KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, June 17, 2017

MGOYI ASEMA HATARAJII KUGOMBEA TENA UJUMBE WA KAMATI YA UTENDAJI TFF



Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema na mwenye Ukarimu
 
TFF inaelekea kwenye Uchaguzi wake mwingine  ambao tunategemea kuundwa kwa safu nyingine ya Uongozi itakayoendeleza Gurudumu la Soka nchini.

Binafsi naomba kuchangia muda nanyi kuwasilisha *SHUKRANI* zangu za dhati kabisa kwa Wadau wote wa soka tulioshirikiana kwa njia moja ama nyingine katika kipindi chote cha miaka 13 ambacho nilichaguliwa na kuhudumu kama Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kwenye chaguzi zote tatu nilizoshiriki ambapo kwa mara ya kwanza nikiingia nikiwa Mjumbe mwenye umri mdogo zaidi kuliko wote. Aidha kuomba radhi kwa mapungufu yoyote na yaliyotokana nayo kwa kipindi chote hicho:

Nawashukuru sana wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF katika Chaguzi tatu za TFF kuonyesha Imani na mimi na kunichagua kwa kishindo cha kura nyingi sana kwa nyakati zote hizo.

Naishukuru Kamati ya Utendaji ya TFF inayomaliza muda wake chini ya Rais Jamal Malinzi kwa ushirikiano uliotukuka na nitawakumbuka sana kwa mengi mchanganyiko.

Namshkuru binafsi Leodegar Chilla Tenga aliyenijenga kuwa Kiongozi imara wa Mpira.

Nawashukuru ma-Rais wote wawili niliofanya nao kazi (Tenga na Malinzi) makamu wao na Kamati zao za Utendaji kwa kuniamini kwa nyakati tofauti kunifanya kuwa msimamizi wa shughuli kadhaa miongoni mwa shughuli za TFF.

Navishukuru vyombo vya habari na wanahabari kwa ushirikiano wakati wote.

Naishukuru klabu mashuhuri, Wana Kinyamtula, Never say Die, The Uncolonized, Watoto wa Jiji,  *Ashanti United* niliyoingoza kama Meneja wa timu mpaka Rais wake kwa zaidi ya miaka 20 kwa kunisaidia sana kunijenga kiUongozi na kuniongezea Uthubutu.

Nawashkuru wadau wa Mpira wa Kigoma kwa kuniamini na kunifanya kuwa sehemu ya Uongozi wa Mpira.

Nawashukuru Vilabu vyote vya VPL, FDL, SDL na RCL kwa ushirikiano navyo kwa nyakati tofauti tofauti.

Nawashkuru wafanyakati wote wa TFF na timu za Taifa nilioshirikiana nao kwa nyakati tofauti.

Naishukuru sana Serikali na watendaji wa serikali kwa ushirikiano wakati wote.

Nawashkuru wadhamini na watendaji wa wadhamini wa TFF niliofanya nao kazi kwa nyakati tofauti.

Shukrani zangu zinatokana na yaliyopita na bado naendelea kuamini nitaendelea kushirikiana na nyanja zote kama sehemu ya familia ya Mpira wa Miguu.

Najisikia Fahari sana kuwa sehemu ya Ujenzi wa TFF katika mifumo thabiti na kuwa sehemu ya Usimamizi wa Mafanikio ya Mabadiliko Chanya ya Shuguli za TFF  bila ya kujali na kuthamini Changamoto za Utii na Uendeshaji zinazosababishwa na kutokana nazo.

Naomba kwa dhati kabisa na nikiendelea kuamini kwenye kuhuishwa na kuendelezwa na kufanywa kwa weledi zaidi kwa mema  yaliyopangwa na kufanywa na TFF kwa vipindi vyote nilivyokuwepo na wakati mwingine ikiwemo Ulinzi kwa Mifumo na Misingi ya kiTaasisi iliyowekwa,  Matumizi sahihi ya Vyombo vya TFF, Uthubutu na Mafanikio kwa Uendelezaji wa Soka la Vijana na Wanawake, Muundo wa Uendeshaji wa Mashindano yetu na Mafunzo.

Pamoja na kuwa bado nina nguvu uwezo na sifa za kuendelea kugombea, lakini pia nimeamini ni wakati wa kutoa nafasi pana zaidi kwa wengine kugombea na kuwa badala yangu na heshima kwa fikra nyinginezo. Na ninaondoka nikiwa mjumbe wa muda mrefu zaidi ya wote kwenye Kamati ya Utendaji inayokamilisha kipindi cha kikatiba na kwa dhati kabisa naamini kwenye kutoa nafasi kwa wengine.

Nawaomba radhi wale wote ambao wangependa au kutarajia ningekuwa miongoni au wakiendelea kuamini kuwa nilistahili kuwa sehemu ya wagombea.. nawashukuru kwa imani yao kwangu na bado nipo nao pamoja, pamoja na wale ambao hawaamini hivyo kama sehemu ya familia ya Mpira wa Miguu Tanzania na kwingineko.

Nawatakia kila la kheri wagombea wote na kwa nafasi na uzoefu wangu najishawishi kuamini kwamba wagombea wote watakuwa wamejipima vya kutosha na kuzihakiki dhamira zao, wamejiridhisha na wanavyoijua TFF, ukubwa wake na shughuli zake, wamefuatilia na kutambua vema mahitaji ya mpira wetu, wametathmini changamoto, madhaifu na makusudi ya kiuongozi na wapo tayari kwa mabadiliko, wametambua maeneo TFF inayofeli au hayajafanywa vema zaidi na wanaamini kwenye kuwa sehemu ya ufumbuzi, wamezikataza nafsi zao kufuata matamanio ya mapenzi ya timu zao, wanafahamu nguzo kuu za mpira wa miguu na changamoto zinazozikabili na namna ya kuzitatua, utayari wao kujitolea kwa hali na mali, kuheshimu miiko ya kiUongozi na kuimarisha nidhamu na Uadilifu.

Nimesukumwa kutoa Ushauri wangu huu kwa kuendelea kuathiriwa na kutoamini sana kwenye Utekelezaji na Udhibiti wa  kimfumo wa kupatikana kwa Viongozi wa Mpira hasa katika ngazi za juu kama hizi zinazokwenda kugombewa.

Kila la kheri Wagombea.
Ramadhani Kareem
Nawashukuru sana.
Ahmed Iddi Mgoyi
Mjumbe Kamati ya Utendaji TFF (Kigoma na Tabora 2004-2017)
13 Juni 2017.

No comments:

Post a Comment