KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, June 11, 2017

TFF YAJITETEA KUHUSU SAKATA LA KUWATELEKEZA VIJANA WA SERENGETI BOYS


Kuna taarifa zimekuwa zikienea na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zikidai kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewatelekeza wachezaji wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.

Wadai kwamba eti hawakulipwa posho na kushutumu viongozi wa juu wa shirikisho kuhusu jambo hilo. Hizi taarifa si za kweli.

Aidha, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linapenda kuwajulisha wazazi na umma kwa ujumla kwamba vijana wetu walilipwa posho zao zote wakiwa kambini Morocco na Cameroon na zile za mashindano ya AFCON nchini Gabon.

Vilevile, Shirikisho linafanya taratibu za kupeleka maombi kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (Football Development Fund FDF) ili kuweza kuwalipa vijana na benchi la ufundi sehemu ya posho zilizokuwa bado hazijakamilishwa wakati wa michuano ya kufuzu kwa AFCON 2017.

Tumeshtushwa na taarifa hizo ambazo tafsiri yake ni kuharibu uhusiano mwema kati ya shirikisho, wazazi na wachezaji ambao wanatarajiwa  kuitumikia timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka  20 maarufu kama Ngorongoro Heroes.

Shirikisho linaendelea kuwatambua vijana wa Serengeti Boys kwani bado ni sehemu ya kikosi cha Ngorongoro Heroes na hivyo ukifika wakati wataitwa kambini kwa ajili ya michezo ya kimataifa ya U-20.

TFF inazidi kuushukuru umma ambao umeendelea kuchangia Mfuko wa FDF ambao kimsingi kazi yake ni kutafuta rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya mpira.

Tunaomba michango iendelee kwani bado tuna changamoto za mashindano mbalimbali kwa timu za wanawake na vijana ikiwemo fainali za wanawake Afrika zitakazofanyika Ghana hapo mwakani kwa timu ya Twiga Stars na AFCON 2019 kwa Serengeti Boys ambayo itakuwa mwenyeji.

Mfuko wa Maendeleo ya Mpira – FDF ulianzishwa kwa lengo la kutafuta rasilimali za maendeleo ya mpira wa miguu hasa kwa wanawake na vijana pamoja na miundombinu ya mchezo huo.

Mfuko huo uko chini ya Mwenyekiti Bw. Tido Mhando anayeongoza Bodi na Mtendaji Mkuu (CEO) ni Bw. Dereck Murusuri anayesimamia sekretarieti.

No comments:

Post a Comment