 2-1 huku Stand ikiilaza Zimamoto mabao 5-4 ilihali Baruti FC ya Mara na Mrusagamba ya Kagera zilipita baada ya wapinzani Gold Sports ya Mwanza na Geita Town kugomea mechi za awali kwa kutojitokeza uwanjani.

MREMBO WA TANZANIA AKABIDHIWA BENDERA YA TAIFA, KWENDA MAREKANI KESHO KUWANIA TAJI LA DUNIA




Mlezi wa Kamati ya Miss Tanzania  ambaye pia Balozi wa Heshima wa Botswana nchini Tanzania, Bw. Emanuel Ole Naiko akimkabidhi bendera Diana Edward Lukumai Miss Tanzania 2016 anayeondoka nchini kesho kuelekea nchini Marekani kwa ajili ya Shindano la Miss Word linalotarajiwa kufanyika nchini humo, Katikati ni Hashim Lundenga Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Hafla hiyo imefanyika leo kwenye hoteli ya New Africa jijini Dar es salaam.
Diana Edward Lukumai Miss Tanzania 2016 akizungumza mbele ya waandishi wa habari leo kwenye hoteli ya New Africa Jijini Dar es salaam wakati alipokabidhiwa bendera ya Taifa kwa ajili ya safari yake ya Marekani atakakoshiriki shindano la dunia la Miss Word, Kulia ni Mkuu wa Itifaki Miss Tanzania Bw. Albert Makoye na katikati ni Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania Bw. Hashim Lundenga.

WAZIRI NAPE ATEMBELEA OFISI ZA DIAMOND




Na Mwandishi Wetu

Kundi la Muziki wa kizazi kipya(Bongo Flavour) Wasafi limemuomba Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye   kusaidia wasanii wa muziki huo kujivunia kazi yao kwa kupata maslahi ya kazi hiyo kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Akizungumza wakati Waziri huyo alipotembelea Studio za Wasafi na kujionea utendaji kazi wa studio hiyo, Mmiliki wa studio hizo Naseeb Abdul (Diamond Platinumz) amesema, kumekuwa na changamoto nyingi katika tasnia ya muziki hasa wizi wa kazi zao ambazo zimekuwa zikirudufiwa na kuuzwa kiholela ndani na nje ya nchi bila wao kufaidika na uuzwaji wa kazi hizo.

Changamoto nyingine alizozitaja  msanii Diamond ni pamoja na kupunjwa mapato yatokanayo na Miito ya Simu (Caller tunes) , kukosekana kwa ukumbi wa kisasa kwa ajj ili ya kufanyia maonesho makubwa ya muziki nchini, kuongezeka kwa uwiano wa nyimbo za kitanzania zinazopigwa redioni dhidi ya nyimbo za kigeni hasa kutoka Afrika ya Magharibi.

Aidha wamemuomba Waziri Nape Moses Nnauye kuwasaidia kupata Elimu juu ya ulipaji kodi ili tasnia ya Muziki nayo iweze kuwa kati ya tasnia zenye mchango mkubwa kwa pato la taifa kwa maendeleo ya wasanii na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye  amehaidi kuzifanyia kazi changamoto hizo na kuifanya tasnia ya muziki kuwa ajira kubwa kwa vijana wengi kwa kuongeza vipato vyao na pato la taifa kwa ujumla.

Wasafi Classic ni kundi la Muziki wa kizazi kipya(Bongo Flavour) Tanzania linalomilikiwa na Msanii Naseeb Abdul (Diamond Platinumz) na mpaka sasa lina wasanii wapatao 16 na linaongozwa na mameneja Babu Tale, Said Fella na Sallam SK.

Tuesday, November 22, 2016

MALINZI AKUMBUKA UKARIMU WA SHEKIONDO




Rais wa  Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania  (TFF), Jamal Malinzi, amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Young Africans Sports Club, Yussuf Manji kutokana na kifo cha Makamu Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Isaac Shekiondo ‘Clinton’.

Shekiondo aliyefariki dunia juzi Novemba 20, mwaka huu kwenye Hospitali ya Amana, Ilala  jijini Dar es Salaam, alikuwa Makamu Mwenyekiti katika Kamati ya Muda ya Young Africans chini ya Mwenyekiti Tarimba Abbas na enzi zake Shekiondo anakumbukwa kutokana na ukarimu wake na uwajibikaji mzuri katika klabu.

Katika salamu hizo, Rais Malinzi amesema amepokea kwa masikitiko kifo cha Shekiondo kwa kuwa anafahamu vema utendaji wa Shekiondo wakati huo akiwa Kiongozi wa Young Africans Sports Club. Ni mtu wa mpira wa miguu ambaye amekuwa kwenye tasnia hii kwa muda mrefu wa maisha yake.

Kadhalika Rais Malinzi alituma salamu hizo kwa familia ya marehemu Shekiondo, ndugu, jamaa na marafiki ambayo kwa muda walikuwa wakimuuguza mpendwa wao na hivyo kutokana na kifo hicho, amewataka kuwa watulivu kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao.

Msiba wa marehemu Shekiondo ulikuwa nyumbani kwake,  Ilala  Mchikichini, Dar es Salaam ambako leo Novemba 22, mwaka huu umeagwa katika Kanisa la KKKT Lutheran, Temeke Wailes kabla ya kusafirishwa kwenda Korogwe kwa Shemsi mkoani Tanga kwa mazishi.

Bwana ametoa, bwana ametwaa. Mungu ampumzishe kwa amani marehemu Shekiondo.

KAMATI YA LIGI YAWASHUSHIA RUNGU MAKOCHA PLUIJM WA YANGA NA HERNANDEZ WA AZAM, SIMBA YATOZWA FAINI 500,000




Uchunguzi dhidi ya waamuzi Martin Saanya, Samuel Mpenzu (mechi ya Yanga Vs Simba), Thomas Mkombozi (mechi ya Coastal Union Vs KMC) na Rajab Mrope (mechi ya Mbeya City na Yanga) umekaribia kukamilika.

Hatua ya mwisho ya uchunguzi huo ni wao kufika mbele ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya Saa 72) ambapo watahojiwa ili kutoa ufafanuzi katika masuala mbalimbali yaliyojitokeza katika taarifa zao.

MATUKIO YA LIGI KUU

Mchezo namba 90 (Simba Vs Toto Africans). Klabu ya Toto Africans imepewa onyo kali kutokana na timu yake kuchelewa kufika uwanja kwa dakika saba. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.

Mechi namba 99 (Mwadui Vs Simba). Klabu zote mbili zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa timu zao kuingia uwanjani kwa kutumia mlango wa washabiki, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(48).

Mechi namba 101 (Ruvu Shooting Vs Stand Utd). Ndanda FC imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kosa la timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi,  kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(48).

Nayo Ruvu Shooting ambayo ilikuwa uwanja wa nyumbani, imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 15. Kitendo hicho ni ukiukwaji wa Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu, na adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48).

Mechi namba 104 (JKT Ruvu Vs Ndanda). Klabu ya Stand United imepewa onyo kali baada ya wachezaji wake kufanya vurugu wakitaka kuingia uwanjani bila ya kuwa na uthibitisho kuwa wao ni wachezaji wa timu hiyo wakati wa mechi kati ya JKT Ruvu na Ndanda iliyofanyika Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 42(1).

Mechi namba 112 (Majimaji Vs JKT Ruvu). Daktari wa JKT Ruvu, Abdullah Yusuf amefungiwa miezi mitatu, na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi kwa kusababisha usumbufu kwa Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, na kuwatolea maneno machafu Mwamuzi na Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 41(2).

Mtaalamu wa viungo wa JKT Ruvu, George Minja amefungiwa miezi mitano na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kumvamia Mwamuzi akitaka kumpiga, na pia kutoa lugha ya matusi kwa waamuzi baada ya mechi hiyo. Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41(2).

Nao wachezaji wa JKT Ruvu, Said Kipao jezi namba moja, Samwel Kamuntu (22), Pela Mavuo (16) na paul Mhidzhe (23) wamefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 kila mmoja kwa kuwatukana waamuzi baada ya mchezo kumalizika. Adhabu imezingatia Kanuni ya 37(7).

Mechi namba 116 (Mbao FC Vs Azam FC). Kocha wa Azam FC, Zeben Hernandez amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi (ordered off) kwa kukataa kuheshimu mipaka ya eneo la ufundi (technical area) katika mechi hiyo. Adhabu imezingatia Kanuni ya 40(11).

Mechi namba 117 (Ndanda Vs Stand Utd). Katika mechi hiyo kadri muda ulivyokuwa ukienda ball boyz walichelewesha kurudisha mipira uwanjani, na mbaya zaidi mipira ilikuwa ikifichwa kiasi cha kubaki miwili kati ya sita iliyokuwepo. Msimamizi wa Kituo ameandikiwa barua ili ahakikishe suala hilo halijitokezi tena.

Mechi namba 59 (Yanga Vs Ruvu Shooting). Timu ya Ruvu Shooting imepewa onyo kali kwa kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 12, jambo ambalo ni kinyume cha Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu.

Kocha wa Yanga, Hans van Pluijm amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa mechi tatu baada ya wakati wa mapumziko kuwazonga waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa. Pia baada ya mechi kumalizika alikwenda kwenye chumba cha waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa. Adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 40(1).

Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya washabiki wake kuwazonga waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa walipokuwa wakiingia vyumbani wakati wa mapumziko. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1).

Mechi namba 60 (Tanzania Prisons Vs Simba). Klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na timu yake kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) na kufika wakati taratibu zote za msingi zikiwa zimemalizika. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu.

Klabu zote (Tanzania Prisons na Simba) zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa timu zao kuingia uwanjani kwa milango isiyo rasmi. Kitendo hicho ni kinyume cha Kanuni ya 14(14), na adhabu imezingatia Kanuni ya 14(48).

Pia Tanzania Prisons imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya gari la Jeshi la Magereza namba MT 0084 aina ya Toyota Land Cruiser Pick Up likiwa na watu 15 kuingia uwanjani kwa nguvu, na kusababisha kupigwa na kuumizwa kwa mlinzi wa getini. Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1).

Kamishna wa mechi hiyo Jimmy Lengwe kutoka Morogoro amepewa onyo kali kwa kutoripoti baadhi ya matukio ya wazi yaliyotokea kabla ya mechi hiyo kuanza.

MATUKIO YA LIGI DARAJA LA KWANZA
GROUP A

Mechi namba 17  (Polisi Dar Vs Ashanti Utd). Kiongozi wa Polisi Dar, Ulimwengu Hamimu amefungiwa miezi sita na kupigwa faini ya sh. 200,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 41(2). Kiongozi huyo alichukua mpira na kuupiga kwenye jukwaa la timu ya Ashanti Utd na kutaka kumpiga Mwamuzi akiwa na mchezaji wake Pascal Theodory mwenye jezi namba 15. Mchezaji huyo amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 100,000.

Mechi namba 19 (Pamba Vs African Sports). Klabu ya African Sports imepewa onyo kali kwa kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) kwa dakika nne, na kufika na viongozi watatu badala ya wanne.

Mchezaji Shaban Kimaro amefungiwa mechi sita na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kumpiga kichwa Mwamuzi Msaidizi Namba Mbili. Mwamuzi alimtoa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa hilo alilolifanya dakika 83. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 24(6) ya Ligi daraja la Kwanza.

Naye Salum Omari pia wa African Sports amefungiwa mechi tatu na faini sh. 300,000. Akiwa mchezaji wa akiba aliingia uwanjani kwa nia ya kutaka kumshambulia Mwamuzi, lakini Polisi walimuwahi na kumtoa.

Mechi namba 20 (Kiluvya Utd Vs Mshikamano). Mchezaji Ayoub Upatu wa Mshikamano amesimamishwa na suala lake limepelekwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF kwa hatua zaidi baada ya Kiluvya Utd kuwasilisha pingamizi dhidi yake kuwa ni mchezaji wao, kwani wana leseni yake. Katika leseni ya Kiluvya Utd ametumia jina la Ayoub Kassim Lipati.

Mechi namba 25 (Ashanti Utd Vs Lipuli). Kamati imetupa malalamiko ya timu ya Lipuli dhidi ya Ashanti Utd kuwa katika mechi yao ilimchezesha mchezaji Patrick James mwenye jezi namba 15 wakati akiwa na kadi tatu za njano. Kamati imebaini wakati James akicheza mechi hiyo alikuwa na kadi mbili za njano, na si tatu.

Mechi namba 27 (Kiluvya Utd Vs Friends Rangers). Kocha Msaidizi wa Friends Rangers, Fadhili Ndumba amefungiwa mechi mbili na faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi na Mwamuzi kwa kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi Msaidizi Namba Moja. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.

GROUP B

Mechi namba 23 (Kurugenzi Vs Kimondo). Viongozi wa Kimondo, Eric Ambakisye, Selestine Mashenzi, na Mussa Minga wamefungiwa miezi sita, na kupigwa faini ya sh. 500,000 kila mmoja kwa kuwafuata waamuzi hotelini baada ya mechi ambapo walimpiga Mwamuzi Mussa Gabriel na kumjeruhi wakishirikiana na baadhi ya wachezaji wao.

Wachezaji waliohusika katika tukio hilo ambapo wamefungiwa mechi sita na faini ya sh. 500,000 kila mmoja ni; January Daraja Mwamlima, Daniel Douglas Silvalwe, Abiud Kizengo na Monte Stefano Mwanamtwa. Adhabu zote ni kwa mujibu wa Kanuni ya 24(6) ya Ligi Daraja la Kwanza.

GROUP C

Mechi namba  23 (Alliance Vs Mvuvumwa). Kocha Msaidizi wa Mvuvumwa, Ezekiel Chobanga amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi dakika ya 59 kwa kumtolea lugha chafu Mwamuzi. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi namba 24 (Polisi Dodoma Vs Rhino Rangers). Mchezaji Sameer Mwishehe wa Rhino Rangers amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumrushia Mwamuzi chupa ya maji baada ya mchezo kumalizika. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 37(7) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi namba 25 (Polisi Dodoma Vs Mgambo Shooting). Kocha wa Mgambo, Athuman Kairo amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kumshambulia kwa maneno Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 40(11).

Mechi namba 28 (Alliance Vs Singida Utd). Baada ya Alliance kupata bao, watu wa huduma ya kwanza walipokuwa wakiitwa kuingia uwanjani, walikuwa wanakwenda kwa kupoteza muda. Msimamizi wa Kituo ameandikiwa barua ya kuwakumbusha watu wa huduma ya kwanza kutekeleza majukumu yao wawapo uwanjani, na kuhakikisha kuwa tukio la aina hiyo halitokei tena.

LIGI DARAJA LA PILI

GROUP A

Mechi namba 4 (Bulyanhulu Vs Green Warriors). Mechi hiyo haikuchezwa kutokana na wachezaji wa Bulyanhulu kutokuwa na leseni, na vilevile kutokuwepo mawasiliano kati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Kamishna wa mechi hiyo juu ya tatizo hilo. Hivyo, mechi hiyo itapangiwa tarehe nyingine na kuchezwa katika uwanja huru (neutral ground).

Mechi namba 7 (Mji Mkuu Vs Bulyanhulu). Mechi hiyo haikuchezwa baada ya wachezaji wa Bulyanhulu wakiongozwa na Katibu Mkuu wao Alphonce Innocent kugomea wakitaka wachezaji watano wa Mji Mkuu ambao hawakuwa na leseni, lakini walikuwa na utambulisho maalum kutoka TFF wasicheze.

Licha ya Kamishna kuwataka wacheze na baadaye wawasilishe malalamiko yao kwake, walikataa huku Katibu wao Innocent akimzonga Kamishna na kumtukana. Bulyanhulu imepoteza mechi hiyo kwa kusababisha ivurugike kwa kuzingatia Kanuni ya 29(4) ambapo pia imepigwa faini ya sh. 1,000,000. Mji Mkuu imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu.

 Pia Katibu Mkuu wa Bulyanhulu, Aplhonce Innocent amefungiwa miezi sita kutojihusisha na shughuli yoyote inayohusu mpira wa miguu. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 29(6) ya Ligi Daraja la Kwanza.

 GROUP B

Mechi namba 1 (African Wanderers Vs AFC). Klabu ya African Wanderers imepigwa faini ya sh. 200,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mechi licha ya kuwa ni wenyeji. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.

Mechi namba 5 (African Wanderers Vs Kitayosce). Wachezaji Ally Rashid na Israel Said wa African Wanderers wamefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa Mwamuzi kuwatoa kwa kadi nyekundu baada ya kwenda nje ya uwanja na kupigana na washabiki. Adhabu imezingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Daraja la Pili.

Mechi namba 12 (JKT Oljoro Vs African Wanderers). Mechi hiyo haikuchezwa baada ya kutokea mkanganyiko wa mawasiliano kati ya African Wanderers na ofisi ya Bodi ya Ligi, hivyo itapangiwa tarehe nyingine.

GROUP D

Mechi namba 2 (Namungo Vs Sabasaba). Baada ya Namungo kufunga bao, washabiki wa timu hiyo waliingia uwanjani kushangilia. Klabu hiyo pamoja na Msimamizi wa Kituo wamepewa onyo kali kuhakikisha tukio hilo halitokei tena. Pia sehemu kubwa ya uwanja huo hauna nyasi, hivyo klabu husika imetakiwa kuhakikisha nyasi zinapandwa kabla ya kuanza mzunguko wa pili.

Mechi namba 9 (Mbarali United Vs Mkamba Rangers). Kamati imefuta kadi nyekundu aliyoonyeshwa mchezaji David Francis mwenye jezi namba 5 wa Mkamba Rangers baada ya kubaini kuwa ilitolewa kimakosa.

MIN 34/MSC/2016 - MAOMBI YA MVUVUMWA KUCHEZA SHINYANGA

Kamati imeridhia maombi ya timu ya Mvuvumwa kuhamishia mechi zake za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga kutoka Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma. Hivyo, kuanzia Mzunguko wa Pili wa SDL, mechi za Mvuvumwa zitachezwa mjini Shinyanga.

MAKONDA AFANYA ZIARA AZAM, AIPONGEZA KWA UWEKEZAJI MAKINI



 MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda, leo mchana amefanya ziara kwenye Makao Makuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC akiwa na lengo kuu la kuipongeza kutokana na juhudi kubwa wanazofanya za kuwekeza katika soka la Tanzania.

Mbali na kuipongeza Azam FC inayomilikiwa na familia ya mmoja ya wafanyabiashara maarufu Afrika, Alhaji Said Salim Bakhresa, pia ametoa shukrani zake kutokana na jitihada zinazoonyeshwa na mfanyabiashara huyo mzawa katika maeneo mengine aliyofanya uwekezaji mkubwa kwenye tasnia ya habari (Azam Media) na viwanda.

Kwenye msafara huo, Makonda aliambatana baadhi ya viongozi wengine wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, alikofanya ziara tofauti kusikiliza kero za wananchi wa wilaya hiyo akiwa sambamba na Mkuu wa Wilaya hiyo, Felix Jackson Lyanivana.

Ugeni huo ulipokelewa na viongozi wa juu wa Azam FC, wakiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Makamu Mwenyekiti, Nassor Idrissa, Meneja wa timu, Phillip Alando, ambao katika kumalizia ziara hiyo waliweza kumtembeza kwenye maeneo mbalimbali yaliyofanyiwa uwekezaji ndani ya Azam Complex.

Akitoa neno lake kwenye ziara hiyo, Makonda alisema haina ubishi kuwa Azam FC ndiyo timu pekee iliyofanikiwa kuwekeza ipasavyo kwenye soka huku akidai kuwa timu hiyo imeshaanza kwa vitendo kutekeleza suala la kupunguza idadi ya vijana walioko mtaani wasiokuwa na dira wala matumaini.

“Leo hii mnatuunga mkono zaidi kwa sababu ni kiwanja kimoja na ni timu moja ambayo kila mtu aliyeko Dar es Salaam anaizungumzia, katika suala zima la kupunguza idadi ya vijana walioko mtaani wasiokuwa na dira wala matumaini nyinyi Azam mmeshaanza kutekeleza kwa vitendo na watu wote hatuwezi kuajiriwa serikalini, haiwezekani leo serikali ikaajiri watu wote.

“Inawezekana kabisa kila mtu na kipaji chake anaweza akafanya vizuri na mwisho wa siku akaendesha maisha yake, kwa hiyo tunawashukuru sana sana sana Azam FC,” alisema.

Makonda alichukua fursa hiyo pia kutoa wito kwa watu wengine wenye uwezo kujitokeza, na kuiga mfano wa watu wa Azam FC ili kuwa na timu nyingi zenye ushindani na kuondoa migogoro kwenye soka la Tanzania.

“Waige mfano wa Azam, watengeneze timu zao, watengeneze viwanja ili tuwe na watu wengi, tuwe na timu nyingi zenye ushindani na hata hii migogoro migogoro inayotokea Yanga na Simba, wenye hela zao wasihangaike, kama wamegoma kukodishwa waje tu watengeneze timu zao ili na wenyewe waendelee kunufaika kwa sababu mwisho wa siku tunajua tukiwa na timu nyingi kama ilivyo Azam FC, ikapatikana timu nyingine ya watu wenye uwezo kama nyie mnavyowajali vijana wenu ushindani utakuwa mkubwa sana.

“Na hivyo ndivyo tunaweza kuweka vijana wengi wakawa kwenye vipaji vyao tukajenga uchumi wetu kupitia ajira inayotokana na michezo na mwisho wa siku tukapeperusha vema bendera ya Taifa letu katika mataifa mbalimbali katika sekta nzima ya michezo, mimi naamini kwa kazi na mfano mnaoonyesha niwaombe watu wengine waendelee kuiga,” alisema.

Katika ziara hiyo, pamoja na mambo mengine Makonda amewaomba Watanzania waendelee kununua bidhaa zinazotengenezwa na wazawa akitolea mfano baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na makampuni ya Bakhresa.

“Mfano kama hivi viwanda vyenu vinatengeneza juisi, mnatengeneza maji, mnatengeneza ngano, walioajiriwa ni Watanzania wenzetu kwa hiyo kadiri mnavyouza bidhaa zenu manake kuna uhakika wa kupanua biashara, mkipanua biashara wadogo zetu, kaka zetu wanapata ajira lakini la pili mkiendelea kuuza mnalipa kodi, ile kodi tunapata barabara, madawa, tunapata shule, tunapata kila kitu tunachokitafuta,” alisema.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Azam FC, alimshukuru Makonda kwa ugeni wake huo ndani ya klabu hiyo, huku akichukua fursa hiyo pia kumwelezea historia fupi ya Azam tokea ianzishwe mwaka 2004 hadi ilipo mpaka sasa.

Mbali na historia, alimweleza timu mbalimbali zilizoko ndani ya Azam Complex, timu ya vijana (U-20) na ile ya wakubwa pamoja na mipango kabambe inayoendelea ya kuunda timu za vijana za chini ya umri wa miaka 15 na 17, mchakato unaoelekea ukingoni ukihusisha mikoa mbalimbali.

“Baada ya michuano ya Copa Coca Cola kutokuwa na mwelekeo, kama klabu tumeamua kuwafuata vijana kule walipo tumefanya majaribio katika mkoa wa Dar es Salaam, tumekwenda Zanzibar, Tanga, Morogoro na wiki iliyopita tulikuwa mkoani Mbeya tulikopata vijana saba, bado tutaendelea kufanya uwekezaji tutaenda mkoani Tabora, Mwanza, Kigoma na Mtwara,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Kwa hiyo sisi tunaamini ya kuwa hata Mheshimiwa hapa Mkuu wa Mkoa utakuwa ni miongoni mwa wadau wetu wakubwa wa kutusapoti na karibu sana Azam FC usichoke kuja wakati wowote…Yote tunayoyafanya ni kutokana na kampuni mama ya Azam na wadhamini wetu ambao ni Benki ya NMB lakini haitoshi kwa hiyo tunachukua fursa hii kuyaomba makampuni mengine ambayo yanaweza kuona nafasi ya wao kuwekeza waje, tuna timu za vijana, njooni mfanye kazi na sisi tuweze kusomba mbele.”

Monday, November 21, 2016

DEDE ASUBIRI BARAKA ZA MSONDO KUNOGESHA USIKU WA SIKINDE

MTUNZI na mwimbaji nyota wa zamani wa bendi ya Mlimani Park Orchestra, Shabani Dede, amesema yuko tayari kulinogesha onyesho la 'Usiku wa Sikinde', litakalofanyika Jumapili ijayo.

Akizungumza na Uhuru, mwishoni mwa wiki iliyopita, Dede alisema anachokihitaji ni kupata baraka kutoka kwa viongozi wake wa bendi ya Msondo Ngoma ili aweze kushiriki kwenye onyesho hilo.

"Sikinde ni bendi yangu, kama nahitajika kushiriki kwenye onyesho hilo, siwezi kuacha kufanya hivyo. Lakini itabidi nipate baraka za viongozi wangu,"alisema.

Mwimbaji huyo mkongwe, ambaye kwa sasa anaitumikia bendi ya Msondo Ngoma, amekuwa mwimbaji wa pili wa zamani wa Sikinde kuthibitisha kushiriki kwenye onyesho hilo. Mwingine ni kiongozi na mwimbaji wa bendi ya Talent, Hussein Jumbe.

Meneja wa Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti alisema hawana tatizo kumruhusu Dede kushiriki kwenye onyesho hilo, isipokuwa ni lazima awajulishe viongozi wenzake.

"Hatuna tatizo kwa hilo, lakini inabidi nikae na viongozi wenzangu kujadili suala hilo kabla ya kutoa ruhusa kwa Dede,"alisema Kibiriti.

Dede ni miongoni mwa watunzi mahiri wa zamani wa Sikinde, akiwa anashika nafasi ya pili kwa kutunga nyimbo nyingi, nyuma ya mkongwe Hassan Bitchuka.

Onyesho la Usiku wa Sikinde, ambalo limelenga kuwakumbusha mashabiki nyimbo za zamani za Mlimani Park Orchestra na mpya, linatarajiwa kufanyika kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.

Dede na Jumbe wanatarajiwa kushiriki kuimba nyimbo mbalimbali za zamani walizowahi kuzitunga na kuziimba walipokuwa Mlimani Park.

Mmoja wa waratibu wa onyesho hilo, Emmanuel Ndege, alisema jana kuwa, maandalizi yanakwenda vizuri, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwasaka wanamuziki wengine nyota wa zamani wa bendi hiyo, akiwemo mpiga gita la solo na rythim, Abdalla Gama.

Ndege alisema wameamua kuliita onyesho hilo kuwa la Usiku wa Sikinde, kwa sababu ni maalumu kwa watu maalumu, lengo likiwa ni kuwakumbusha mashabiki,enzi bendi hiyo ilipokuwa ikitamba kwa miondoko hiyo.

Aidha, Ndege alisema bendi hiyo pia itatumia fursa hiyo kutambulisha baadhi ya nyimbo zake mpya na zile zilizorekodiwa katika albamu ya hivi karibuni, inayojulikana kwa jina la Jinamizi la talaka.

Ndege alisema wakati wa onyesho hilo, kutatolewa zawadi mbalimbali kwa mashabiki watakaovutia kwa mavazi na kujimwayamwaya Kisikinde. Pia, alisema mashabiki watakaoingia ukumbini mapema, watapatiwa zawadi.

Mratibu huyo alisema onyesho hilo limedhaminiwa na Kampuni ya Isere Sports, inayojihusisha na uuzaji wa vifaa mbalimbali vya michezo, gazeti la Burudani na kituo cha Redio Uhuru.

Kiongozi wa bendi hiyo, Abdalla Hemba, aliwahakikishia mashabiki kwamba, watapata burudani murua na adimu, ambayo hawataisahau katika maisha yao.

Sunday, November 20, 2016

HUSSEIN JUMBE KUPAMBA ONYESHO LA USIKU WA SIKINDE

MWIMBAJI nyota wa muziki wa dansi nchini, Hussein Jumbe, amethibitisha kushiriki katika onyesho maalumu la 'Usiku wa Sikinde', lililopangwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.

Jumbe, ambaye kwa sasa anamiliki bendi ya Talent, alisema jana kuwa, atashiriki onyesho hilo kwa sababu bendi ya Mlimani Park Orchestra ni nyumbani kwake.

Onyesho hilo, ambalo limelenga kuwakumbusha mashabiki nyimbo za zamani za Mlimani Park na mpya, linatarajiwa kufanyika kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.

Jumbe alisema katika onyesho hilo, atashiriki kuimba nyimbo mbalimbali za zamani alizowahi kuzitunga na kuziimba alipokuwa bendi ya Mlimani Park.

Alizitaja baadhi ya nyimbo hizo kuwa ni Isaya mrithi wangu, Nachechemea, Hisia za Mwanadamu na Nuru ya Upendo.

Kwa upande wake, Mratibu wa onyesho hilo, Rashid Zahor, alisema maandalizi yote muhimu yanakwenda vizuri, ikiwa ni pamoja na bendi hiyo kuzifanyia mazoezi ya nguvu baadhi ya nyimbo za zamani.

"Hili ni onyesho maalumu kwa watu maalumu, ndio sababu tumelipa jina la 'Usiku wa Sikinde', kwa sababu tunataka kuwakumbusha mashabiki, zile enzi bendi ilipokuwa ikitamba kwa miondoko hiyo,"alisema Zahor.

Alizitaja baadhi ya nyimbo adimu zitakazopigwa kuwa ni pamoja na Celina, Maudhi, Taraka rejea, Clara, Christina Bundala, Hiba, Barua kutoka kwa mama, Chenga ya mwili, Dua la kuku, Sitokubali kuwa mtumwa, Mtoto akililia wembe, Cenjesta, Epuka jambo lisilokuhusu na nyinginezo.

Aidha, Zahor alisema bendi hiyo pia itatumia fursa hiyo kutambulisha baadhi ya nyimbo zake mpya na zile zilizorekodiwa katika albamu ya hivi karibuni, inayojulikana kwa jina la Jinamizi la talaka.

Nyimbo hizo ni Jinamizi la Talaka, Za mkwezi mbili, Nikipata nitalipa,Kibogoyo, Dole gumba, Ng'ombe haelemewi nundu, Tabasamu, Supu umeitia nazi na Wali nazi.

Kwa mujibu wa Zahor, wakati wa onyesho hilo, mashabiki wataruhusiwa kuomba nyimbo watakazotaka kupigiwa na pia kutatolewa zawadi mbalimbali kwa watakaovutia kwa mavazi na kujimwayamwaya vizuri. Pia, alisema mashabiki watakaoingia ukumbini mapema, watapatiwa zawadi ya bia moja bure.

Mratibu huyo alisema onyesho hilo limedhaminiwa na Kampuni ya Isere Sports, inayojihusisha na uuzaji wa vifaa mbalimbali vya michezo, gazeti la Burudani na kituo cha Redio Uhuru.

Kiongozi wa bendi hiyo, Abdalla Hemba, aliwahakikishia mashabiki kwamba, watapata burudani murua na adimu, ambayo hawataisahau katika maisha yao.

Alisema wameshaanza kuzifanyia mazoezi baadhi ya nyimbo za zamani ili kuwapa mashabiki ladha halisi na kwamba, hakutakuwa na tofauti
licha ya wanamuziki wengi wa zamani kutokuwepo kwenye bendi hiyo kwa sasa.

Hemba amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenye onyesho hilo ili kuiunga mkono bendi yao, ambayo imekuwa mstari wa mbele kukuza na kuendeleza muziki wa dansi wa miondoko ya asili.

Aidha, kiongozi huyo wa Sikinde alisema watalitumia onyesho hilo kumkaribisha tena jukwaani mwimbaji nyota nchini, Hassan Bicthuka, ambaye alipumzika kutokana na kuwa mgonjwa.

SERENGETI BOYS YACHUNGULIA FAINALI ZA AFRIKA



Kama ilivyoripotiwa hapo awali, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) baada ya kutoridhika na kujiridhisha kuwa mmoja wa wachezaji wa Jamhuri ya Congo-Brazzaville, alikiuka kanuni za mashindano ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17, mwaka huu  lilimkatia rufaa mchezaji Langa-Lesse Bercy katika Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).

Kutokana na rufaa hiyo dhidi ya mchezaji huyo wa Congo, Langa Lesse Bercy, CAF liliagiza apelekwe Makao Makuu ya Shirikisho hilo, lililoko Cairo, Misri  kwa ajili ya kurudia na kuthibitisha umri wake kwa kipimo cha MRI (Magnetic Imaging Resonance).
TFF iliagizwa na CAF igharimie zoezi zima ikiwa ni pamoja na kulipia gharama za usafiri wa mchezaji husika na daktari wake  pamoja na kulipia gharama za vipimo. TFF ilikubaliana na matakwa hayo ya CAF na kulipia.
Kipimo ilikuwa kifanyike leo Novemba 19, 2016 saa 5.00 asubuhi mjini Cairo, Misri. Ujumbe wa TFF wa watu wanne ukiambatana na madaktari wawili uliwasili mjini Cairo tangu Novemba 17, 2016 ili  kuwa shuhuda wa zoezi la kipimo hicho.

Jana usiku saa 5.00 TFF ilipokea ujumbe kutoka CAF kuwa mchezaji Langa Bercy ameshindwa kusafiri kwenda Cairo kwa kuwa yuko katika eneo lililoko "vitani",eneo hilo halikutajwa.
 
TFF inaendelea kufuatia kwa karibu jambo hili ili kuhakikisha haki inatendeka .

Kadhalika Aidha TFF inaomba wadau wa mpira wa miguu wawe na subira katika kipindi hiki.

Thursday, November 17, 2016

SIKINDE YAWAANDALIA MASHABIKI ONYESHO MAALUMU NOVEMBA 27, NI LA USIKU WA VITU ADIMU, LITAFANYIKA DDC KARIAKOO



BENDI ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra, imewaandalia mashabiki wake onyesho maalumu litakalojulikana kwa jina la 'Usiku wa Sikinde'.

Onyesho hilo, ambalo limelenga kuwakumbusha mashabiki nyimbo za zamani za bendi hiyo na mpya, linatarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu, kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.

Akizungumza mjini Dar es Salaam, jana, Mratibu wa onyesho hilo, Rashid Zahor, alisema maandalizi yote muhimu yanakwenda vizuri, ikiwa ni pamoja na bendi hiyo kuzifanyia mazoezi ya nguvu baadhi ya nyimbo za zamani.

"Hili ni onyesho maalumu kwa watu maalumu, ndio sababu tumelipa jina la 'Usiku wa Sikinde', kwa sababu tunataka kuwakumbusha mashabiki, zile enzi bendi ilipokuwa ikitamba kwa miondoko hiyo,"alisema Zahor.

Alizitaja baadhi ya nyimbo adimu zitakazopigwa kuwa ni pamoja na Celina, Maudhi, Taraka rejea, Clara, Christina Bundala, Hiba, Barua kutoka kwa mama, Chenga ya mwili, Dua la kuku, Sitokubali kuwa mtumwa, Mtoto akililia wembe, Cenjesta, Epuka jambo lisilokuhusu na nyinginezo.

Aidha, Zahor alisema bendi hiyo pia itatumia fursa hiyo kutambulisha baadhi ya nyimbo zake mpya na zile zilizorekodiwa katika albamu ya hivi karibuni, inayojulikana kwa jina la Jinamizi la talaka.

Nyimbo hizo ni Jinamizi la Talaka, Za mkwezi mbili, Nikipata nitalipa,
Kibogoyo, Dole gumba, Ng'ombe haelemewi, Nundu, Tabasamu, Supu umeitia nazi na Wali nazi.

Kwa mujibu wa Zahor, wakati wa onyesho hilo, mashabiki wataruhusiwa kuomba nyimbo watakazotaka kupigiwa na pia kutatolewa zawadi mbalimbali kwa watakaovutia kwa mavazi na kujimwayamwaya vizuri.

Mratibu huyo alisema onyesho hilo limedhaminiwa na Kampuni ya Isere Sports, inayojihusisha na uuzaji wa vifaa mbalimbali vya michezo, gazeti la Burudani na kituo cha Redio Uhuru.

Kwa upande wake, kiongozi wa bendi hiyo, Abdalla Hemba, aliwahakikishia mashabiki kwamba, watapata burudani murua na adimu, ambayo hawataisahau katika maisha yao.

Alisema wameshaanza kuzifanyia mazoezi baadhi ya nyimbo za zamani ili kuwapa mashabiki ladha halisi na kwamba, hakutakuwa na tofauti
licha ya wanamuziki wengi wa zamani kutokuwepo kwenye bendi hiyo kwa sasa.

Hemba amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenye onyesho hilo ili kuiunga mkono bendi yao, ambayo imekuwa mstari wa mbele kukuza na kuendeleza muziki wa dansi wa miondoko ya asili.

Aidha, kiongozi huyo wa Sikinde alisema watalitumia onyesho hilo kumkaribisha tena jukwaani mwimbaji nyota nchini, Hassan Bicthuka, ambaye alipumzika kutokana na kuwa mgonjwa.

Mlimani Park Orchestra ilianzishwa 1978 na lililokuwa Shirika la Usafiri na Huduma za Taksi (TTTS), kwa lengo la kutoa burudani kwa mashabiki. Shirika hili lilikuwa mali ya serikali.

TTTS iliacha kuiendesha bendi hiyo mwaka 1982, ikachukuliwa na Shirika la Uchumi na Maendeleo la Mkoa wa Dar es Salaam (DDC). Kuanzia wakati huo, bendi ilibadilishwa jina la kuitwa DDC Mlimani Park Orchestra.

Mwaka 2010, uongozi wa DDC uliamua kujitoa kuiendesha bendi hii na kukabidhi vyombo kwa wanamuziki ili waweze kujiendesha. Tangu wakati huo, bendi hii imekuwa ikiendeshwa na wanamuziki wenyewe na kuchagua viongozi kila baada ya miaka miwili.

Baadhi ya wanamuziki waliowahi kuiongoza bendi hii ni marehemu Michael Enock, Muhidin Gurumo, Bennovilla Anthony, marehemu Nasir Lubua, Shabani Dede, Hussein Jumbe, Habibu Abbas 'Jeff' na Hemba.



Tuesday, November 15, 2016

SHAABAN IDD AELEZA SIRI YA MAFANIKIO YAKE AZAM FC



STRAIKA kinda anayechipukia kwa kasi katika timu ya Azam FC, Shaaban Idd, ameeleza siri ya mafanikio yake ya hivi karibuni, akidai kuwa kitendo cha Kocha Mkuu, Zeben Hernandez, kumuondolea uoga na kumpa maelekezo bora ndio mambo makuu yanayombeba hivi sasa.

Kinda huyo aliyelelewa kwenye kituo cha Azam FC Academy, jana alifunga mabao mawili muhimu na kutengeneza moja kwenye ushindi mnono wa Azam FC wa mabao 4-1, wakiifunga Mwadui ya Shinyanga, mengine yakifungwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na Francisco Zekumbawira.

Mabao hayo yamemfanya Idd kutimiza mabao matatu msimu aliyoifungia Azam FC baada ya kupandishwa kwenye kikosi cha timu kubwa huku akitoa pasi mbili za mabao, moja akimpa nahodha Bocco kwenye ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Kagera Sugar na nyingine akiitoa jana kwa straika nyota kutoka Zimbabwe, Zekumbawira.

Idd ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa mbali na kocha wa timu hiyo kumuondolea uoga, pia maelekezo mazuri anayompa na kumpa uhuru uwanjani nayo yamechangia kubadilika kwa kiwango chake kwenye mechi za hivi karibuni tofauti na mechi za awali mwanzoni mwa msimu.

“Kitu cha kwanza napenda kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kuweza kunijalia kuweza kuisaidia timu yangu kuibuka na ushindi wa mabao 4-1, pia napenda kumshukuru kocha wangu kwa kunipatia maelekezo mazuri ya kunifundisha jinsi mpira unavyochezwa na mimi bila kipingamizi nimetendea haki maelekezo yake na kuweza kuisaidia timu yangu kuibuka na ushindi.

“Kwa kweli ninafuraha sana na hii pia ni siku muhimu kwa ajili ya kiongozi wetu mkubwa ambaye amefariki (Mzee Said Mohamed Abeid) hivi majuzi (Jumatatu iliyopita), hivyo ushindi huu una maana nyingi sana kwetu,” alisema.


Kocha ampa uhuru
Idd aliyeibuka mfungaji bora wa michuano ya Azam Youth Cup yaliyofanyika mwaka huu akifunga mabao matano, alisema kuwa katika vitu vilivyomsaidia kubadilika hivi sasa ni kutokana na kocha kumpa zaidi uhuru uwanjani.

“Kocha kanipa nafasi na kanipa uhuru wa kujiamini nisiwe na uoga wowote tofauti na nilivyokuwa nikicheza mwanzo kwani nilikuwa nacheza na uoga, hivyo kocha kaliangalia hilo na kulitambua na hatimaye akanipa nafasi na kuniambia nicheze nisiwe na uoga wowote, nisiogope kitu chochote na nicheze kwa kiwango change,” alisema.

Alisema kwa kuwa ligi ya msimu huu ni ngumu na huu ukiwa ni msimu wake wa kwanza kucheza, amesema atazidi kupambana na kujitahidi kuweza kuisaidia zaidi timu yake hiyo katika mzunguko wa pili wa ligi unaokuja na michuano mingine pamoja na yeye kujijengea uzoefu.

Mashabiki nao wamuamini
Straika huyo, 18, alichukua fursa hiyo kuwaomba mashabiki wa Azam FC waendelea kumuunga mkono, kumvumilia na kumuamini zaidi kwani bado ana mambo mengi anayotaka kuifanyia Azam FC.

“Mashabiki wasichoke kutuombea dua na kutusapoti katika hii kazi yetu tunawaahidi tutawapa burudani nzuri na timu yetu kuwa katika nafasi nzuri kwenye mzunguko wa pili,” alimalizia kinda huyo.

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola ambacho ni mahususi kabisa kwa ajili ya kuchangamsha mwili wako na kuburudisha koo lako pamoja na Benki bora nchini kwa usalama wa fedha zako ya NMB, imemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi ikiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikijikusanyia jumla ya pointi 25 ikizidiwa pointi 10 tu na vinara Simba waliojizolea 35.

WATANO WACHAGULIWA MAJARIBIO YA AZAM FC U-17 ZANZIBAR


KAMA ulimisi taarifa ya majaribio ya wazi ya mwisho ya Azam FC kwenye msako wa kusaka vijana wenye umri chini ya miaka 17 (U-17) yaliyofanyika Visiwani Zanzibar mwishoni mwa wiki iliyopita.

Taarifa rasmi ni kuwa tulifanikiwa kuwachagua vijana watano kutoka visiwani humo, ambao wameingia kwenye mchujo wa mwisho utakaofanyika mwezi ujao makao makuu wa Azam Complex, yatakayohusisha vijana wote waliochaguliwa kwenye mikoa mbalimbali.

Vijana hao watano wanaungana na wengine 37 waliochaguliwa kwenye maeneo tofauti nchini katika mikoa ya Morogoro (12), Dar es Salaam (13), Tanga (12) na kufikisha idadi ya vijana 42 waliochaguliwa mpaka sasa kati ya vipaji 2,143 waliofanyiwa usaili.

Uongozi wa Azam FC kwa kushirikiana na idara ya ufundi ya timu hiyo, una nia dhati ya kuboresha mfumo wa kituo chake cha kukuza vipaji 'Azam FC Academy' ili kihusishe vijana wa umri tofauti kwa ajili ya kuvuna vipaji vingi zaidi kwa manufaa ya baadaye ya timu hiyo na Taifa kwa ujumla.

Hadi sasa Azam FC imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwenye uleaji wa vipaji katika kituo hicho, ikivuna vijana kadhaa wanaotamba sehemu tofauti katika timu mbalimbali nchini, wengine wakiwa wanaing'arisha timu kubwa ya kituo hicho.

Baadhi ya waliopandishwa kwenye timu kubwa ni makipa Aishi Manula, Metacha Mnata, mabeki Ismail Gambo, Gadiel Michael, Abdallah Kheri (mkopo Ndanda), viungo Mudathir Yahya, Masoud Abdallah, Bryson Raphael (mkopo Ndanda).

Wengine ni Joseph Kimwaga (mkopo Mwadui), Farid Mussa (aliye mbioni kujiunga na CD Tenerife - Hispania), wshambuliaji Kelvin Friday (mkopo Mtibwa Sugar) na Shaaban Idd.

Wanaotamba na timu nyingine baadhi yao ni Simon Msuva (Yanga), Mohamed Hussein (Simba), Rashid Mandawa (Mtibwa Sugar), Joseph Mahundi (Mbeya City), Jamal Mnyate (Simba).

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuendelea na mpango wake wa Kitaifa wa kusaka wachezaji chini ya umri wa miaka 17 (U-17) Jumamosi ijayo Novemba 12 mwaka huu kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 9.00 alasiri ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Baada ya wikiendi iliyopita kufanya majaribio ya wazi visiwani Zanzibar, ambako walichaguliwa wachezaji watano, sasa tunarudisha mkazo wetu Tanzania Bara na kufanya majaribio ya mwisho katika jiji la Dar es Salaam.

Kwa majaribio mengine ya wazi katika maeneo mengine kuzunguka Tanzania yatatangazwa hivi karibuni.

AZAM KUKIONGEZEA NGUVU KIKOSI CHAKE



UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kwa kushirikiana na benchi la ufundi la timu hiyo hivi sasa upo kwenye mchakato wa kukiongezea nguvu kikosi hicho.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni nia ya dhati kabisa ya Azam FC kutaka kufanya vizuri zaidi kwenye mzunguko wa pili wa ligi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na michuano ya Kimataifa inayokuja kuanzia mwezi ujao na mwakani (Kombe la Kagame na lile la Shirikisho Afrika).

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii mwaka huu, tayari wamemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi wakiwa kwenye nafasi ya tatu kwenye msimamo wakijikusanyia jumla ya pointi 25, wakizidiwa pointi 10 na kinara Simba aliyejizolea 35.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz juzi Kocha Msaidizi wa Azam FC, Yeray Romero, alisema kuwa kuelekea mzunguko wa pili wa ligi wanatarajia kuangalia mapungufu ya kikosi hicho kabla ya kuingiza sura mpya kwenye usajili ya dirisha dogo kwa ajili ya kuinyanyua timu na kufika kwenye nafasi nzuri zaidi.

“Wakati wachezaji wapya wanaingia pia tunatarajia kuwaangalia wachezaji ambao tunadhani kwa sasa kikosini hawawezi kuisaidia timu, ambao ndio watawapisha wachezaji hao, lengo la yote haya ni kuweza kuipeleka mbele zaidi timu zaidi ya hapa ilipo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Romero aliwapongeza wachezaji kwa kazi waliyoweza kuifanya mpaka sasa huku wao kama benchi la ufundi wakiahidi kufanya kazi nzuri zaidi kwa asilimia 100 katika kuirekebisha zaidi timu na kuziba mapungufu yaliyopo.

Matarajio yamefikiwa?   

“Kiufupi matarajio hayakuwepo ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye mzunguko wa kwanza, hatukuwa tumepanga kufika nafasi hiyo lakini mazingira tuliyokuwa nayo yametufanya kumaliza hapo, licha ya yote hii ni nafasi nzuri kwetu na tunachoangalia kwenye raundi ijayo ni kufika nafasi pili na ya kwanza,” alisema.

Kauli kwa mashabiki Azam FC

Kocha huyo wa zamani wa timu za CF Reale Juventud Laguna na CD Tenerife zote za Hispania, aliwashukuru mashabiki wa Azam FC kwa sapoti kubwa wanayoendelea kutoa kwenye mechi zao licha ya kupitia wakati mgumu kwenye baadhi ya mechi.

“Kwa kweli nachukua fursa hii kuwapongeza mashabiki wa Azam FC, kwa yote yaliyotokea wao wamekuwa pamoja nasi, timu inapofanya vibaya wapo na inapofanya vizuri wapo na ambacho tunaweza kuwaahidi ni mashabiki wetu ni kwamba waendelee kuwa na imani na timu yao kwa sababu nafasi tuliyofikia hivi sasa si mbaya sana, lakini ingawaje si kama ndio tuliyokuwa tumepanga kufika.

“Hivyo tunategemea raundi ya pili itakapoanza kwa nguvu ambazo tutaziingiza kikosini basi wakiwa wanaendelea kutusapoti kama mwanzo naamini ya kuwa mashabiki watajikuta kwamba hawakukosea kuichagua Azam FC kwa sababu matokeo yatakuwa ni mazuri kwa timu kuweza kupata ushindi,” alimalizia mtaalamu huyo.

Azam FC kuendelea kujifua

Wakati huo huo, mara baada ya kikosi cha Azam FC kurejea jana jioni jijini Dar es Salaam kikitokea mkoani Shinyanga kilipocheza na Mwadui, taarifa ni kuwa wachezaji wa timu hiyo wataendelea na mazoezi kama kawaida jioni ya leo.

Kwa mujibu wa programu ya benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Zeben Hernandez, mara baada ya mazoezi ya leo, kikosi hicho kinatarajia kucheza mchezo wa kirafiki kesho Jumamosi kabla ya kupumzika Jumapili na Jumatatu kitacheza mchezo mwingine wa kujipima ubavu.

Tathimini ya mzunguko wa kwanza

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi ya Azam Cola kinachochangamsha mwili na kuburudisha koo na Benki bora nchini kwa usalama wa fedha zako ya NMB, imefanikiwa kucheza jumla ya mechi 15 kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi ikifanikiwa kushinda jumla ya mechi saba, sare nne na kupoteza nne ikiwa imekunja kibindoni pointi 25.

Takwimu pia zinaonyesha kuwa, Azam FC imeshinda robo tatu ya mechi zake ilizocheza ugenini, ikiibuka na ushindi mara tano kati ya mechi nane za ugenini, ikifungwa tatu, kati ya mechi saba ilizokuwa mwenyeji imefanikiwa kuibuka kidedea mara mbili, sare nne na kuteleza mechi moja.

Hivyo takwimu hizo zinaeleza kuwa Azam FC imefanikiwa kupata alama 15 kwenye viwanja vya ugenini kati ya 24 ilizotakiwa kuvuna, ambapo imepoteza jumla ya pointi tisa ugenini.

Mabingwa hao wamevuna jumla ya pointi 10 kati ya 21 katika uwanja wa nyumbani, ikiwa imeacha uwanjani jumla ya pointi 11, nane katika uwanja wake wa Azam Complex kutokana na sare nne ilizotoa ndani ya dimba hilo na tatu ikiziacha ndani ya Uwanja wa Uhuru kufuatia kupoteza bao 1-0 dhidi ya Simba ambayo inaongoza ligi ikiwa na pointi 35 pungufu ya pointi 10 na mabingwa hao.

Rekodi ya ufungaji wa mabao zinaonyesha kuwa mpaka sasa kikosi hicho kimefunga 21, ukiwa ni wastani wa bao 1.4 kwenye kila mchezo katika mechi 15 ilizocheza huku pia ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 14 (yaani wastani wa kufungwa bao 1.0 kwenye kila mchezo iliocheza).

Nahodha John Bocco ‘Adebayor’, ndiye ameonekana kinara wa kutupia mabao msimu huu ndani ya Azam FC mpaka sasa akitupia sita akizidiwa mabao matatu na Shiza Kichuya wa Simba aliyekuwa kileleni kwa mabao tisa, wengine wanaomzidi ni Rashid Mandawa (Mtibwa Sugar), Simon Msuva, Amissi Tambwe (Yanga), ambao wote wamefunga saba kila mmoja.

Bocco pia yupo kileleni kwenye utengenezaji wa mabao akiwa ametoa pasi za mwisho nne, akifuatiwa kwa ukaribu na Khamis Mcha aliyechangia matatu ambaye pia ametupia wavuni matatu, huku Shaaban Idd aliyeweka kambani matatu naye akipika mawili.

Mpaka raundi ya kwanza inamalizika mchezaji wa Azam FC aliyecheza mechi nyingi kuliko mwingine yoyote ni kipa namba moja, aliyecheza 14 sawa na dakika 1,260 kati ya 1,350, alizotakiwa kucheza hadi ligi inafikia katikati na hii ni baada ya kupumzishwa mechi moja wakati kikosi hicho kikikabiliana Mbao, mchezo ulioisha kwa Azam FC kuteleza kwa kufungwa mabao 2-1.