KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 12, 2012

Mogella atoa tahadhari kwa Yanga






00000
MMOJA wa wanasoka waliong’ara nchini miaka ya 1980 hadi 1990 ni Zamoyoni Mogella, ambaye alikuwa maarufu zaidi kwa jina la Golden Ball. Mbali na kuwa mwanasoka nyota enzi hizo, Zamoyoni ni miongoni mwa wachezaji wachache walioweza kunufaika kimaisha kutokana na soka. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na ATHANAS KAZIGE, mchezaji huyo anazungumzia masuala mbalimbali kuhusu soka.
00000


SWALI: Wakati ukiwa Simba na baadaye Yanga, mliwahi kupambana na timu mbalimbali kutoka Misri katika michuano ya klabu za Afrika. Nini maoni yako kuhusu mechi ijayo ya klabu bingwa Afrika kati ya Yanga na Zamalek?
JIBU: Ninachoweza kuwashauri viongozi na wachezaji wa Yanga ni kwamba, wajiandae vizuri kabla ya kukabiliana na Zamalek kwa sababu ni timu nzuri na tishio kisoka barani Afrika, ikiwa imewahi kutwaa ubingwa mara kadhaa.
Ni kweli nina uzoefu mkubwa na timu za Misri. Ni timu zenye uzoefu mkubwa na mbinu za kila aina, ndani na nje ya uwanja.
Pia ni timu zenye uwezo mkubwa kifedha na viongozi wao hutoa ahadi nono ya pesa kwa wachezaji wao kila zinapokabiliwa na mechi ngumu na muhimu hiyo ni miongoni mwa sababu zinazozifanya timu zao zifanye vizuri.
Mashabiki wa timu hizo pia wana umoja, hasa timu mojawapo inapokuwa ikiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa, tofauti na hapa kwetu, ambapo mashabiki wa timu moja huweza kuwazomea wapinzani wao na kuwapa nguvu wageni. Kwa Wamisri, hilo halipo kabisa.
Kuna mbinu moja inayotumiwa sana na wachezaji wa Misri ya kujiangusha hovyo uwanjani na iwapo mwamuzi hatakuwa makini, ni rahisi kwa timu yao kushinda, hasa wanapocheza nyumbani.
SWALI: Unadhani ni kipi kinachotakiwa kufanywa na Yanga ili iweze kuitoa Zamalek na kusonga mbele?
JIBU: Mazoezi ndiyo siri pekee ya ushindi. Wachezaji wanapaswa kujifua kwa nguvu zote ili kuhakikisha timu inakuwa fiti. Litakuwa jambo zuri zaidi iwapo timu itapatiwa mechi za kirafiki za kimataifa kabla ya kukabiliana na Zamalek.
SWALI: Kumekuwepo na mgogoro wa chini kwa chini kati ya uongozi, kocha na wachezaji kuhusu mishahara kucheleweshwa. Unadhani hili linaweza kuiathiri Yanga katika mechi hii?
JIBU: Nadhani kuna umuhimu mkubwa kwa wachezaji wa Yanga kuandaliwa kisaikolojia, si kwa sababu ya mgogoro huo, bali pia kuwaandaa wachezaji kimashindano.
Kwa maoni yangu, nadhani wakati umefika kwa Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kuajiri mtaalamu wa masuala ya kisaikolojia kwa lengo la kuwaandaa wachezaji wa timu ya taifa na za klabu zinaposhiriki michuano ya kimataifa.
Mtaalamu huyo ni muhimu kwa vile wachezaji wengi wa Tanzania hawajitambui kwamba wana vipaji, ndio sababu wanashindwa kucheza soka kwa miaka mingi. Wengi hustaafu kucheza soka baada ya muda mfupi.
Binafsi ningependa kuona klabu za ligi kuu nazo zinaajiri wataalamu wa aina hii ili ziweze kuwaandaa wachezaji wake kimashindano badala ya ilivyo sasa, ambapo wanashindwa kujitambua na kutambua umuhimu wa soka kwao. Wachezaji wanapaswa kuandaliwa vyema kabla ya mashindano.
SWALI: Kwanini unasisitiza sana suala la wachezaji kuandaliwa kisaikolojia?
JIBU: Nimefanya uchunguzi na kubaini kwamba, timu za Tanzania zinaundwa na wachezaji wengi wazuri na wenye uwezo wa kufika mbali, lakini hawajitambui.
Wapo baadhi ya wachezaji wetu wenye vipaji vya soka kama ilivyo kwa Samuel Eto’o wa Cameroon, lakini wanashindwa kuonyesha uwezo wake kutokana na kutojitambua.
Matokeo yake ni kwamba, vipaji vya wachezaji wetu wengi hufifia baada ya muda mfupi na wengine kuupa kisogo mchezo huo kwa kuona hauna manufaa kwao.
Ninaamini wakiwepo wataalamu wa saikolojia, wataweza kuwasaidia wachezaji na kuwafanya wajitambue na hivyo kuuona mchezo wa soka ni ajira kubwa kwao.
SWALI: Umeshatazama mechi nyingi za michuano ya ligi na zile zinazoihusisha timu ya taifa, Taifa Stars. Umegundua tofauti ipi ya uchezaji enzi zenu na hivi sasa?
JIBU: Tofauti ipo kubwa. Enzi zetu tulikuwa tunacheza soka kwa mapenzi, lakini hivi sasa soka ni pesa. Wachezaji wanalipwa vizuri na kupata zawadi nyingi, hasa wale wa Taifa Stars, lakini inashangaza kuona kuwa, hakuna mafanikio.
Kwa kawaida, mchezaji anatakiwa kulipwa vizuri ili aweze kutimiza malengo yake. Enzi zetu mapenzi ndiyo yaliyotufanya tucheze kwa bidii na kujituma. Wachezaji walikuwa wanajitolea zaidi.
Lakini hivi sasa huwezi kusikia mchezaji anasajiliwa bila kulipwa pesa. Ujio wa baadhi ya wafadhili umesaidia sana kuongeza ushindani, hivyo kinachotakiwa ni kwa wachezaji kuongeza ushindani, kuwa na ari na kujituma.
Enzi zetu timu zilikuwa chache na zilimilikiwa na taasisi mbalimbali za serikali na ndio sababu wachezaji wake walicheza kwa kujituma. Timu kama RTC Kagera, Pamba ya Mwanza, Pilsner na Reli ya Morogoro ni miongoni mwa timu zilizokuwa zikitamba enzi hizo.
Wachezaji wa sasa hawachezi kwa kujituma sana. Wanafanya hivyo pale tu wanapoahidiwa kupewa zawadi. Pia kumezuka matabaka kwenye baadhi ya timu. Kuna wachezaji wanaolipwa pesa nyingi na wanaolipwa pesa kiduchu. Hali hii inachangia kutokuwepo kwa umoja na kushuka kwa ari ya wachezaji.
Kibaya zaidi, wamezuka baadhi ya viongozi, ambao wanaingia madarakani si kwa lengo la kuendeleza soka, bali kujinufaisha wao binafsi. Watu wa aina hii ni hatari kwa maendeleo ya soka.
SWALI: Unapenda kutoa ushauri gani kwa TFF ili yawepo mabadiliko katika uendeshaji soka nchini?
JIBU: Nawashauri viongozi wa TFF wawe makini kuwekeza nguvu zaidi katika kukuza vipaji vya vijana na kuwaendeleza.Hakuna njia ya mkato ya kupata maendeleo zaidi ya kuwekeza katika soka ya vijana.
Nchi nyingi zilizoendelea kisoka barani Afrika, zimepata mafanikio kutokana na kuwekeza kwa vijana. Tazama nchi kama Senegal, Ivory Coast, Ghana na Cameroon, zinatisha kisoka kwa sababu ya kutilia mkazo soka ya vijana. Nasi tunapaswa kuiga mfano huo.
SWALI: Unatoa mwito gani kuhusu watu wanaoingia katika michezo kwa lengo la kujinufaisha?
JIBU: Nawashauri wanachama wa klabu za soka nchini na wajumbe wa vyama vya soka vya wilaya, mikoa na TFF taifa, kuhakikisha wanawachagua watu wenye uwezo, mwelekeo na mapenzi ya soka. Wasithubutu kuwachagua watu wasiokuwa na historia yoyote ya soka, ambao mara nyingi lengo lao ni kujinufaisha wao binafsi badala ya kuleta maendeleo.
Vilevile navishauri vyombo vinavyochuja wagombea katika chaguzi mbalimbali, kutowaonea aibu wagombea wasiokuwa na mwelekeo wa kimichezo. Wanapowaruhusu wagombea wa aina hii kuwania uongozi, ndipo wanapokaribisha matatizo.
Kwa sasa, wapo viongozi wengi wa soka, ambao hawana rekodi zozote za maana, ikiwa ni pamoja na kucheza soka au hata kuongoza timu za mitaani, lakini wanazo pesa nyingi na ndizo zinazowawezesha kushinda nafasi wanazogombea.
SWALI: Ungependa kutoa ushauri gani kwa viongozi wa serikali kuhusu michezo?
JIBU: Naishauri Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhakikisha michezo inaendelezwa zaidi katika ngazi za shule za msingi, sekondari na vyuo, ambako ndiko chimbuko la wanamichezo. Pia ihakikishe walimu wa michezo wanapatiwa mafunzo ya kitaalamu ili waweze kuinua viwango vya michezo mbalimbali katika ngazi hizo.
Naiomba pia serikali kwakushirikiana na halmashauri za wilaya kuhakikisha wavamizi wote wa viwanja vya michezo wanaondolewa ili kutoa nafasi kwa watoto wetu kuvitumia viwanja hivyo kucheza michezo mbalimbali.

Wednesday, January 11, 2012

Mzee Kipara afariki


MMOJA wa waigizaji wakongwe wa maigizo na vichekesho nchini, Fundi Saidi ‘Mzee Kipara’ amefariki dunia.
Habari zilizopatikana mjini Dar es Salaam leo zimeeleza kuwa, Mzee Kipara alifariki dunia saa tatu asubuhi nyumbani kwake Kigogo.
Kwa mujibu wa habari hizo, Mzee Kipara alifikwa na mauti baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi mbalimbali, yakiwemo ya kuvimba miguu.
Mzee Kipara alijipatia umaarufu mkubwa kuanzia miaka ya 1970 alipokuwa akishiriki michezo ya kuigiza iliyokuwa ikirushwa hewani na Radio Tanzania Dar es Salaam.
Mkongwe huyo aliendelea kujizolea umaarufu baada ya kujitosa kwenye fani ya filamu, ambapo alishiriki kucheza tamthilia mbalimbali zilizokuwa zikiandaliwa na kikundi cha Kaole.

Tuesday, January 10, 2012

BASATA YAONYA MAPROMOTA WABABAISHAJI

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewaonya wakuzaji sanaa nchini kuacha mara moja ubabaishaji wanapokuwa wanaendesha matukio na matamasha mbalimbali ya Sanaa.
Onyo hilo limetolewa mapema wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Sanaa wa Baraza hilo, Vivian Nsao Shalua wakati akiongea na wadau wa Sanaa kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika kwenye ukumbi wa BASATA uliopo Ilala Sharifu Shamba.
Shalua alisema kuwa, Mapromota wamekuwa wakiwarubuni wasanii kwa kuwafanyisha kazi zisizo na mikataba huku wao wakinufaika na kuwaacha wasanii wakishindwa kujikwamua kimaisha.
“Utaratibu uliopo sasa kila mdau yeyote anapoandaa tamasha au tukio lolote linalohusisha wasanii lazima aje na mikataba na wasanii hao, aoneshe uwezo wake kifedha katika kuendesha tukio lakini pia awe na kamati inayoeleweka ya uendeshaji” alisisitiza Shalua.
Aidha, aliongeza kuwa, kumekuwa na ukiukwaji kanuni na taratibu za uendeshaji matukio hayo ambapo Baraza limekuwa likiwapa onyo na kuwafungia wahusika lakini akasisitiza kuwa, njia pekee ya kuepuka hali hii ni kwa mapromota kufuata taratibu zilizopo.
Akizungumzia kuhusu suala la mikataba, aliwataka Wasanii kuhakikisha hawashiriki tukio au onyesho bila kuwa na mkataba na waandaaji kwani hali hiyo inawafanya wadhulumiwe na kushindwa kudai haki zao kwa mujibu wa makubaliano.
“Ni lazima sasa wasanii wadai mikataba. Sisi tunawabana wakuzaji sanaa (mapromota) kuambatanisha mikataba yao kabla hatujawapa kibali lakini lazima na wasanii waoneshe wajibu wao kwa kudai mikataba na kutoshiriki maonyesho bila makubaliano ya maandishi” alionya Shalua.
Alisisitiza kuwa, Baraza litakuwa makini katika kufuatilia wadau wanaopewa vibali vya kuendesha matamasha na matukio mbalimbali ya Sanaa na mara taratibu na kanuni zitakapokiukwa halitasita kuchukua hatua za makusudi

AHADI YA WAZIRI MKUU KWA STARS



Waziri Mkuu Mizengo Pinda tayari amekabidhi sh. milioni 10 kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ikiwa ni ahadi yake aliyotoa kwa Taifa Stars ikiwa ni motisha kwa wachezaji wa timu hiyo kabla ya mechi yao na Chad iliyochezwa Novemba Mosi mwaka jana jijini N’Djamena.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia kwa Meneja wa Taifa Stars, Leopold Tasso linaanda orodha ya wachezaji wanaostahili kunufaika na ahadi hiyo, na baadaye kuiwasilisha BMT kwa ajili ya mgawo kwa wahusika.

Tunamshukuru Waziri Mkuu Pinda kwa ahadi hiyo, kwani Taifa Stars ilifanikiwa kushinda mechi hiyo ya ugenini mabao 2-1, ushindi ambao bila shaka ulichagizwa na ahadi hiyo.

KUUZWA KWA TIMU YA SMALL KIDS

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana Desemba 30 mwaka jana ilijadili masuala mbalimbali yaliyofikishwa mbele yake ikiwemo malalamiko juu ya kuuzwa kwa timu ya Small Kids ya Rukwa.

Usikilizaji wa suala hilo uliahirishwa na Kamati kuagiza kwanza ipatiwe vitu vifuatavyo; Katiba iliyosajiliwa ya Small Kids, muhtasari (minutes) na uamuzi wa kikao chochote kilichofanyika kuzungumzia mauzo ya timu hiyo ambayo iko daraja la kwanza.

Pia Kamati inataka ipatiwe mawasiliano (correspondences) yote yaliyofanyika kuhusiana na ununuzi/mauzo ya timu hiyo. Hivyo suala hilo litasikilishwa katika kikao kingine cha kamati baada ya kuwasilishwa nyaraka hizo.


MGOGORO WA UONGOZI TAREFA

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji itatuma wajumbe wake wawili Tabora kukutana na Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA).

Wajumbe hao katika kikao chao na Kamati ya Utendaji ya TAREFA watasikiliza kuhusu kiini cha mgogoro uliopo na baadaye watawasilisha taarifa kwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji. Kamati itafanyia kazi ripoti hiyo kabla ya kufanya uamuzi.


MAREKEBISHO YA KATIBA ZA WANACHAMA

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji pia ilifanyia kazi suala la marekebisho ya katiba za wanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Katiba hizo zimegawanywa katika makundi matatu; katiba za wanachama wapya, katiba ambazo tayari zimerekebishwa na katiba ambazo hazijarekebishwa.

Maelekezo ya Kamati ni kuwa itatoa mwelekeo (roadmap) utakaoonesha muda wa mwisho (deadline) wa kufanya marekebisho kwa makundi yote hayo matatu ambapo kwa wanachama watakaoshindwa hawataruhusiwa kuingia kwenye Mkutano Mkuu wa TFF.

Maeneo ya msingi ya marekebisho ni sifa za uongozi. Katiba zote za wanachama wa TFF kwa upande wa sifa za uongozi ni lazima ziwe sawa. Maeneo mengine ni kuainishwa wazi kwa majukumu ya Kamati ya Utendaji, Mkutano Mkuu na namna ya kutatua migogoro ya wanachama ili kuepuka watu kwenda mahakamani.

Monday, January 9, 2012

MECHI LIGI KUU KUCHEZWA SIKU TATU KWA WIKI



Siku za mechi (match days) kwa Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2011/2012 ambayo itaanza mzunguko wake wa pili Januari 21 mwaka huu sasa itakuwa ni Jumamosi, Jumapili na Jumatano tu.

Uamuzi huo umefanya na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Januari 5 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine ilikuwa kupitia ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom na ile ya Daraja la Kwanza.

Kutokana na kituo cha Dar es Salaam kuwa na timu saba kati ya 14 za Ligi Kuu zinazotumia viwanja viwili tu (Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Azam), kamati imepitisha uamuzi kuwa mechi mbili zinaweza kuchezwa kwa wakati mmoja (Taifa na Azam) ili ligi ichezwe ndani ya kalenda.

Timu zinazotumia viwanja hivyo kama vya nyumbani katika Ligi Kuu ya Vodacom ni African Lyon, Azam, JKT Ruvu Stars, Moro United, Villa Squad, Simba na Yanga.

LIGI DARAJA LA KWANZA FEBRUARI 4

Mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara inayochezwa katika makundi matatu tofauti kwa mtindo wa nyumbani na ugenini itaanza Februari 4 mwaka huu.

Timu zitakazomaliza katika nafasi tatu za juu zitacheza hatua ya fainali itakayokuwa na timu tisa. Kundi A lenye timu za Burkina Faso ya Morogoro, Mgambo Shooting ya Tanga, Morani ya Manyara, Polisi ya Dar es Salaam, Temeke United ya Dar es Salaam na Transit Camp ya Dar es Salaam litaanza ligi hiyo kwa mechi moja kati ya Morani na Burkina Faso itakayochezwa mkoani Manyara.

Februari 4 mwaka huu katika kundi B kutakuwa na mechi kati ya Small Kids ya Rukwa na Polisi ya Iringa itakayochezwa mjini Morogoro, Mbeya City na Tanzania Prisons zitaumana Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya wakati Majimaji na Mlale JKT wataoneshana kazi Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Kundi C mechi za ufunguzi zitakuwa kati ya Manyoni FC na AFC itakayofanyika mjini Singida, Rhino FC dhidi ya Polisi ya Tabora zitacheza Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora wakati 94 KJ na Polisi ya Morogoro zitakwaruzana Februari 5 mwaka huu mjini Mlandizi.

16 WAOMBA AJIRA YA OFISA WA LIGI

Mchakato wa kumpata Ofisa wa Ligi bado unaendelea. Kamati ya Ligi ilipitia maombi ya watu 16 yaliyowasilishwa TFF kwa nafasi ya Ofisa huyo kwa ajili ya Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza. Mwisho wa kutuma maombi ilikuwa Desemba 28 mwaka jana.

Maombi yote 16 yalipitiwa ambapo waliopita katika mchujo huo wa kwanza wataitwa kwa ajili ya usaili. Waombaji wataarifiwa siku ya usaili kupitia mawasiliano waliyotumia wakati wanawasilisha maombi yao.


KANYENYE AREJESHEWA KIBENDERA FIFA

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limemthibitisha tena mwamuzi msaidizi John Kanyenye wa Tanzania kuingia katika orodha yake kwa mwaka 2012.

Awali FIFA ilituma TFF majina ya jumla ya waamuzi 14 wa Tanzania wakiwemo waamuzi wasaidizi wawili wapya kwa ajili ya mwaka 2012.

Jina la Kanyenye halikuwamo katika orodha hiyo iliyokuwa imetumwa awali. Kwa vile Kanyenye alikuwamo katika orodha ya waamuzi wa Tanzania wanaotambuliwa na Shirikisho hilo kwa mwaka 2011 na jina lake halikurudi, TFF ililazimika kuiandikia FIFA ili kupata ufafanuzi wa kuenguliwa kwa Kanyenye.

Uamuzi wa FIFA kumrejesha Kanyenye kwenye orodha inaifanya Tanzania sasa kuwa na jumla ya waamuzi 15. Waamuzi wa kati ni Israel Mujuni, Judith Gamba, Orden Mbaga, Ramadhan Ibada na Sheha Waziri. Waamuzi wasaidizi ni Ali Kinduli, Erasmo Clemence, Ferdinand Chacha, Hamisi Chang’walu, John Kanyenye, Josephat Bulali, Khamis Maswa, Mwanahija Makame, Saada Tibabimale na Samuel Mpenzu.

KWADWO: Tumepania kufanya maajabu CAN 2012


ROME, Italia
KWADWO Asamoah ni mmoja wa wachezaji wa kimataifa wa Ghana wanaotamba kisoka barani Ulaya kutokana na uwezo mkubwa alionao katika kusakata kabumbu.
Kiungo huyo anayekipiga katika klabu ya Udinese ya Italia, alianza kung’ara mwaka 2010 alipoichezea Ghana katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Afrika Kusini.
Katika mwaka huo, Asamoah aliichezea Ghana katika mechi zote za Kombe la Mataifa ya Afrika na kufuzu kucheza fainali na pia katika mechi za Kombe la Dunia, ambapo Ghana iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kufuzu kucheza robo fainali.
Kwadwo (23) ni mchezaji mwenye kasi, nguvu na mbinu za aina yake za kuwatoka mabeki wa timu pinzani. Hivi karibuni, alishinda tuzo ya mchezaji bora mwenye kipaji anayechipukia barani Afrika.
Chipukizi huyo wa Ghana alikuwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Udinese kumaliza msimu wa ligi ya Serie A ya Italia mwaka 2011 ikiwa ya tatu. Mekeke yake uwanjani yalizifanya klabu nyingi za Ulaya kuanza kumkodolea macho, ikiwemo Manchester United ya England.
Kwadwo ni mmoja wa wachezaji waliomo kwenye kikosi cha Ghana, kinachotarajiwa kushiriki katika fainali za mwaka huu za Kombe la Mataifa ya Afrika zinazotarajiwa kufanyika Equatorial Guinea na Gabon.
Ghana ni miongoni mwa nchi zinazopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye fainali hizo huku Kwadwo akitarajiwa kung’ara na hivyo kuzivutia zaidi klabu za Ulaya.
Akihojiwa na mtandao wa FIFA hivi karibuni, mwanasoka huyo amekiri kuwa, licha ya Udinese kuuza wachezaji wake nyota kadhaa msimu huu, lakini imeweza kuanza vyema katika ligi ya Serie A na ligi ya Ulaya.
Alisema msimu uliopita, walicheza vizuri na kupambana na timu ngumu, ambazo ziliwasaidia kuwafanya wachezaji wajiamini na hivyo kupata matokeo mazuri.
Kwadwo alisema mafanikio ya Udinese yamechangiwa na timu hiyo kuundwa na wachezaji wengi vijana na wenye kiu ya kupata mafanikio makubwa zaidi kisoka.
‘Timu yetu ni mojawapo yenye wachezaji wenye umri mdogo katika ligi ya Serie A. Tunasaidiana kwa hali na mali uwanjani na tuna umoja wa aina yake. Mwelekeo wetu ni kama ilivyokuwa mwaka jana, japokuwa wamekuja wachezaji kadhaa wapya, ‘ alisema.
Kwadwo amekiri kuwepo kwa tofauti kiuchezaji katika klabu ya Udinese na timu ya taifa. Akiwa Udinese anacheza nafasi ya kiungo mkabaji wakati akiwa kikosi cha Ghana, anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji.
‘Nikiwa Ghana nacheza nyuma ya mshambuliaji wa kati, Asamoah Gyan wakati nikiwa Udinese, nimejifunza kucheza kama kiungo mkabaji nafasi ya kushoto na kusaidia sehemu zote za uwanja. Wakati mwingine hutokea nikacheza nafasi ya ulinzi, ‘alisema.
Kwadwo alitamba kuwa, Ghana ina matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika fainali za Afrika kwa vile timu yao ni nzuri, inaundwa na wachezaji wenye kiwango cha juu kisoka na haina matatizo.
Alisema kama watacheza kwa ari na kujituma, kama ambavyo Kocha Goran Stevanovic amekuwa akiwasisitizia, watakuwa tishio kwa timu yoyote watakayocheza nayo.
Kiungo huyo alikiri kuwa, kutokuwepo kwa timu ngumu kama vile Misri, Cameroon na Nigeria katika fainali hizo, kutapunguza ladha ya ushindani, lakini alisisitiza kuwa, kutwaa ubingwa ni kazi ngumu.
‘Siku zote zimekuwa zikijitokeza timu mpya, ambazo hutoa ushindani mkali kwa timu yoyote. Timu zote zilizofuzu kucheza fainali hizi zilistahili,’ alisema.
Kwadwo hakuwa tayari kutabiri timu inayoweza kutwaa ubingwa. Alisema timu zote zitaanza fainali hizo zikiwa katika kiwango sawa, lakini alikiri kuwa huenda yakajitokeza matokeo ya kushangaza.
Akizungumzia michuano ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014, Kwadwo alisema Zambia ndiyo timu pekee ya kuihofia katika kundi lao. Timu zingine zilizopangwa kundi hilo ni Sudan na Lesotho.
Kwadwo alisema hakushangazwa Ghana ilipotolewa hatua ya robo katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 kwa sababu hivyo ndivyo mchezo wa soka ulivyo.
“Ndivyo soka ilivyo. Kuna wakati mbaya na vipigo visivyotarajiwa. Jambo zuri ni kwamba siku zote unakuwa na nafasi ya kujirekebisha,”alisema.
“Tulikaribia kufuzu kucheza nusu fainali, lakini dakika za mwisho tulikosa penalti, ambayo ingetuwezesha kuweka historia, lakini inaweza kutokea. Tuna matumaini ya kujirekebisha katika fainali zijazo. Ningependa kupata nafasi hiyo,” aliongeza.
Kwadwo alisema anafurahia maisha nchini Italia, ikiwa ni pamoja na kuichezea Udinese, ambayo alijiunga nayo miaka minne iliyopita.
Pamoja na kuwepo Italia kwa miaka minne, Kwadwo alisema hafikirii kubadili uraia kwa sababu anafurahia asili yake. Lakini alisisitiza kuwa, anafurahia kuishi Italia.
Kiungo huyo alisema pia kuwa, anafurahia chakula cha kiitaliano, lakini anafurahia zaidi kula pasta na ubwabwa, japokuwa wakati mwingine hukikumbuka chakula chao cha asili cha fufu.

Omotola na wenzake wanusurika kufa baharini


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa kike nchini Nigeria, Omotola Jalade pamoja na mwongoza filamu, Teco Benson wamenusurika kufa baharini baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzima ghafla.
Tukio hilo lilitokea hivi karibuni wakati Omotola, Benson pamoja na waigizaji wengine 22 pamoja na wapiga picha walipokuwa wakiigiza filamu ya Blood In The Lagoon.
Habari za uhakika kutoka eneo la tukio zimeeleza kuwa, boti hiyo ilikuwa imekodishwa na Benson kwa ajili ya kuwasafirisha waigizaji hao kurudi Lagos wakitokea kisiwa cha Victoria.
Kwa mujibu wa habari hizo, boti hiyo ilikwama ghafla ilipokuwa ikikaribia kisiwa hicho kilichopo kwenye bahari ya Atlantiki na kusababisha mtafaruku wa aina yake miongoni mwa waigizaji hao.
Vyanzo vya habari vimeeleza kuwa, kukwama kwa boti hiyo baharini kulitokana na kuishiwa mafuta kwenye tanki.
Akihojiwa kuhusu tukio hilo, Benson alisema halikuwa kosa lao, bali la wamiliki wa boti hiyo. Alisema waliishiwa mafuta wakati walipokuwa wakirejea kutoka kwenye eneo la kupiga picha za filamu yake mpya.
“Tulikodi boti kwa gharama kubwa, lakini pengine hawakutazama kiwango cha mafuta kilichokuwemo kabla ya kutusafirisha. Tulikuwa watu kama 22 kwenye boti,”alisema.
“Wakati tukio hilo lilipotokea, tulikuwa tukikaribia ubalozi wa Marekani na tulikuwa na wasiwasi huenda walinzi wake wangetushambuliaji kwa kuhisi sisi ni magaidi, lakini hakuna kilichotokea,”aliongeza.
Benson alisema wamiliki wa boti hiyo waliwasiliana na wenzake, ambao walifika na boti nyingine baadaye na kuwaondoa kwenye eneo hilo la hatari.
Kwa mujibu wa Benson, walidumu kwenye eneo hilo la bahari kwa muda wa kama dakika 45 kabla ya kuokolewa.
“Hakukuwa na cha zaidi, lakini wanawake waliokuwemo kwenye boti walionyesha hofu kubwa na kufikiri wanaweza kufa baharini. Tunamshukuru Mungu hakuna kibaya kilichotokea,”alisema.
“Lilikuwa tukio la kufurahisha, tulipiga picha za filamu ya Blood Ine Lagoon na kuhisi Lagoon alitaka damu zetu halisi,”aliongeza Benson huku akicheka.

UKWA: Nimepata mchumba





LAGOS, Nigeria
MWIGIZAJI machachari wa Nigeria, Osita Iheme, maarufu kwa jina la Ukwa, ametangaza kuwa naye amepata mchumba na wanatarajia kufunga ndoa hivi karibuni.
Ukwa ametoa taarifa hiyo siku chache baada ya swahiba wake mkubwa na mwigizaji mwenzake, Chinedu Idekieze ‘Aki’ kufunga ndio na Nneoma.
Hata hivyo, Ukwa hakuwa tayari kutaja jina la mchumba wake huyo, mwonekano wake ama taarifa zozote zaidi kuhusu kufunga naye ndoa.
Ukwa alisema amefurahishwa na uamuzi wa rafiki yake, Aki kufunga ndoa na kuongeza kuwa, ameamua kufuata nyayo zake.
“Nami nimepata mpenzi. Niko makini katika uhusiano wetu wa kimapenzi,”alisema Aki na kumtaka mwandishi wa mtandaji wa filamu za Kinigeria kuwa na subira kabla hajaweka mambo hadharani.
Ukwa pia alieleza kufurahishwa kwake na uamuzi wa serikali ya Nigeria kuwapa tuzo baadhi ya waigizaji nyota wan chi hiyo, akiwemo yeye.
“Ni jambo zuri na la kufurahisha kuwa miongoni mwa watu maarufu nchini Nigeria. Nilipokosa nafasi hii mwaka jana, niliwaeleza watu kwamba zamu yangu inakuja,”alisema mcheza filamu huyo.
“Na hatimaye zamu yangu sasa imefika. Nina furaha kubwa sana. Namshukuru Rais Goodluck Jonathan kwa kunipa heshima hii. Naahisi siwezi kumwangusha,”aliongeza.
Ukwa amecheza filamu zaidi ya 100 akishirikiana na Aki. Filamu yao ya kwanza iliyowapatia umaarufu inajulikana kwa jina la Aki na Ukwa.
Wachezaji filamu hao wawili wafupi na wenye vituko, kwa sasa ni miongoni mwa wasanii tajiri nchini Nigeria, wakiwa wanamiliki nyumba katika mini ya Aba, Enyimba na Abia na pia magari ya kifahari.
Ukwa anaishi Ogba, Ikeja nje kidogo ya Jiji la Lagos. Kwa sasa, wacheza filamu hao wamepanga kujenga jengo la pamoja katika mji huo.

Azam yazua balaa Yanga

HALI si shwari kwa klabu ya Yanga baada ya baadhi ya wachezaji nyota wa timu hiyo kutishia kugoma kwa madai ya kupinga kulipwa nusu ya mishahara yao.
Tishio la wachezaji hao limekuja siku moja baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 3-0 na Azam katika mechi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Kipigo ilichokipata Yanga kimeifanya ifungashe virago katika michuano hiyo na timu hiyo ilitarajiwa kurejea Dar es Salaam jana jioni kwa boti ikitokea Zanzibar.
Wakizungumza na Mzalendo kwa njia ya simu kutoka Zanzibar jana, baadhi ya wachezaji hao walisema uamuzi wa uongozi kuwalipa nusu ya mshahara kila mchezaji haukuwafurahisha.
Wachezaji hao, ambao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini walisema, kabla ya kwenda Zanzibar, walikutana na kujadiliana kuhusu uamuzi wa uongozi kuwalipa mishahara nusu.
Mmoja wa wachezaji hao alisema, kitendo hicho kiliwafanya wagawanyike, ambapo wengine walikubali kwenda Zanzibar kushiriki mashindano hayo huku wengine wakigoma.
Hata hivyo, mchezaji huyo alisema baada ya mvutano mkali kati yao, walikubali kwenda Zanzibar, lakini walitaka wakutane na uongozi ili kujadili tatizo hilo.
Kufuatia uongozi kushindwa kueleza hatma yao, mchezaji mwingine alisema, wamepanga kugoma kufanya mazoezi hadi watakapomaliziwa mishahara yao.
“Huo ndio msimamo tuliofikia kwa sababu hali kwa kweli ni mbaya sana, kila mchezaji ana matatizo na viongozi wetu hawatujali. Hatuelewi tutaishi vipi,”alisema mmoja wa wachezaji waandamizi wa klabu hiyo.
Tishio la mgomo la wachezaji hao limekuja siku chache baada ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic kupasua jipu, akieleza kuwa, wachezaji na benchi la ufundi hawajalipwa mishahara kwa miezi miwili.
Alipoulizwa kuhusu tishio hilo la wachezaji jana, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema hana taarifa yoyote.
Sendeu alisema anachofahamu ni kwamba, timu ilitarajiwa kurejea Dar es Salaam jana jioni na kuingia moja kwa moja kambini kujiandaa kwa mechi yao ya awali ya michuano ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri.
Akizungumzia kipigo cha juzi kutoka kwa Azam, Sendeu alisema ni matokeo ya kawaida ya mchezo na kwamba hakiwezi kusababisha timu yao isambaratike.
Katika mechi ya juzi, Azam ilijipatia mabao yake kupitia kwa John Boko na Kipre Tchetche, aliyefunga mabao mawili.
Wakati huo huo, Mafunzo juzi ilifuzu kucheza nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuichapa Kikwajuni bao 1-0 katika mechi iliyochezwa jioni kwenye uwanja huo.
Bao pekee na la ushindi la Mafunzo lilipachikwa wavuni na mshambuliaji Sadik Habib dakika ya 59.

BAUSSI: Tulishinikizwa kuibeba Simba

NA ABOUD MAHMOUD,ZANZIBAR
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Miembeni United, Salum Baussi Nassor amefichua siri kuwa, walilazimishwa waibebe Simba katika michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Baussi alifichua siri hiyo juzi mara baada ya timu yake kuchapwa mabao 4-3 na Simba katika mechi ya michuano hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
Mbali na kufichua siri hiyo, Baussi ametangaza kujiuzulu kuifundisha timu hiyo kwa madai kuwa, shinikizo alilopewa la kuibeba Simba limeshusha hadhi yake.
“Kusema kweli kitendo kilichofanywa na uongozi wa Miembeni kulilazimisha benchi la ufundi kuibeba Simba katika mechi hiyo kimeonyesha dharau kubwa kwetu na kunishushia hadhi mimi binafsi,”alisema kocha huyo huku akionyesha sura ya masikitiko. Baussi alisema tangu alipoanza kufundisha soka visiwani Zanzibar, hajawahi kukutana na tukio la aina hiyo na kuongeza kuwa, huko ni kudumaza maendeleo ya mchezo huo.
Kocha huyo alisema timu yoyote inapaswa kushinda mechi kutokana na uwezo wake na si kubebwa na timu pinzani na kwamba mashabiki wamekoseshwa burudani waliyoitarajia.
“Viongozi walishinikiza tuiachie Simba ishinde ili yapatikane mapato mengi katika mechi ya fainali. Kitendo hiki kimeniumiza sana na kwa kweli kimenishushia hadhi yangu,”alisisitiza mchezaji huyo wa zamani wa Zanzibar.
Alisema katika mechi hiyo, wachezaji wake walionyesha uwezo wa juu wa kucheza soka ikilinganishwa na wapinzani wao, lakini wamevunjwa moyo kutokana na shinikizo lililotolewa na uongozi.
Hata hivyo, Baussi hakuwa tayari kutaja majina ya viongozi wa Miembeni waliotoa shinikizo hilo, lakini baadhi ya vyombo vya habari jana vilimtaja mmiliki mkuu wa timu hiyo, Ahmed Makungu.
Baussi alisema wakati sasa umefika kwa watanzania kuacha kuzipa kipaumbele Simba na Yanga katika soka kwa vile kufanya hivyo kunadumaza vipaji vya wanasoka chipukizi.
Katika mechi hiyo, Simba ilijipatia mabao yake kupitia kwa Felix Sunzu, aliyefunga mawili, Patrick Mafisango na Haruna Moshi. Mabao ya Miembeni yalifungwa na Peter Elanda, Issa Othman na Ibrahim Khamis.

Thursday, January 5, 2012

Yanga yaiadhibu Kikwajuni



NaHamad Hija, Maelezo, Zanzibar

MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Yanga jana waliona mwezi baada ya kuichapa Kikwajuni mabao 2-0 katika mechi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.

Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa Yanga katika michuano hiyo iliyoanza kutimua vumbi mwishoni mwa wiki iliyopita. Katika mechi yake ya kwanza, Yanga ilichapwa bao 1-0 na Mafunzo.

Iliwachukua Yanga dakika 24 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Jerry Tegete kwa shuti kali, ambali kipa wa Kikwajuni alishindwa kulizuia. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Zikiwa zimesalia dakika tano pambano hilo kumalizika, Yanga iliongeza bao la pili kupitia kwa mshambuliaji wake, Pius Kisambale.

Mashindano hayo ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar zinazotarajiwa kufikia kilele Januari 12 mwaka huu.

Hard Mad ahimiza uzalendo kwanza



BAADA ya ukimya wa muda mrefu, msanii machachari wa muziki wa miondoko ya dance hall na raga nchini, Hard Mad ameibuka na kibao kipya.
Hard Mad alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, kibao chake hicho kinakwenda kwa jina la Uzalendo kwanza.
Msanii huyo aliyetengeneza nywele zake kwa mtindo wa rasta alisema, kibao hicho kimelenga kukemea matendo mbalimbali yanayotokea katika jamii.
“Ninachokisisitiza katika wimbo huo ni kuwataka wafanyakazi maofisini na kwenye ofisi za serikali waweke uzalendo mbele katika kazi zao,”alisema.
Hard Mad amewataka mashabiki wake watarajie vitu vipya na vikali kwa mwaka 2012 kwa vile ameamua kutoka kivingine.
Hivi karibuni, msanii huyo aliipua kibao kikali kinachojulikana kwa jina la Ujio mpya, akiwa amemshirikisha msanii Enika.
“Napenda kuwaambia wasanii wangu kwamba watarajie vitu vya kikubwa na ujio mpya kwa sababu hata jina langu sasa limebadilika. Kwa sasa najulikana kwa jina la Mkushi Moja,”alisema msanii huyo.
Hard Mad alianza kutambulika kimuziki mwaka 2001 baada ya kutoa albamu yake ya kwanza inayojulikana kwa jina la Sina muda. Albamu hiyo ilibeba vibao vingine kadhaa kama vile ‘Ninapotaka, Malaika, Niambie na Jakia.
Albamu yake ya pili inajulikana kwa jina la Ni wewe, aliyoitoa mwaka 2006 ikiwa na vibao kama Blessing from Jah, Tamara, Give it to me’ na nyinginezo. Albamu hiyo ilipata mapokeo mazuri, ikiwa ni pamoja na kumuwezesha kutwaa tuzo ya msanii bora wa ragga/dancehall katika tuzo za muziki za Kilimanjaro.

Riyama aibuka na filamu kali



MWIGIZAJI na mtayarishaji maarufu wa filamu nchini, Riyama Ali yupo katika hatua za mwisho za maandalizi ya filamu yake mpya ya Likwata.
Riyama alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, picha za filamu hiyo zinatarajiwa kupigwa ndani ya mji wa Dodoma, ambako ndiyo yanakotarajiwa kuwa makao makuu ya serikali.
Mwigizaji huyo alisema, filamu yake hiyo inatarajiwa kuwakutanisha wasanii kadhaa nyota na itarekodiwa katika vitongoji mbalimbali vya mji huo.
Kwa mujibu wa Riyama, Likwata ni jina la mmoja wa wasanii watakaocheza filamu hiyo, ambayo itakuwa ya kufungua mwaka 2012 kwake.
Mmoja wa washiriki wa filamu hiyo, Swebe Santana alisema baada ya kusoma maelezo yake, alivutiwa nayo na kukubali mara moja kushiriki kuicheza.
“Kaka ukiona msanii anakubali kuja kurekodi filamu mkoani, tambua kuwa filamu hiyo si mchezo,” alisema msanii huyo.
“Likwata ni filamu ya kipekee na ya aina yake, Riyama aliponifuata na kuniomba nishiriki kuicheza, nilimwomba ‘script’ nisome na niliposoma, niligundua kuwa filamu imetulia, ndio maana nipo hapa Dodoma,”alisema Swebe.
Washiriki wengine wa filamu hiyo ni Stara Thomas, Adam Melele, Zuber Mohamed ‘Niva’, Adam Kuambina, Hagy na baadhi ya wasanii kutoka Dodoma.
Riyama, ambaye ni mshindi wa tuzo za Risasi (Risasi Award 2005/2006), ndiye msanii pekee ambaye bado hajapotea katika tasnia ya filamu.
Baadhi ya filamu alizoshiriki kuzicheza ni Fungu la kukosa, Fake Promise, My Darling’, 'Simu ya Kifo’, ‘Darkness Night’, ‘Mwana Pango’, ‘Kolelo’,'Segito’, ‘Miwani ya Maisha’ na ‘Mzee wa Busara.

HEMED: Mademu, wake za watu sasa basi


MSANII nyota wa filamu na muziki wa kizazi kipya nchini, Hemed Suleiman amesema mademu na wake za watu kwake sasa basi.
Hemed alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, ameamua kuachana na mambo hayo kwa lengo la kuuanza mwaka 2012 kivingine.
Alisema uamuzi wake huo umelenga kuondokana na matukio yaliyomchafua na kumtia doa mwaka 2011.
“Wake za watu, mademu za watu hakuna tena 2012,”alisema msanii huyo aliyeshiriki mashindano ya Tusker Project Fame mara mbili nchini Kenya.
“Wamenifanya nigombane na watu wengi mwaka jana. Washkaji zangu wa karibu walinishusha thamani. Lazima nibadilike mwaka 2012,”alisisitiza.
Hemed alisema kwa sasa anajiandaa kupakua albamu yake, itakayokwenda kwa jina la Hedach, ambayo inatarajiwa kuingia sokoni mwezi ujao.
Mbali na kuachia albamu hiyo, amesema amepania kuingia gym kwa lengo la kupunguza unene baada ya mashabiki wake kumlalamikia kwamba amenenepa kupita kiasi.
Hemed ni miongoni mwa wasanii waliotawala vyombo vya habari mwaka jana baada ya kuandamwa na kashfa za kutembea na wake za watu pamoja na wapenzi wa marafiki zake.
Msanii huyo aliwahi kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akidai kuwa, fani ya filamu ndiyo iliyosababisha apapatikiwe na wanawake wengi.
Mmoja wa wasanii wa filamu wa kike, aliyeonekana kumpapatikia waziwazi Hemed ni Jennifer Raymond ‘Penina’, ambaye aliapa lazima afunge ndoa na msanii huyo.
Penina alisema hayo katika mahojiano aliyoyafanya na kituo cha televisheni cha Channel Five, kupitia kipindi cha Friday Night.

Sikuolewa na Aki sababu ya pesa-Nneoma



LAGOS, Nigeria
MKE wa mcheza filamu nyota wa Nigeria, Nneoma Ikedieze amesema hakuolewa na mumewe, Chinedu Idekieze ‘Aki’ kwa sababu ya pesa na umaarufu wake.
Nneoma, ambaye alifunga ndoa na Aki mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema wiki hii mjini hapa kuwa, ameamua kuolewa na mcheza filamu hiyo kwa sababu ya mapenzi aliyonayo kwake.
Mwanadada huyo, ambaye ni mhitimu wa shahada ya mawasiliano ya umma, aliyoipata Chuo Kikuu cha Enugu alisema, alianza kuwa na uhusiano na Aki miaka mitatu iliyopita.
“Tulikutana Lagos. Tulifanyakazi pamoja. Siku zote nilizoea kumuona. Napenda staili ya maisha yake. Hivyo tulianza kuwa marafiki na kuanzia hapo ndipo safari yetu ilipoanza,”alisema Nneoma.
Alisema tangu alipokutana na Aki, aliweza kubaini mara moja kuwa ni aina ya mwanaume anayempenda kutokana na jinsi alivyo.
Alimwelezea Aki kuwa ni mwanaume mwenye akili na mtanashati na pia mwenye mapenzi ya kweli.
Nneona alisema wazazi wake hawakupatwa na mshangao wowote baada ya kuwaeleza kuhusu uamuzi wake wa kutaka kufunga ndoa na Aki.
“Baba yangu aliniambia niendelee na mipango yangu iwapo ndiye chaguo langu,”alisema mwanadada huyo, ambaye anamzidi Aki kwa umbo na urefu.
Nneoma alisema anampenda mno Aki kama alivyo na kusisitiza kuwa, kamwe hawezi kufanya hivyo kwa sababu ya pesa na umaarufu wake.
“Watu wanaweza kusema vyovyote wapendavyo. Ni kauli zisizokuwa na msingi wowote. Nimefunga ndoa na Chinedu Ikedieze, sikuolewa na Aki,”alisisitiza.
Alisema hakuna chochote, ambacho angependa kibadilike kwa Aki baada ya kufunga naye ndoa na kwamba, alivyo anatosha kwake.

FLAVIANA: Sipendi kuitwa mrembo


MWANAMITINDO wa kimataifa wa Tanzania, Flaviana Matata amesema hafurahii kuitwa mrembo kwa sababu kazi yake ni tofauti na fani hiyo.
Flaviana (25), ambaye aliwahi kutwaa taji la Miss Universe Tanzania mwaka 2007, alisema hayo wiki hii kupitia kipindi cha Mkasi kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Channel Five.
Alisema kazi ya uanamitindo imempa heshima na thamani kubwa kwa vile anaweza kwenda popote na kusikilizwa, tofauti na wasichana wengine waliowahi kushiriki mashindano ya urembo.
Mwanadada huyo alisema wanamitindo waliopo sasa Tanzania wanajiharibia wenyewe kutokana na kutokuwa makini na kazi yao na pia kutojiheshimu.
Binti huyo maridhawa aliwaponda wabunifu wa mavazi wa Tanzania kuwa, hawawalipi wanamitindo wao inavyotakiwa, badala yake wamekuwa wakiwatumia kujinufaisha.
“Wabunifu hawawalipi wanamtindo wao ndio sababu mimi binafsi hatuelewani. Wengine wanawalipa wanamitindo sh. 50,000 wakati pesa wanazopata ni nyingi.
“Kuna siku niliwahi kuwaeleza baadhi ya wanamitindo bajeti ya wabunifu wa mavazi, lakini wengine hawakujali, pengine kwa sababu wanapenda kuuza sura,”alisema mwanamitindo huyo mwenye makazi yake nchini Marekani hivi sasa.
Flaviana alisema dawa pekee ya kupambana na wabunifu wa aina hiyo ni kuwagomea, lakini alieleza kusikitishwa kwake kuona kuwa, wanamitindo wa Tanzania hawana umoja.
“Hapa naona cha msingi ni wewe binafsi kuwa na msimamo,”alisema Flaviana, ambaye alishiriki shindano la dunia la Miss Universe mwaka 2007 na kuingia hatua ya 15 bora na kushika nafasi ya sita.
Mwanamitindo huyo alisema wapo baadhi ya wabunifu wa mavazi na wanamitindo wanaomuona anaringa kutokana na mafanikio yake, lakini alisema hivyo sivyo alivyo.
“Hata kama najidai, nina haki ya kufanya hivyo kwa sababu hakuna hata mtu mmoja aliyewekeza pesa zake kwangu, lakini wapo walionipa moyo na kuniunga mkono katika kazi hiyo,”alisema.
Mwanadada huyo mwenye mwili mwembamba mithili ya mtu asiyependa kubugia msosi kwa wingi alisema, mafanikio yake katika fani hiyo yametokana na kujiamini kwake na kufanyakazi kwa bidii.
Alieleza kusikitishwa kwake kuona kuwa, wanawake wengi wa Tanzania wanashindwa kupongezana na kupeana moyo katika mafanikio, badala yake hawapendani.
Alisema kupitia mtandao wa facebook, amekuwa akipata maoni mengi kutoka kwa wanaume kuhusu kazi yake hiyo ya uanamitindo kuliko wanawake wenzake.
Alipoulizwa kuhusu uhusiano wa kimapenzi, Flaviana alisema kwa sasa hana rafiki yoyote wa kiume kwa vile hapendi kukutwa na madhila yaliyompata miaka kadhaa iliyopita.
Alikiri kuwa, wapo wanaume wengi waliowahi kumtongoza, lakini hapendi kuwa na uhusiano wa kimapenzi kwa sasa kwa kuhofia kukutwa na yaliyowahi kumkuta.
Flaviana alisema mwili wake hautokani na kujinyima kula ama kufanya mazoezi gym, bali hayo ni maumbile yake aliyozaliwa nayo.
“Mimi kamwe sijikondeshi, huu ni mwili wangu. Kama ni kula chakula, nakula sana, sijawahi kufanya mazoezi gym hata siku moja,”alisema.
Akizungumzia taasisi yake aliyoianzisha mwanzoni mwa mwaka jana, Flaviana alisema imelenga kutoa misaada ya aina mbalimbali kwa watu wenye matatizo.
Alisema kupitia taasisi yake hiyo, ameamua kuwasomesha watoto 10 wa kike katika shule za sekondari kutokana na wazazi wao kutokuwa na uwezo wa kufanya hivyo.
Flaviana alisema iwapo Mungu ataendelea kumuweka hai, anataka kuona watoto hao wanamaliza shule na kufanyakazi ili waweze kujitegemea kimaisha.
Flaviana alizaliwa Juni 1987. Mama yake alifariki katika ajali ya meli ya MV Bukoba iliyotokea mwaka 1996.
Licha ya picha yake kutumika kutangaza vipodozi vya Sherri Hill, mwanadada huyo aliwahi kushinda tuzo ya mwanamitindo bora wa mwaka 2011 kupitia jarida la Arise la Nigeria.
Picha za mwanadada huyu pia zimewahi kutumika kupamba majarida ya Dazed & Confused, Glass na ID ya Marekani. Pia amewahi kuonyesha mavazi ya wanamitindo maarufu duniani kama vile Vivienne Westwood, Tory Burch, Suno na Louise Gray.

PAPIC: Sina bifu na viongozi wa Yanga


SWALI: Hivi karibuni ulikaririwa ukisema kuwa upo kwenye wakati mgumu kutokana na wewe binafsi na wachezaji wako kukosa mishahara kwa miezi kadhaa. Je, uongozi wa Yanga umeshalitafutia ufumbuzi tatizo hilo? Na nini hatma yako Yanga?
JIBU: Mwanzoni niliamua kuvumilia, lakini baada ya kukabiliana nalo kwa muda mrefu, nimeamua kuweka mambo hadharani kwa wanachama na wadau wote wa Yanga ili waweze kufahamu ukweli wa mambo.
Mbali na kucheleweshewa mshahara, nyumba niliyopangiwa na Yanga ina matatizo makubwa, ikiwa ni pamoja na kukatwa kwa huduma ya maji na umeme.Huduma hizo hazipatikani nyumbani kwangu.
Lakini kwangu hayo naona ni matatizo ya kawaida. Kikubwa ni kwamba nilijisikia vibaya baada ya mimi na wachezaji wangu kukosa mishahara kwa miezi miwili. Hili liliwavunja nguvu sana wachezaji.
Hebu fikiria, mtu mwenye familia anakosa mishahara kwa miezi miwili na mbele yake kuna sikukuu za Krismas na mwaka mpya. Unadhani mtu huyu ataweza kufanyakazi kwa kujituma? Haiwezekani.
Atakachokifanya ni kutafuta mahali, ambako anaweza kwenda kuomba msaada ama kukopa pesa ili aweze kujikimu.
Hivyo napenda kuweka wazi kuwa, sina ugomvi na kiongozi yeyote wa Yanga, isipokuwa nataka kuweka mambo sawa ili huko mbele nisije kulaumiwa mimi kwa kuonekana sifai wakati tatizo ni la uongozi.
SWALI: Baada ya kuzungumza na viongozi wa Yanga, mambo yakoje? Huoni kwamba kauli yako hiyo inaweza kujenga chuki kati yako na viongozi?
JIBU: Hapana, sidhani kama itakuwa hivyo. Kwa sasa nasubiri kikao cha kamati ya utendaji, ambacho kitajadili tatizo lililojitokeza ikiwa ni pamoja na kutafuta suluhisho.
Na kama itatokea viongozi wa Yanga kunichukia, watakuwa wamefanya kosa kwa vile sioni ubaya nilioufanya. Nilichokifanya ni kueleza ukweli wa mambo.
Lakini bado nina imani na viongozi wa Yanga kwamba wataweza kujipanga vizuri na kuwalipa wachezaji mishahara ili waweze kuwa na ari ya kuitumikia timu yao.
SWALI: Binafsi upo tayari kujiuzulu iwapo hali itaendelea kuwa ngumu kwako na kwa wachezaji?
JIBU: Sidhani kama jambo hilo linaweza kutokea kwa sababu Yanga ni klabu kubwa na inao wanachama na wapenzi wengi wenye uwezo wa kuisaidia kifedha.
Ninavyojua ni kwamba, kwa sasa uongozi upo kwenye mikakati ya kutafuta pesa kutoka kwa wafadhili na watu mbalimbali ili uweze kuiweka timu kambini na kuwahudumia wachezaji.
Kwa sasa, sipendi kuzungumzia jambo hilo kwa undani zaidi. Ninachoweza kusema ni kwamba mimi bado ni kocha wa Yanga na nitaendelea kuwepo hapa. Napenda kuiona timu yangu ikifanya vizuri katika michuano ya klabu bingwa Afrika.
SWALI: Unawaeleza nini wana Yanga kuhusu matatizo yaliyojitokeza katika klabu yao.
JIBU: Nawaomba viongozi na wanachama wawe makini katika maandalizi ya michuano hii kwa sababu ni mikubwa na timu tuliyopangwa kuanza nayo (Zamalek) ni ngumu.
Mashindano hayo ni makubwa na yana faida mbili za msingi, ikiwemo kupata pesa nyingi endapo tutafuzu kucheza hatua ya makundi ama kuibuka mabingwa wa Afrika.
Pia baadhi ya wachezaji wanaweza kupata ofa kutoka timu za nje na kununuliwa iwapo wataonyesha viwango vya juu na hivyo klabu kunufaika kipesa.
Kwa maana hiyo, ni vyema tukawekeza nguvu kubwa katika kujiandaa na mashindano hayo ili lengo hilo au ndoto tuliyonayo iweze kutimia.
Lakini pia bado tunakabiliwa na changamoto kubwa ya kutetea ubingwa wetu wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Wasiwasi wangu ni kwamba, iwapo uongozi utazembea kutatua matatizo yaliyopo sasa, ari ya wachezaji itashuka na hivyo tutashindwa kufanya vizuri katika mashindano yanayotukabili.
SWALI: Je, umeshapata taarifa zozote kuhusu timu ya Zamalek ya Misri, ambayo mnatarajiwa kupambana nayo mwezi ujao?
JIBU: Taarifa nilizonazo hadi sasa kuhusu Zamalek ni chache na nimezipata kupitia mitandao mbalimbali. Lakini bado naendelea kuwasiliana na viongozi wa kamati ya mashindano ya Yanga ili tuweze kupata taarifa nyingi zaidi na pia kujipanga kukabiliana nayo.
SWALI: Unazungumziaje michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyoanza wiki hii huko Zanzibar. Je, kuna matumaini yoyote kwa timu yako kufanya vizuri?
JIBU:Nilichopanga ni kuyatumia mashindano hayo kupima uwezo wa wachezaji na pia kujiandaa kwa mzunguko wa pili wa ligi kuu na mechi yetu dhidi ya Zamalek. Hakuna lingine zaidi ya hayo.

PROFESA JAY AKIFANYA MAVITU



MSANII mkongwe wa muziki wa kizazi kipya, Joseph Haule (Profesa Jay- kulia) akicheza na shabiki wake wakati alipotumbuiza katika sherehe za ufunguzi wa ukumbi mpya wa burudani wa Dar Live uliopo Mbagala, Dar es Salaam wiki iliyopita.

Simba chali kwa Jamhuri


MABINGWA watetezi wa Kombe la Mapinduzi, Simba juzi walianza vibaya kutetea kombe hilo baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Jamhuri ya Pemba katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
Kipigo hicho kwa Simba kimekuja siku chache baada ya watani wao wa jadi Yanga, nao kuchapwa bao 1-0 na Mafunzo katika mechi nyingine ya michuani hiyo iliyochezwa kwenye uwanja huo.
Katika pambano hilo lililochezwa kuanzia saa mbili usiku, Simba ilipata nafasi nyingi za kufunga mabao kipindi cha kwanza, lakini zilipotezwa na washambuliaji wake.
Nafasi ya kwanza ilipatikana dakika ya 28 wakati Ramadhani Singano aliposhindwa kuunganisha wavuni krosi ya Gervas Kago kabla ya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati naye kupotesa nafasi dakika ya 36.
Edward Christopher naye alishindwa kuifungia bao Simba dakika ya 45 wakati alipopewa pasi akiwa ndani ya 18, lakini shuti lake lilitoka nje. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote mbili kuongeza kasi ya mchezo na kufanya mashambulizi mengi zaidi. Mashambulizi hayo yalizaa matunda kwa Jamhuri dakika ya 55 baada ya kupata bao la kuongoza kupitia kwa Ali Othman Mmanga.
Bao hilo liliiongezea nguvu Jamhuri, ambayo ilifanikiwa kuongeza bao la pili dakika ya 66 lililofungwa na Bakari Khamis baada ya kutokea kizaazaa kwenye lango la Simba.
Simba ilizinduka dakika ya 74 na kupata bao la kujifariji kupitia kwa Shomari Kapombe baada ya mabeki wa Jamhuri kuzembea kuokoa hatari kwenye lango lao.
Kocha Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic alisema baada ya mchezo huo kuwa, licha ya kufungwa, timu yake ilicheza vizuri, isipokuwa mabeki wake walimwangusha. “Mabeki wangu leo wameniangusha sana, hasa Nyoso (Juma). Sikutegemea kabisa kuwa ataweza kuachia goli ambalo tumefungwa dakika moja tu baada ya yeye kuingia uwanjani,”alisema.
Kocha Mkuu wa Jamhuri, Renatus Mayunga alisema kufanya vizuri kwa timu yake katika mechi hiyo kumewapa moyo wa kutwaa kombe hilo mwaka huu.

Wednesday, January 4, 2012

KUMRADHI



Wapenzi wasomaji wa blogu hii ya Liwazozito, kwa takriban mwezi mmoja sasa sikuweza kuweka habari yoyote mpya kwenye blogu hii kwa sababu nilikuwa likizo ya mwaka kutoka kwa mwajiri wangu. Hivyo niliamua kwenda mapumziko nyumbani Tabora. Niliamua kupumzisha akili na mawazo nyumbani kwetu kwa sababu hiyo ndiyo maana halisi ya kuwa likizo. Unatakiwa upumzishe akili na mawazo kwa kufanya vitu tofauti na vile ulivyovizoea.

Nimerejea rasmi mjini Dar es Salaam, Januari 5, 2012 na nawaahidi kuendelea kuwapa habari mbalimbali kuhusu michezo na burudani pamoja na makala za kusisimua za mastaa wa michezo mbalimbali.

Bila kusahau, nawatakia wasomaji wapenzi wa blogu hii heri ya mwaka mpya na tumuombe Mola wetu aendelee kutuweka hai ili tuendelee kuwasiliana mara kwa mara kupitia blogu hii. Ahsanteni.

Ramoza.