'
Monday, October 6, 2014
TFF YAFAFANUA MAAMUZI YA KAMATI YA UTENDAJI
TAARIFA KWA VYOMBO UFAFANUZI KUHUSU MAAMUZI YA KAMATI YA UTENDAJI
Vyombo kadhaa vya habari vimeripoti kuhusu hali ya mgongano kati ya Kamati ya Utendaji ya TFF na Bodi ya ligi Tanzania (Tanzania Premier league Board).
Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania linapenda kutoa ufafanuzi ufuatao:
1.Bodi ya ligi imeundwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF kifungu 40(11).Hivyo Bodi ya ligi ni zao la Mkutano Mkuu wa TFF.
2.Katiba ya TFF imeipa mamlaka kamati ya utendaji ya TFF kutunga kanuni za uendeshaji wa Bodi ya ligi,kanuni hizi ndiyo nguzo kuu ya uendeshaji wa shughuli za Bodi ya ligi na ndizo zinaipa Bodi uhalali wake wa kuendesha shughuli zake za kila siku.
3.Bodi ya ligi ni chombo cha TFF kama vilivyo vyombo vingine vikiwemo kamati mbali mbali za TFF.Kisheria Bodi ya ligi sio chombo huru (its not a legal entity) hivyo Bodi pamoja na mambo mengine haina mamlaka ya kuingia mikataba ya aina yoyote ya kisheria .
4.Katiba ya TFF inatamka kuwa Bodi ya ligi itaheshimu na kufuata maagizo ya TFF.Maagizo haya yanatolewa na Sekretarieti ya TFF kwa niaba ya kamati ya utendaji ya TFF.
5.Mwenye mamlaka ya kutengua maamuzi ya kamati ya utendaji ya TFF ni Mkutano Mkuu wa TFF peke yake,hakuna chombo kingine cha chini chenye mamlaka hayo.
6.Kanuni za mashindano zinaandaliwa na kamati ya mashindano ya TFF na kupitishwa na kamati ya utendaji ya TFF. Kikao cha kamati ya utendaji kilichopitisha rasimu ya kanuni za ligi za mwaka 2014/15 kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa bodi ya ligi,Makamu mwenyekiti wa Bodi ya ligi na pia Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya TFF,hawa wote ni wajumbe wa Bodi ya ligi na walishiriki kikamilifu katika kikao cha kamati ya utendaji kilichopitisha kanuni za ligi 2014/15 ukiwemo na utaratibu wa mgawanyo wa mapato ya milangoni na ya udhamini.Katiba ya TFF inaagiza hivyo kuwa Viongozi wakuu wa Bodi ya ligi watakuwa pia ni wajumbe wa kamati ya utendaji ya TFF. Aidha mtendaji mkuu wa Bodi ya ligi alikuwepo kwenye kikao hiki cha kamati ya utendaji kama mwajiriwa.
7. Uamuzi wa kuunda mfuko maalum wa kuendeleza soka la vijana ni uamuzi uliopitishwa na kamati ya utendaji.Lengo la kuanzishwa mfuko huu ni kuwa na chombo maalum ambacho kitakuwa kinakusanya fedha toka vyanzo mbali mbali kwa ajili ya kuendeleza miradi ya soka la vijana nchini.Kwa sasa miradi hii ni:
(a) Kuanzisha vituo vya kulea na kuendeleza vipaji vya watoto kuanzia miaka 8-17 (sports centres) katika kila mkoa nchini mwetu.Mradi huu ni mkubwa utahitaji nyenzo hasa walimu na vifaa.
(b) Kuandaa timu ya taifa umri chini ya miaka 12 kwa ajili ya mashindano ya Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2019. Timu hii itaanza kuandaliwa mwaka huu Desemba baada ya mashindano ya kitaifa umri chini ya miaka 12. Hii timu itakusanywa na kuwekwa katika shule moja ya bweni ambapo watalelewa na kuendelezwa vipaji vyao wakiwa pamoja huku wanasoma.Tanzania tumeomba kuwa wenyeji wa fainali hizi.
(c) Kuandaa timu ya Taifa umri chini ya miaka 14 kwa ajili ya michuano ya awali mwaka 2016 kuelekea fainali za Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2017.
(d) Kuandaa timu ya Taifa umri chini ya miaka 17 kwa ajili ya michuano ya awali mwaka 2016 kuelekea fainali za Afrika umri chini ya miaka 20 mwaka 2017.
(e) Kuandaa mashindano ya Taifa ya mpira wa wanawake na ligi ya taifa ya mpira wa wanawake.
Miradi yote hii muhimu kwa maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania haina udhamini lakini ni lazima ifanyike ili tujihakikishie tunainua mpira nchini mwetu.Mafanikio ya miradi hii sio tu yatafaidisha na kuimarisha timu zetu za Taifa lakini pia yatakuwa chimbuko madhubuti la wachezaji mahiri wa vilabu vyetu vya mpira wa miguu.
Kimsingi tunatarajia kuwa vyanzo vikuu vya mapato ya kutunisha mfuko wa maendeleo ya mpira Tanzania vitakuwa:
- Mapato yatokanayo na mechi za ligi zetu madaraja yote
- Mapato yatokanayo na mechi za kimataifa
- Wadhamini
- Serikali kuu kupitia bajeti za Wizara zenye dhamana ya michezo,halmashauri na vyuo
- Wafadhili
- Shughuli mbali mbali za kutunisha mfuko.
Kamati ya utendaji ya TFF ilimteua Bwana Leodeger Tenga kuwa mwenyekiti wa kwanza wa mfuko huu na wajumbe wake ni Bw Tarimba Abbas, Bw Ephraim Mafuru, Mzee Ayoub Chamshama Bw Frederick Mwakalebela na Mh Zarina Madabida. Bw Henry Tandau na Bw Boniface Wambura ni waratibu wa mfuko huu. Imani ya TFF ni kuwa wajumbe hawa kwa kutumia uzoefu wao katika uongozi wa jamii watatusaidia kuhakikisha mfuko huu unaanza vyema shughuli zake.
Upande wa TFF tumefungua akaunti maalum benki kwa ajili ya kuingiza fedha zote zinazokusanywa kama mchango wa TFF kwenye mfuko huu zikiwemo asilimia 5 za makato ya fedha za udhamini na ZILE zitokanazo na mfuko wa jichangie,TFF inatoa wito kwa wadau wote wa mpira wa miguu Tanzania kuchangia mfuko huu ili utumike kunusuru mpira wetu. Fedha zitakazokusanywa matumizi yake yatasimamiwa na kanuni za uendeshwaji wa mfuko huu.
Hitimisho:
Kila mwanafamilia wa TFF anawajibika kuheshimu na kufuata maelekezo ya Kanuni za mashindano ya ligi kuu kama zilivyopitishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF .Hivyo utaratibu wa mgawanyo wa mapato yatokanayo na fedha za milangoni na za wadhamini kama ulivyoainishwa kwenye kanuni hizi uko pale pale. Ninaiagiza Bodi ya ligi kusimamia utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya utendaji ya TFF mara moja. Mwenye malalamiko kuhusu kanuni hizi ayalete kwenye vyombo husika vya TFF kwa kufuata Katiba,kanuni na taratibu za Shirikisho.Sote tunajenga nyumba moja hakuna haja ya kugombea fito.
Jamal Malinzi
Rais wa TFF
Dar es salaam
02/October/2014.
ZIMAMOTO YAIZIMA MALINDI LIGI KUU ZENJ
Pambano la ligi kuu ya Grand Malt ya Zanzibar jana kwenye uwanja wa Amaan mjini Unguja.
kati ya Zimamoto na Malindi. Zimamoto ilishinda bao 1 - 0.
UZINDUZI NANI MTANI JEMBE 2 WAFANA DAR
Viongozi wa timu za Simba na Yanga, Geofrey Nyange Kaburu, kushoto ambaye ni Makamu wa Rais Simba na Mohamed Bhinda, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Yanga (kulia) wakishindana kupiga danadana kuashiria uzinduzi rasmi wa kampeni ya Nani Mtani Jembe 2 inayoendeshwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager. Uzinduzi huo ni kwaajili ya wadau wa timu hizo ulifanyika jana viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam jana
Viongozi wa timu za Simba na Yanga, Geofrey Nyange Kaburu, kushoto ambaye ni Makamu wa Rais Simba na Mohamed Bhinda, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Yanga (kulia) wakivuta kamba kuashiria uzinduzi rasmi wa kampeni ya Nani Mtani Jembe 2 inayoendeshwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager. Uzinduzi huo rasmi kwa wadau wa Simba na Yanga ulifanyika jana viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.Katikati ni Meneja wa bia hiyo, George Kavishe na Mkurugenzi wa Masoko wa TBL, Bi Kushilla Thomas (aliyevaa suruali nyeupe).
Mashabiki wa Timu za Simba na Yanga wakicheza muziki wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Nani Mtani Jembe 2 kwa wadau wa timu hizo mbili katika hafla iliyofanyika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam jana.
Na Mwandishi Wetu
Shindano la ‘Nani Mtani Jembe2’ linalowakutanisha wakongwe wa Soka hapa nchini Simba na Yanga, limeanza kwa kasi msimu huu, baada ya jana kuwepo kwa shamrashamra za aina yake katika uzinduzi rasmi uliofanyika katika viwanja vya Leaders Jijini Dar es Salaam.
Mashabiki lukuki wa timu hizo na viongozi wao jana walijitokeza kwa wingi katika viwanja hivyo katika hafla iliyopambwa na makundi mbalimbali ya timu hizo yaliyokuwa yakitambiana mwanzo mwisho.
Msimu huu wa ‘Nani Mtani Jembe2’ unaoendeshwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager- wadhamini wakuu wa timu hizo, ulishuhudiwa Simba akianza vema katika mchezo wa soka baada ya Mjumbe wake wa Kamati ya Utendaji Said Tully kuwabuziga Yanga bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki wa mashabiki wa Simba na Yanga uliokuwa sehemu ya uzinduzi huo.
Katika mchezo huo wa soka ambao ulionekana kuwa na ushindani mkubwa, Simba waliwafunga Yanga iliyoongozwa na nahodha wao Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Mohamed Bhinda huku kwa upande wa danadana Bhinda akimshinda Makamu wa Rais wa Simba Geofrey Nyange ‘Kaburu’,huku kwa upande wa kuvuta kamba mashabiki wa tiu hizo wakitoka sare.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa timu hizo ‘Kaburu’ wa Simba pamoja na Mohammed Bhinda wa Yanga wote walianza kujigamba kuhakikisha wanaibuka na kitita cha mil 100 ambacho kimeandaliwa na Kilimanjaro Premium Lager.
Kaburu alisema, Yanga wameonekana wazi kuanza kushindwa, baada ya kuwatembezea kichapo cha bao 1-0 na pia kutoka sare ya kuvutana kamba hasa wakizingatia msimu uliopita wa Nani Mtani Jembe waliwazidi katika kila idara isipokuwa katika kura zilizopigwa na mashabiki ambapo Yanga walipigiwa zaidi kura na kuibuka na kitita cha shilingi milioni 98 kati ya milioni 100.
“Hapa imeonekana tumetoka sare katika kuvuta kamba, ila Yanga kama mnavyowajua wanapenda ubishi, wamevuta kamba wengi zaidi ya sisi lakini tumewaachia tu na msimu huu tutahakikisha tunachukua pesa zote na kuwaachia kifuta jasho tu,’alisema Kaburu.
Naye Bhinda aliwataka wanachama na mashabiki wa Yanga kuhakikisha wanaitendea haki Nani Mtani Jembe2 hii ili Yanga iwagalagaze Simba, kwa kuwa msimu uliopita waliwawaonea huruma Simba na kuwapa nafasi ya kuwafunga mabao 3-1 baada ya kuona wamezidiwa katika kuvutana.
“Sisi bwana hatuna shida na hawa watani zetu ndio maana tukawaleta wachezaji kutoka katika kitovu cha soka Brazil na bila ya kuwaleta sisi Simba wangetoa wapi nafasi ya kuwaona Wabrazil wakisakata kabumbu Tanzania,”alisema Bhinda.
Alisema kwa kila bia ya Kilimanjaro Premium Lager yenye ujazo wa milita 500 ambayo mteja atanunua ataona namba maalum na ataandika jina la timu yake (SIMBA au YANGA) ikifuatiwa na namba hiyo na atatuma kwenda namba 15415 na kwa kufanya hivyo atakuwa amepunguza kiasi cha shilingi 10,000 kwenye akaunti ya klabu pinzani na kuiongezea klabu yake kiasi hicho cha sh. 10,000.
“Msimu huu ni wa kipekee sana maana tumeona bora atakayefungwa siku ya mechi ya Nani Mtani Jembe walau apate kifuta jasho cha sh mil 5 huku mshindi akipata milioni 15. Klabu itanufaika, wachezaji watanufaika na mashabiki watanufaika. Sasa ni kazi kwenu viongozi kuwahamasisha mashabiki wa timu zenu,”alisema Kavishe.
SIMBA YABANWA NA STAND UNITED, YANGA YAIGAGADUA JKT RUVU
WAKATI timu kongwe ya soka nchini, Simba ikiendelea kusuasua katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Stand United, watani wao wa jadi Yanga wamezidi kupaa baada ya kuichapa JKT Ruvu mabao 2-1.
Simba ililazimishwa sare hiyo ya mabao na Stand United katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, matokeo yaliyopokewa kwa majonzi makubwa na mashabiki wa klabu hiyo.
Sare hiyo imeifanya Simba iwe imeambulia pointi tatu katika mechi tatu ilizocheza hadi sasa wakati Yanga imechupa nafasi za juu ikiwa na pointi sita katika mechi tatu.
Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa kiungo wake Shaaban Kisiga baada ya kupokea pasi kutoka kwa Emmanuel Okwi.
Bao hilo halikudumu kwa muda mrefu kwani dakika ya 45, Kheri Mohamed aliisawazishia Stand United baada ya kufanyika kwa shambulizi kali kwenye lango la Simba.
Nayo Yanga iliendelea kupaa nafasi za juu baada ya kuichapa JKT Ruvu mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Bao la kwanza la Yanga lilifungwa na beki Kevin Yondan kwa shuti kali la mbali, kufuatia kona iliyochongwa na kiungo Haruna Niyonzima.
Niyonzima aliiongezea Yanga bao la pili dakika ya 74 kwa mpira wa adhabu ndogo baada ya Genilson Jaja kuchezewa rafu nje kidogo ya eneo la hatari.
JKT Ruvu ilipata bao la kujifariji dakika ya 89 kupitia kwa mshambuliaji wake, Jabir Azizi.
Friday, October 3, 2014
SIMBA, YANGA MAJARIBUNI TENA WIKIENDI HII
VIGOGO vya soka nchini, Simba na Yanga mwishoni mwa wiki hii vitakuwa na kazi nyingine pevu wakati vitakaposhuka dimbani kusaka pointi tatu muhimu katika mechi za michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Wakati Simba itashuka dimbani kesho kumenyana na Stand United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, watani wao Yanga watashuka dimbani kwenye uwanja huo Jumapili kumenyana na JKT Ruvu.
Mechi zote mbili zina umuhimu mkubwa kwa Simba na Yanga kutokana na matokeo mabaya ziliyoyapata katika mechi mbili za mwanzo.
Simba ilianza ligi hiyo kwa kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Coastal Union kabla ya kulazimishwa sare nyingine dhidi ya Polisi Moro. Mechi zote mbili zilichezwa kwenye Uwanja wa Taifa.
Yanga ilianza ligi hiyo vibaya baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro kabla ya kuambulia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Katika mechi zingine za ligi hiyo zitakazochezwa kesho, Polisi Moro itaikaribisha Kagera Sugar mjini Morogoro, Ndanda FC watakuwa wageni wa Coastal Union mjini Tanga, Prisons itaikaribisha Azam mjini Mbeya wakati Ruvu Shooting itacheza na Mbeya City mjini Ruvu mkoani Pwani.
Mechi nyingine itachezwa Jumapili kati ya Mtibwa Sugar na Mgambo JKT, zitakazomenyana mjini Turiani, Morogoro.
Wednesday, October 1, 2014
TAMASHA KUBWA LA FILAMU KUFANYIKA TANGA
MENEJA Masoko wa kinywaji cha Grand Malt Tanzania, Fimbo Buttala akizungumza na
waandishi wa habari katika ukumbi wa Kebbys Hotel juu ya uzinduzi wa Tamasha la
Filamu jijini Tanga litakalofanyika kuanzaia Jumamosi hadi Oktoba 8, mwaka huu.
TAMASHA la wazi la filamu Tanzania “Grand Malt Film Festival 2014” sasa litafanyika kuanzia Oktoba 4hadi 8 mwaka huu kwenye viwanja vya Tangamano jijinia Tanga imeelezwa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Meneja Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Fimbo Butallah, alisema kuwa maandalizi ya tamasha hili yamekamilisha na uzinduzi rasmi utafanyika Jumamosi
Oktoba 4 na mgeni rasmi ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Halima Dendegu.
Butallah alisema kuwa tamasha hilo ni la wazi na hakuna kiingilio kwa wadau wa Sanaa hiyo ya filamu na uzinduzi utafanyika kuanzia saa tisa mchana.
Alisema kuwa kabla ya uzinduzi wa tamasha hilo, wasanii mbalimbali nyota ambao wanatarajia kushirikishi tamasha hilo watafanya kazi ya jamii kwa kutembelea kituo cha watoto wenye matatizo ya ngozi.
Aliongeza kuwa kupitia tamasha hili Grand Malt inasaidia kuinua na kutangaza kazi za wasanii wa hapa nchini na kuwapa nafasi ya kuwakutanisha na wadau na mashabiki wao.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Bongo Movie, Single Mtambalike, aliishukuru Grand Malt, kwa kufanikisha tamasha hili kwa mwaka wa tatu mfululizo.
Mtambalike alisema kuwa Sanaa ya filamu inasaidia kuwapatia ajira watu mbalimbali hapa nchini na kutaja katika maandalizi ya filamu moja, Zaidi ya wasanii 50 wanatumika kucheza filamu hiyo.
“Tunaashukuru sana Grand Malt na Sophia Records kwa kufanikisha tamasha hili ambalo linathibitisha wazi kuwa tasnia hii ni biashara kubwa”, alisema Mtambalike.
Rose Ndauka, ambaye naye ni msanii ya filamu aliwataka wadau wote kujitokeza na kutaja moja ya vitu watakavyotoa kwa watoto watakaowatembelea ni magodoro 60.
Awali tamasha hilo lilipangwa kufanyika mapema mwezi Agosti mwaka huu mkoani Mtwara.
26 WAITWA TAIFA STARS ITAKAYOIVAA BENIN
Wachezaji 26 wameitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars) kwa ajili mechi ya Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya Benin itakayochezwa Oktoba 12 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Kocha Mart Nooij ambaye yuko Cairo, Misri kwenye kongamano la makocha la Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), amesema kikosi cha Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kitaingia kambini Oktoba 6 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Wachezaji walioitwa ni makipa Deogratias Munishi (Yanga), Aishi Manula (Azam), na Mwadini Ali (Azam).
Mabeki ni Said Moradi (Azam), Shomari Kapombe (Azam), Oscar Joshua (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Aggrey Morris (Azam), Miraji Adam (Simba), Charles Edward (Yanga) na Emmanuel Simwanda (African Lyon).
Viungo ni Erasto Nyoni (Azam), Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar), Amri Kiemba (Simba), Himid Mao (Azam), Salum Abubakar (Azam), Said Ndemla (Simba) na Haruna Chanongo (Simba).
Washambuliaji ni Khamis Mcha (Azam), Simon Msuva (Yanga), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DR Congo), Mbwana Samata (TP Mazembe, DR Congo), Mrisho Ngasa (Yanga), Mwegane Yeya (Mbeya City), na Juma Liuzio (Zesco, Zambia).
METTY AJA NA KIBAO KIPYA 'NAJUA'
Wimbo mpya ya msanii Metty, uitwao 'Najua', unatarajiwa kuzinduliwa leo katika vyombo mbalimbali vya habari, ndani na nje ya nchi.
Katika wimbo huo, Metty amemshirikisha msanii Conrad, anayekuja kwa kasi katika tasnia ya muziki wa bongo flava.
Wimbo huo umetayarishwa katika studio mpya za kisasa za Centric Records, chini ya producer Davy Machords.
Metty amewaomba wadau na wapenzi wa muziki wa kizazi kipya kutoa ushirikiano wa nguvu katika kazi zake za muziki.
Thursday, September 25, 2014
SIMBA YAPATA PIGO, IVO MAPUNDA AVUNJIKA KIDOLE, KUIKOSA YANGA OKTOBA 12
Zikiwa zimebakia wiki mbili kabla ya kukutana na mahasimu wao wa jadi, Simba imepata pigo kubwa katika timu kwa sababu kipa namba moja wa timu hiyo Ivo Mapunda amevunjika kidole mazoezini Zanzibar jana asubuhi na anatakiwa kuwa nje ya uwanja kwa wiki nane.
Hatoweza kusimama golini wakati tiu yake ikicheza na Yanga October 12 2014 ambapo daktari wa Simba SC Yassin Gembe amesema Ivo aliumia wakati anachupia mpira katika mazoezi ya asubuhi na kwa bahati mbaya mpira ukamgonga kwenye kidole kidogo cha mwisho mkono wa kulia.
Gembe amesema Ivo alitoka mazoezini baada ya tukio hilo na baadaye akapelekwa hospitali ya Mnazi Mmoja kisiwani humo ambako baada ya vipimo ikagundulika amevunjika sana.
“Si kuvunjika kwa mzaha, amevunjika sana na anatakiwa kupumzika kwa wiki nane, baada ya hapo aanze taratibu… ina maana makadirio ya kurudi tena uwanjani ni hadi baada ya miezi mitatu‘ – Gembe.
Kuumia kwa Ivo kunatoa nafasi kwa makipa chipukizi Hussein Sharrif ‘Cassilas’ na Peter Manyika kujibidiisha ili kuziba pengo lake ambapo sasa Ivo anafanya idadi ya wachezaji majeruhi ambao ni tegemeo Simba kufikia wanne baada ya Paul Kiongera anayetakiwa kuwa nje wiki sita, Haroun Chanongo na Issa Rashid ‘Baba Ubaya’.
NYOTA WATANO WA KIGENI SIMBA WAPIGWA MARUFUKU KUCHEZA LIGI KUU, HAWANA VIBALI VYA KUFANYAKAZI, HATARINI KUIKOSA YANGA OKTOBA 12
Mshambuliaji wa Simba raia wa Uganda, Emmanuel Okwi na wenzake wanne wanaweza kuwa wameiingiza klabu hiyo kwenye mgogoro mkubwa; hawana kibali cha kufanya kazi nchinilicha ya kutumiwa kwenye mechi za ufunguzi wa Ligi Kuu mwishoni mwa wiki.
Idara ya Uhamiaji ilisema jana kuwa Okwi, Joseph Owino, Pierre Kwizera, Amis Tambwe na Raphael Kiongera hawana kibali cha kufanya kazi nchini, ambacho ni moja ya masharti makubwa ya kupata leseni ya kusakata soka.
Mbali na wachezaji hao, kocha Patrick Phiri pia haruhusiwi kukaa kwenye benchi la ufundi kwa kuwa naye hana kibali cha kufanya kazi nchini.
Akizungumza na gazeti hili jana, naibu kamishna wa Uhamiaji ambaye pia ni msemaji wa Idara hiyo, Abbas Mussa Irovya alisema nyota hao wa kigeni wa Simba hawaruhusiwi kuingia uwanjani wala kufanya mazoezi mahali popote hapa nchini na watakapoonekana wakifanya kazi kuanzia leo, watakamatwa.
“Tayari idara imemuagiza Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwakamata kuanzia kesho (leo) endapo wataonekana uwanjani aidha kwenye mechi au kwenye mazoezi na sheria itachukua mkondo wake,” alisema Irovya.
“Hatujapokea ombi lolote la klabu ya Simba kumuombea kibali mchezaji wala kocha wao wa kigeni ili afanye kazi hapa nchini na uwepo wao katika majukumu ya mazoezi au mechi ni kinyume cha sheria,” aliongeza msemaji huyo na kueleza kushangazwa na kitendo cha TFF kuwaachia waendelee kucheza wakati ikijua fika kuwa hawana kibali.
Okwi alikuwa na kibali cha kufanya kazi nchini alichoombewa na Yanga mwaka jana na baada ya kuidhinishwa Simba, klabu hiyo inatakiwa kumuombea kibali kipya.
“Tunamtambua Okwi kama muajiriwa wa klabu ya Yanga kwa kuwa ana kibali cha kufanya kazi hapa nchini chenye namba 1027397 kinachokwisha Machi 3, 2016 kilichoombwa na Yanga na siyo Simba alipo sasa,” alisema.
“Inachokifanya Simba ni kinyume cha sheria za nchi na za Idara ya Uhamiaji... kumwajiri mtu ambaye ana kibali cha kufanya kazi Yanga bila kutoa taarifa uhamiaji ni kukiuka taarifa za uhamiaji.”
Kwa mujibu wa kifungu cha 43 cha Kanuni za Ligi, mchezaji hawezi kupewa leseni ya kucheza soka nchini hadi atimize masharti mawili; kufanikiwa katika vipimo vya afya na kuwa na kibali cha kufanya kazi.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, kaimu katibu mkuu wa TFF, Boniface Wambura alijibu: “Wewe umeongea na Simba, wanasemaje?” na baadaye kumtaka mwandishi kuwasiliana na katibu mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa ambaye hakupatikana.
Kwa mujibu wa Irovya, Yanga ilishapeleka maombi ya vibali vya wachezaji wake kutoka Brazil, Genilson Santos ‘Jaja’ na Andrey Coutinho na makocha wao wawili kutoka nchi hiyo pia, Marcio Maximo na Leonardo Neiva na wako kwenye utaratibu wa kupata vibali hivyo
KATIBA MPYA KUWATAMBUA WASANII
Msanii wa filamu nchini Tanzania maarufu kama Mzee Chilo akiwa katika picha ya pamoja na mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Angellah Kairuki jana katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Kiongozi wa msafara wa wasanii waliofika katika Bunge Maalumu la Katiba,Simon Mwakifwamba akiwa katika picha ya pamoja na mjumbe wa bunge hilo, Angellah Kairuki katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Baadhi ya Wasanii wakijadiliana jambo mara baada ya kutoka nje ya Bunge Maalumu la Katiba jana mjini Dodoma.
Baadhi ya wasanii wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Fenella Mukangara (wa pili toka kushoto) wakati alipokutana nao maeneo ya viwanja vya bunge hilo.
Wasanii wakiendelea kumsikiliza Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Fenella Mukangara wakati alipokutana nao maeneo ya viwanja vya bunge hilo jana mjini Dodoma.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Fenella Mukangara akiwa katika picha ya pamoja na wasanii maeneo ya viwanja vya bunge hilo jana mjini Dodoma.
Na Happiness Mtweve, Dodoma
HATIMAYE Bunge Maalumu la Katiba, limeridhia mapendekezo ya kuboresha Rasimu kuhusu kuanzishwa kwa Ibara mpya inayohusu uhuru wa taaluma, ubunifu na ugunduzi.
Akiwasilisha Rasimu ya Katiba Mpya iliyopendekezwa na Bunge hilo mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge, alisema hayo ni moja ya mapendekezo kutoka makundi mbalimbali yaliyoridhiwa.
“Kamati ya Uandishi, imekubaliana na pendekezo hilo na imeanzisha Ibara mpya ya 48 A inayohusu uhuru wa taaluma, ubunifu na ugunduzi ili kutoa fursa ya mtu kujifunza, kufundisha, kutafiti na kueneza matumizi ya matokeo ya utafiti kulingana na kanuni za kitaaluma na za kiutafiti,” alisema Chenge.
Aidha, alisema serikali imepewa mamlaka ya kulinda hakimiliki za ugunduzi na ubunifu, ikiwa ni pamoja na haki za wabunifu na watafiti nchini kwa manufaa ya Taifa.
Mwenyekiti huyo pia alisema Kamati ya Uandishi imependekeza kuongezwa kwa aya mpya ya (f) inayoweka masharti kwa serikali kukuza na kuendeleza utafiti inayoeleza: “Mambo mengine yanayohusu ubunifu, ugunduzi na utafiti.”
Hatua hiyo ni mwanzo wa mafanikio kwa wasanii wa fani mbalimbali nchini, ambapo sasa wataweza kunufaika kutokana na kulindwa na kutambulika kwa kazi zao.
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Martha Mlata, akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge jana, alieleza kufurahishwa na Katiba Inayopendekezwa, kuwatambua wasanii kwa kuwa kilikuwa kilio chake cha muda mrefu ndani na nje ya Bunge.
Alisema kwa muda mrefu wasanii nchini wamekuwa wakipambana kufanya kazi kwa ajili ya kuinuka kiuchumi, lakini wamekuwa wakikwamishwa kutokana na kunyonywa, hivyo kutopata kile wanachostahili, jambo ambalo kwa sasa limeangaliwa kwa umakini.
"Nimefarijika mno kuwepo kwa mapendekezo ya kutambua wasanii na kazi zao za sanaa...ni muda mrefu sana nimekuwa nikililia hili kwa manufaa ya wasanii wote nchini. Nawaomba wasanii waungane kuhakikisha wanatetea na kuipigia kura katiba hii ili kuhakikisha inapita," alisema Martha, ambaye amekuwa mstari wa mbele kutetea haki za wasanii nchini.
SSB KUDHAMINI TUZO ZA TASWA KWA MIL 10/-
TUZO za Wanamichezo Bora wa Tanzania zinazotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) zinatarajiwa kufanyika Desemba 12 mwaka huu, huku Kampuni ya Said Salim Bakhresa (SSB) Group Limited ikijitokeza kuwa mdhamini mshiriki wa tuzo hizo kwa kutoa Sh. Milioni 10.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mgahawa wa City Sports Lounge, Dar es Salaam katika hafla ya kutangaza udhamini huo jana, Meneja Mkuu wa SSB Limited, Said Muhammad Said alisema wameamua kudhamini tuzo hizo kama hatua mojawapo ya kuinua michezo nchini.
Aliupongeza uongozi wa TASWA kwa juhudi kubwa inazofanya katika kuhamasisha michezo na kwamba wameona waunge mkono juhudi hizo kwa kutoa fedha hizo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto alisema kampuni mbalimbali zimeonesha nia ya kudhamini tuzo hizo na watakuwa wanazitangaza kadri watakavyomalizana nazo.
“Tunaishuku sana Bakhressa kwa mchango huu mkubwa kwetu, pia tunaomba wadau tushirikiane kwa kila hali kuhakikisha tuzo zetu zinafanikiwa na tunaomba kampuni zaidi zijitokeze.
“Bajeti ya tuzo zetu ni Sh milioni 120, zipo kampuni zimeonesha nia ya kutusaidia, mwishoni mwa wiki hii au mwanzoni mwa wiki ijayo tutatangaza wadhamini wengine,” alisema Pinto.
Naye Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando alisema Kamati Maalum ya Tuzo hizo inaendelea na mchakato wake wa kupata wanamichezo hao na kwamba kadri watakavyokuwa wanapiga hatua watatoa taarifa kwa wanahabari.
Alisema maandalizi mengine yanaenda vizuri na wanaamini zitakuwa tuzo bora kuliko zote zilizowahi kufanywa na chama hicho katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa miaka mitano iliyopita walioshinda Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa TASWA walikuwa ni Samson Ramadhani (2006), Martin Sulle (2007), Mary Naali (2008), ambao wote ni wanariadha, wakati 2009 na 2010 alikuwa mcheza netiboli Mwanaidi Hassan na mwaka 2011 alikuwa beki Shomari Kapombe ambaye sherehe za kumkabidhi tuzo zilifanyika Juni mwaka 2012. Mwaka jana tuzo hizo hazikufanyika.
Wakati huohuo, Mhando alisema chama chake kinaendelea na mazungumzo na wadhamini mbalimbali kuhusiana na tamasha kwa ajili ya vyombo vya habari ‘Media Day Bonanza’ na kwamba mapema mwezi ujao suala hilo litakuwa limemalizika.
Tuesday, September 23, 2014
MREMBO MWENYE KIPAJI ASAKWA MANYARA
Warembo 15 kati ya 30 wanaoshiriki shindano la Redds Miss Tanzania 2014
wakisindikizwa na mkali wa Bongo Fleva kutoka Jijini Dar es Salaam,
Tunda Man, wametoa burudani kali wakati wa shindano dogo la awali la
kumtafuta mrembo mwenye kipaji lililofanyika Babati Mkoani Manyara.
WASANII WASISITIZWA MATUMIZI SAHIHI YA MITANDAO
Afisa Habari wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Aristides Kwizela (Kulia) akisisitiza jambo kwa Wasanii (Hawako pichani) wakati wa Jukwaa la Sanaa lililofanyika mapema wiki kwenye Ukumbi wa Baraza hilo ulioko Ilala, Sharif Shamba jijini Dar es Salaam. Katikati ni mdau wa Sanaa, Henry Mdimu na Afisa Sanaa wa Baraza hilo, Augustino Makame.
WASANII nchini wamesisitizwa juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwani waandaaji wa matamasha na matukio mbalimbali ya kisanaa sehemu mbalimbali duniani wamekuwa wakiitumia katika kuwapa kazi.
Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa lililofanyika mapema wiki hii kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam, mdau wa Sanaa Henry Mdimu alisema kuwa ni jambo la kushangaza kuona wasanii wakitumia kurasa zao kuonesha mambo binafsi kama ya mapenzi na matusi wakati zinapaswa kutumika kwa ajili ya kazi zao za Sanaa na kuwasiliana na mashabiki wao.
Alisisitiza kwamba si kila kitu kinapaswa kuwekwa kwenye kurasa za kijamii za wasanii na kwamba lazima wasanii wajifunze kutenganisha maslahi au masuala yao binafsi dhidi ya yale ya wapenzi wao na kwamba Sanaa iko kwa ajili ya walaji na si wasanii pekee.
“Wasanii hawana budi kuelewa kuwa hawatengenezi sanaa au kurasa za mitandao ya kijamii kwa ajili yao. Wanaitengeneza ili kuwasiliana na mashabiki wao kuhusu kazi wazifanyazo na kutafuta fursa za masoko na kazi nje. Lazima waelewe mapromota wa kimataifa hutumia sana kurasa hizi katika kutoa fursa” alisisitiza Mdimu.
Aliongeza kwamba, msanii yeyote anayefanya kazi ya Sanaa kama kazi yake lazima afikirie kutumia mitandao hii ya kijamii kiweledi katika kujitangaza kwani kutokufanya hivyo ni bora kufanya kazi nyingine maana hiyo ndiyo njia kuu kwa sasa ya kujitangaza na kupata fursa za maonesho mbalimbali ya kimataifa kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake Afisa Sanaa kutoka BASATA, Augustino Makame alisema kwamba Baraza limekuwa mstari wa mbele kusisitiza matumizi sahihi ya teknolojia za kupashana habari muiongoni mwa wasanii na kwamba sasa ni muda wa wasanii kuona umuhimu wa mitandao hii ya kijamii na kuitumia ipasavyo katika kukuza Sanaa zao.
TASWA KUTETA NA WANAHABARI KESHO
Habari mdau, naomba kukujulisha kuwa kesho Jumatano Septemba 24, 2014, saa tano kamili asubuhi, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Juma Pinto, akiambatana na wadhamini washiriki wa Tuzo za Wanamichezo Bora Tanzania zinazoandaliwa na TASWA, watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kwenye mgahawa wa City Sports Lounge, Posta, Dar es Salaam kutangaza udhamini huo.
Pia katika mkutano huo, masuala ya Media Day Bonanza 2014 na mambo yahusiyo mafunzo kwa waandishi wa habari za michezo nayo yatazungumzwa.
Naomba ukipata taarifa hii, mjulishe na mwenzako. Karibu sana.
Ahsante,
Katibu Mkuu TASWA
0713-415346
MAKONGORO AIPA CHANGAMOTO TaSUBA
Mgeni rasmi ambaye, pia ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere (kushoto) akifuatilia maonyesho mbalimbali yaliyokua yakiendelea wakati wa uzinduzi wa Tamasha la 33 la Sanaa lililofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) jana. Katikati ni Mtendaji Mkuu TaSUBa, Michael Kadinde na kulia ni Mkurugenzi Maendeleo ya Utamaduni, Prof. Hermas Mwansoko.
Ghonche Materego wakati wa uzinduzi wa Tamasha la 33 la Sanaa lililofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) jana. Picha hii imechorwa sura ya Makongoro na msanii aliyefahamika kwa jina la Sunday Richard Kamangu.
Makongoro (kushoto) akimpa mkono wa pongezi msanii Sunday Richard Kamangu baada ya kupokea zawadi ya picha iliyochorwa na msanii huyowakati wa uzinduzi wa Tamasha la 33 la Sanaa lililofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) jana.
Baadhi ya watazamaji wakifurahia mambo yalivyokuwa wakati wa uzinduzi wa Tamasha la 33 la Sanaa lililofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) jana. Picha zote na: Genofeva Matemu - MAELEZO
Benjamin Sawe, Bagamoyo
TAASISI ya Sanaa Bagamoyo imeaswa kuendelea kutoa mafunzo ya sanaa na utamaduni ambayo yatakidhi mahitaji ya soko kwa nchi za Afrika Mashariki.
Hayo yamesemwa na Makongoro Nyerere kwa niaba ya Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Margaret Ntantongo Zziwa katika Ufunguzi wa Tamasha la 33 la sanaa na utamaduni wa Mtanzania lililofanyika katika Taasisi hiyo mjini Bagamoyo jana
Makongoro alisema Sanaa na Utamaduni vinaweza kutumiwa kuelezea masuala yote yanayomuhusu binadamu na mazingira yake hususani suala zima la utaliii
Alisema ni wakati mwafaka kwa jamii kuondokana na dhana ya kuona watalii ni wale wa kutoka nje ya nchi na kusahau kuwa wale wa ndani ambao kwa idadi kubwa ni wengi wa kuwezesha Serikali kukusanya maduhuli ya kutosha.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TaSUBa Bw. Michael Kadinde alisema sanaa hutumika kuelimisha jamii katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na Utawala Bora, kuhifadhi mazingira, madahara ya rushwa katika jamii, namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na aina nyingine nyingi za utoaji elimu katika jamii.
Alitolea mfano wa sanaa ya ngoma, nyimbo, hadidhi simulizi, majigambo, uchoraji na sanaa nyingine nyingi za makabila mbalimbali vinaeleza utamaduni wa Mtanzania hivyo huwa kitambulisho cha jamii.
Kadinde alisema sanaa huonya na kutaadhalisha jamii juu ya mambo mabaya yanayoweza kuleta madahara katika jamii ikiwa ni pamoja na kuendekeza rushwa, Vijana au jamii nzima kuwa na tabia zisizokuwa na heshima .
Aliomba Bodi ya Utalii ya Tanzania mahali palipo na vituo vya Utalii viwatumie wahitimu wa TaSUBa kuanzisha vikundi vya sanaa ili watangaze utalii wa nchi ili na kuongeza mapato ya nchi na jamii kwa ujumla
Alisema kutoa mafunzo ya Sanaa na Utamaduni kwa nchi za Afrika Mashariki kuna changamoto zake ikiwa ni pamoja na upanuzi wa miundombinu ili kukidhi mahitaji ya ufundishaji ambapo iliyopo haiwezi kubeba mzigo mzito wa kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa nchi za Afrika Mashariki.
Tamasha la Sanaa Bagamoyo lilianzishwa mwaka 1982 ambapo mwaka huu kauli mbiu yake ni “Sanaa na Utamaduni katika kukuza utalii”.
Monday, September 22, 2014
LAVEDA; MWAKILISHI WA TANZANIA BIG BROTHER AFRICA 2014
Tanzania
Laveda
Age: 23
Bachelor of Arts & Social Sciences graduate Laveda was born in Dar Es Salaam. She’s single and describes herself as ‘eccentric, loving, caring, simple and fun’. Laveda is the eldest of three children and she has a younger brother and sister. She says her mom is her role model, because she has moulded her over the years and inspired her in different ways ‘through the struggles and joy of life’.
Laveda says her favourite foods are pasta and minced meat, and prawns. She loves to read John Grisham novels and enjoys the music of Shakira, D’Banj, Miriam Makeba, P.Square, Rihanna, Beyonce, Tiwo Savage, Yvonne Chaka Chaka and Brenda Fassie. She’s a mean entertainer herself, she plays the saxophone, sings, acts and dances and thinks she’d make a ‘potential’ presenter. Laveda’s favourite movies include The Notebook, Titanic and Avatar.
She entered Big Brother Hotshots to be a role model and act as a voice for Africa’s youth. Laveda says that viewers can expect ‘massive entertainment’ from her and that if she wins, she’ll give her mom some money, ‘surprise disadvantaged children’, travel and invest the rest.
LIEWIG ATEULIWA KUWA KOCHA WA VIJANA AZAM
MFARANSA Patrick Liewig anatarajiwa kuchukua nafasi ya Mhindi, Vivek Nagul aliyeachia ngazi katika akademi ya Azam FC ya Dar es Salaam.
Katibu wa Azam FC, Nassor Idrissa Mohamed ‘Father’ amesema kwamba klabu hiyo imefikia makubaliano na Liewig, ambaye kwa sasa yupo Ufaransa na atakuja nchini mara moja kusaini Mkataba.
Nassor amesema klabu inatarajia makubwa kutoka kwa Mfaransa huyo aliyewahi kufanya kazi ASEC Mimosas ya Ivory Coast kwa mafanikio.
Amesema Vivek aliomba kuachia ngazi baada ya kupata kazi Chennayin FC ya Ligi Kuu ya kwao India, ambako anakwenda kuwa chini ya kocha Mkuu, Mbrazil, Zico na wachezaji maarufu kama Robert Pires, Edgar Marcelieno na Migeul Herlin.
Vivek alijiunga na Azam FC mwaka 2011 na katika kipindi hicho cha miaka mitatu na ushei, pamoja na kuzalisha vipaji vingi, pia ameiwezesha Akademi kushinda Kombe la Uhai mara mbili na Rollinstone mara moja
“Tunamtakia kila la kheri na ataendelea kuwa kwenye kumbukumbu zetu baada ya kuipa akademi mafanikio makubwa sana. Kazalisha nyota wengi ambao wamejaa timu zote za Ligi Kuu,” amesema Father.
Nassor amewataja baadhi ya wachezaji hao kuwa ni
Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba SC, Simon Msuva wa Yanga SC, wakati Azam A wapo
Manula Aishi, Gardiel Michael, Bryson Raphael, Mudathir Yahya, Kevin Friday, Farid Mussa Malik,
Joseph Kimwaga, Dizana issa na Mgaya Abdul.
KUHUSU LIEWIG;
Nassor amesema kwamba klabu imeridhishwa na falsafa ya ufundishaji ya Mfaransa huyo baada ya kumuona akifanya kazi Simba SC mwaka jana, hivyo kuamua kumchukua ahamishie mafanikio yake Chamazi.
Liewig ana Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller na amehudhuria pia kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dijon.
Kwa upande wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.
Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990: alikuwa Meneja Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi 1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez, 1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa Msaidizi wa Alain Giresse.
Liewig pia alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
Januari mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za U20 nchini Burkina Faso.
Kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
Amekuwa Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia.
Januari mwaka jana alitua Simba SC ambako alifanya kazi hadi mwishoni mwa msimu alipoondoka kwa sababu ya matatizo ya uongozi wa klabu hiyo
Sunday, September 21, 2014
SIMBA YABANWA MBAVU NA COASTAL UNION
TIMU kongwe ya soka ya Simba jana ilitolewa jasho na Coastal Union baada ya kulazimishwa kutoka nayo sare ya mabao 2-2 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutoka uwanjani na ushindi kwani ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 hadi mapumziko, yaliyofungwa na Shaaban Kisiga na Amisi Tambwe.
Uzembe wa mabeki wa Simba uliiruhusu Coastal Union kupata bao la kwanza dakika ya 68 lililofungwa na Yayo Lutimba kabla ya Ramadhan Salim kusawazisha dakika ya 81.
Kutokana na matokeo ya mechi za mwanzo za ligi hiyo, timu pekee iliyoibuka na ushindi mnono wa mabao ni Ndanda FC ya Mtwara, ambayo iliicharaza Stand United ya Shinyanga mabao 4-1.
YANGA YAZIMWA NA MTIBWA LIGI KUU, AZAM YACHANUA, NDANDA YAANZA KWA KISHINDO
YANGA jana ilianza vibaya kampeni ya kuwania ubingwa wa michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar.
Katika mechi hiyo iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, mshambuliaji Genilson Jaja aliikosesha Yanga bao baada ya kupoteza penalti katika kipindi cha kwanza.
Mtibwa ilipata bao la kuongoza dakika ya 15 kupitia kwa mshambuliaji wake, Mussa Hassan 'Mgosi' baada ya kupokea pasi kutoka kwa Shaaban Nditi.
Yanga ilipata penalti dakika ya 46 baada ya Mrisho Ngasa kumnawisha mpira beki Saidi Mbonde wa Mtibwa. Hata hivyo, shuti la jaja liliokolewa kwa mguu na kipa Saidi Mohamed kabla ya mabeki wake kuuondosha kwenye hatari.
Zikiwa zimesalia dakika tano pambano hilo kumalizika, jahazi la Yanga lilizidi kuzama baada ya Ali kuifungia Mtibwa bao la pili kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Nditi.
Wakati huo huo, mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Azam jana walianza vyema kutetea taji lao baada ya kuichapa Polisi Moro mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mabao yaliyoiwezesha Azam kutoka uwanjani na ushindi huo mnene yalipachikwa wavuni na Didier Kavumbagu, aliyefunga mawili na Aggrey Morris.
Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa juzi, Ndanda FC iliibamiza Stand United mabao 4-1, Mgambo JKT iliichapa Kagera Sugar bao 1-0, Ruvu Shooting ilipigwa mweleka wa mabao 2-0 na Prisons wakati Mbeya City ilitoka suluhu na JKT Ruvu.
Subscribe to:
Posts (Atom)










