KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, August 21, 2016

SIMBA YAANZA LIGI KUU KWA KISHINDO, YAINYUKA NDANDA FC MABAO 3-1, AZAM YAAMBULIA SULUHU KWA AFRICAN LYON

SIMBA jana ilianza vyema michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ndanda FC ya Mtwara mabao 3-1, katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mshambuliaji Laudit Mavugo kutoka Burundi alidhihirisha kuwa thamani yake ni dhahabu baada ya kuifungia Simba bao la kuongoza dakika ya 20, akimalizia pasi maridhawa kutoka kwa beki Mohamed Hussein 'Tshabalala.'

Ndanda FC ilifanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 37 kupitia kwa mshambuliaji wake machachari, Omary Mponda, baada ya kupokea krosi kutoka kwa nahodha wake, Kiggi Makassy. Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko.

Simba ilikianza kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji, ambapo Kocha Joseph Omog aliwapumzisha Jamal Mnyate na Ibrahim Hajib, ambao nafasi zao zilichukuliwa na Mwinyi Kazimoto n Frederick Blagnon.

Mabadiliko hayo yaliongeza uhai kwa Simba, ambayo ilifanikiwa kuongeza mabao mengine mawili kupitia kwa Blagnon na Shiza Kichuya.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Azam ilishindwa kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na African Lyon.

Lyon ilikuwa ya kwanza kufunga bao dakika ya 46 kupitia kwa Hood Mayanja kabla ya John Bocco kuisawazishia Azam dakika za majeruhi.

No comments:

Post a Comment