KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, December 20, 2016

WACHEZAJI YANGA WAMGOMEA LWANDAMINA MAZOEZINI





WACHEZAJI wa Yanga, jana walifanya mgomo wa mazoezi  asubuhi wakiushinikiza uongozi wa timu yao kuwalipa mishahara yao ya mwezi Novemba.

Yanga walitakiwa kufanya mazoezi saa tatu asubuhi. katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya African Lyon, utakaopigwa kwenye uwanja huo.
 
Akizungumza Dar es Salaam jana, mmoja wa vigogo wa Yanga, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema wachezaji wote walifika uwanjani hapo saa tatu na nusu asubuhi.

Alisema baada ya kuwasili kwenye uwanja huo, waligoma kubadili nguo na kuvaa za mazoezi huku wakisisitiza kuwa hawatafanya mazoezi hadi hapo uongozi utakapowalipa mishahara yao.

Alisema licha ya Kocha George Lwandamina kutoka Zambia, kuwasihi wafanye mazoezi angalau kwa muda wa nusu saa, wachezaji hao walimuwekea ngumu na kumwambia msimamo wao upo pale pale hadi hapo watakapolipwa mishahara yao.

“Jumatatu iliyopita waligoma kuingia kambini kwa sababu hii hii, lakini tuliwasihi wasitishe mgomo ili wajiandae na mchezo wetu dhidi ya JKT Ruvu  walikubali.

“Tulicheza dhidi ya JKT Ruvu kwa morali ingawa tulikuwa na wasiwasi kuwa huenda  wakaharibu kwenye mchezo ule, lakini tulishukuru waliingia uwanjani na kucheza kwa moyo mmoja na ndio maana tulifanikiwa kupata ushindi wa mabao 3-0,”alisema kiongozi huyo.

Alisema wachezaji walitegemea baada ya mchezo huo wangerekebishiwa madai yao, hali ambayo haijatekelezwa hadi sasa.

Alisema anadhani wachezaji hao wameona ufumbuzi wa suala hilo ni kutofanya mazoezi na kuendelea na mgomo wao.

Kutokana na mgomo huo, benchi la ufundi la Yanga lilifanya jitihada za kuwasiliana na uongozi ili kuona wanatatua vipi tatizo hilo ili wachezaji hao warejee kwenye morali ya kufanya mazoezi.

“Hadi sasa bado hatujajua suala hili litaisha muda gani, kama ni leo (jana) au kesho (leo), tunawasiliana na viongozi tujue tunafanyaje,”alisema.

Wachezaji wote wa Yanga walitimka uwanjani hapo ilipofika saa 4:30 na kurejea majumbani mwao kusubiri mustakabali wa madai yao.

Yanga ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikijikusanyia pointi 36 huku Simba ikiwa kileleni mwa ligi kwa kuwa na pointi 38.

Baada ya mchezo wao na African Lyon, Yanga itasafiri kwenda visiwani Zanzibar, kucheza michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambapo Yanga itaanza kurusha karata yake ya kwanza dhidi ya Jamhuri, mchezo utakaopigwa Januari 2 saa mbili usiku.

No comments:

Post a Comment