'
Thursday, December 1, 2016
USIKU WA SIKINDE HAIJAPATA KUTOKEA
BENDI ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra, juzi iliwapa mashabiki wake burudani murua na adhimu wakati ilipofanya onyesho maalumu la Usiku wa Sikinde.
Katika onyesho hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam, kuanzia saa moja hadi saa sita usiku, mashabiki lukuki waliofurika kwenye ukumbi huo walirejea nyumbani wakiwa roho kwatu kutokana na kupata burudani ya vitu adimu.
Ikiongozwa na mwimbaji mkongwe, Abdalla Hemba, akisaidiwa na Karama Regesu, Hassan Kunyata na Musemba wa Minyigu, bendi hiyo kongwe ilianza onyesho hilo kwa kuporomosha vibao vyake vilivyowahi kutamba mwishoni mwa miaka ya 1970.
Kutokuwepo kwa mtunzi na mwimbaji mkongwe, Hassan Bitchuka, ambaye alikuwa mgonjwa, kulizua maswali mengi, lakini pengo lake lilizibwa vyema na Karama na Musemba.
Vibao vilivyotia fora na kuwakuna mashabiki ni pamoja na Taksi driver, Maudhi maudhi na Neema, ambavyo viliwafanya mashabiki wakumbuke mbali, ikiwa ni pamoja na kuwakumbuka watunzi na waimbaji halisi wa nyimbo hizo, ambao kwa sasa hawapo katika bendi hiyo.
Safu ya magita iliongozwa vyema na Ramadhani Mapesa, Mjusi Shemboza na Karama Tony wakati kwenye drums walikuwepo Habibu Abbas, Juma Choka huku tumba ikikongotwa vilivyo na Ally Jamwaka.
Katika saxaphone na trumphet walikuwepo Hamisi Milambo, Mbaraka Othman na Shabani Lendi, ambao walizipuliza ala hizo kwa umahiri wa aina yake.
Onyesho hilo lilihudhuriwa na mashabiki wa rika tofauti, ambapo wengi ilikuwa mara yao ya kwanza kufika kwenye ukumbi huo,lakini walivutiwa na matangazo yaliyokuwa yakitolewa kuhusu onyesho hilo.
Baadhi ya wanamuziki wakongwe waliohudhuria onyesho hilo na kuelezea furaha yao kutokana na uamuzi wa Sikinde kuandaa onyesho hilo ni pamoja na Abuu Omar na Juma Kakere.
Abuu, ambaye anamiliki bendi ya Tanzanites, yenye maskani yake Falme za Kiarabu, alisema alifarijika kwa muziki wa Sikinde, hasa ilipopiga vibao vyake vya zamani.
"Kwa kweli tumepata burudani ya kutosha na pia nimepata nafasi ya kukutana na watu wengi, ambao nilipoteana nao,"alisema mkongwe huyo.
Akizungumzia onyesho hilo, mmoja wa mashabiki aliyejitambulisha kwa jina la Kaniki Hassan, alisema lilikuwa uzuri, lakini lilichelewa kuanza kwa muda ulioangwa.
"Siku nyingine Sikinde wakipanga kuanza onyesho saa 12 jioni, basi iwe muda huo, sio wafanya kama leo wameanza saa moja,"alisema.
Mratibu wa onyesho hilo, Rashid Zahor, alisema kutokana na maombi mengi waliyoyapata kutoka kwa mashabiki, wameanga kuandaa lingine mwishoni mwa Desemba, mwaka huu.
Mwakilishi wa Kampuni ya Isere Sports, iliyodhamini onyesho hilo, Damas Omwigamba, alisema wamefurahia mwitikio wa mashabiki katika onyesho hilo na kwamba wataendelea kuidhamini bendi hiyo kwa sare za muziki.
Kiongozi wa bendi hiyo, Abdalla Hemba, alisema hawakutarajia kupata mashabiki wengi kama ilivyokuwa na kuongeza kuwa, huo ni uthibitisho wa wazi kwamba muziki wa dansi bado unapendwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment