'
Tuesday, August 16, 2016
AKILIMALI AMUOMBA RADHI MANJI NA WANA-YANGA
HATIMAYE mwanachama mkongwe wa klabu ya Yanga na Katibu wa Baraza la Wazee la klabu hiyo, Ibrahim Akilimali, amemuomba radhi mwenyekiti wake, Yussuf Manji.
Akilimali alifikia uamuzi huo leo asubuhi baada ya wanachama wengi wa Yanga kujitokeza hadharani kushutumu kitendo chake cha kupinga Manji kuikodisha timu kwa miaka 10.
Akihojiwa na kituo cha redio cha EFM leo asubuhi, Akilimali alisema amempigia simu Manji kumuomba radhi kuhusu kauli hiyo na kwamba kwa sasa wapo kitu kimoja.
Akilimali alisema kama kuna watu wanaompenda Manji katika Yanga, basi yeye ni namba moja na kusisitiza kuwa hana tatizo naye.
Hivi karibuni, Akilimali alikaririwa na kituo kimoja cha redio akipinga kitendo cha Manji kuomba akodishwe kuisimamia Yanga kwa miaka 10, huku akitaka apewe umiliki wa logo ya klabu hiyo.
Aidha, Akilimali aliuponda mkutano mkuu wa dharula wa Yanga ulioitishwa na Manji kwa madai kuwa, wanachama walikurupuka kupitisha uamuzi huo.
"Nimempigia simu Manji na kumuomba radhi na narudia tena kumuomba radhi hapa ili Watanzania wote wanisikie,"alisema.
Vyombo vingi vya habari nchini leo viliripoti habari ya kujiuzulu kwa Manji, kufuatia shutuma zilizotolewa na Akilimali dhidi yake.
“Hatuna tatizo na Manji, tunampenda na ataendelea kuwa mwenyekiti hadi atakapotaka kuacha mwenyewe. Yanga ni moja, hatutaki tena kurejea kwenye mitafaruku ya kuanza kuitwa Yanga raizoni na Yanga kandambili,” alisema Akilimali.
Kwa mujibu wa mzee huyo, alichokosea Manji ni kutowaita wajumbe wa Baraza la Wazee wa Yanga ili kuzungumzia suala hilo kwanza kabla ya kulifikisha mbele ya wanachama.
Hata hivyo, alikiri kuwa Baraza la Wadhamini ndilo lenye nguvu kikatiba kuhusu masuala ya Yanga na sio Baraza la Wazee, ambalo halimo kwenye katiba.
Wakati huo huo, kikao cha matawi ya klabu ya Yanga yaliyoko mkoani Dar es Salaam, kimetoa pendekezo la kutaka Mzee Akilimali avuliwe uanachama kutokana na kauli zake zinazohatarisha umoja na mshikamano klabuni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment