Na Mwandishi Wetu
KWA umri, msanii Mohamed Ngwenje, maarufu kwa jina la
Mo Flavour, bado ni mdogo. Ndio kwanza amefikisha umri wa miaka 19, ikiwa ni miaka michache baada ya
kumaliza elimu ya sekondari katika shule ya Uwanja wa Taifa, iliyoko mkoani
Morogoro.
Pamoja na umri wake huo mdogo na pia kuwa na miaka
michache tangu alipojitosa katika fani ya muziki wa kizazi kipya, msanii huyo
ameshafanya mambo makubwa mawili.
Kwanza amesharekodi nyimbo mbili, Usibeti aliouimba
peke yake na Kusudi, ambao ameuimba kwa kushirikiana na wanamuziki nyota wawili
nchini, Jose Mara na Khalid Chuma ‘Chokoraa’.
Wimbo wake wa Usibeti ndio uliomtambulisha katika anga
za muziki huo wa kizazi kipya na ndio uliomwezesha kukutana na Jose Mara na
Chokoraa na hatimaye kukubali kurekodi naye wimbo wa Kusudi.
Tayari Mo Flavour ameshaurekodi wimbo wa Usibeti kwenye
video na audio na kwa sasa anafanya mipango ya kurekodi video ya wimbo wa
Kusudi, baada ya kukamilisha kazi ya kurekodi audio.
Mo Flavour amerekodi nyimbo hizo kwenye studio za Moro
Town Records ya Morogoro na Amoroso Sound ya Dar es Salaam, ambayo ilitumika
kuchanganya ala za muziki kitaalamu zaidi.
Kwa mujibu wa msanii huyo chipukizi, alifanikiwa
kurekodi nyimbo hizo kwa udhamini wa baba yake mzazi, Ngwenje Mohamed, ambaye
pia amekuwa akimtumia kama meneja wake.
“Kwa sasa baba ndiye kila kitu kwangu katika masuala ya
muziki, lakini lengo langu kubwa huko mbele ni kuwa na meneja wa uhakika kwa
ajili ya kusimamia kazi zangu,”alisema Mo Flavour, alipozungumza na Uhuru, hivi
karibuni mjini Dar es Salaam.
Msanii huyo, ambaye kwa sasa anachukua masomo ya
kompyuta katika Chuo cha Royal, kilichoko Ubungo, Dar es Salaam, alisema
anamshukuru Mungu kwamba, nyimbo zake zote mbili zimepokelewa vizuri na
mashabiki wa muziki wa kizazi kipya.
Alisema kupokelewa vizuri kwa nyimbo hizo,
kulijidhihiridha wakati wa utambulisho wa kibao chake cha kwanza cha Usibeti,
alioufanya mwaka jana, kwenye ukumbi wa Jahazi Garden, mjini Morogoro.
Kwa mujibu wa Mo Flavour, alifanya onyesho hilo la
uzinduzi kwa udhamini wa baba yake na kuongeza kuwa, lilihudhuriwa na mashabiki
lukuki.
“Hata mapato niliyoyapata yalikuwa mazuri na ndiyo
yaliyoniwezesha kupata fedha za kurekodi wimbo wangu uliofuata wa Kusudi,”alisema
Mo Flavour.
Mbali na mafanikio hayo, alisema amekuwa akipata
mialiko mingi ya kufanya maonyesho mbalimbali ya muziki huo kwa kushirikiana na
baadhi ya wasanii maarufu nchini.
“Jambo la kufurahisha ni kwamba, nimeanza kupokea
mialiko kutoka hata katika nchi jirani za Uganda na Kenya. Hii inadhihirisha
kwamba, kazi zangu zinakubalika,”alisema.
Akizungumzia hali ya muziki huo nchini, Mo Flavour
alisema ni nzuri na ya kuridhisha kutokana na mafanikio yaliyofikiwa na wasanii
wengi wa fani hiyo.
Hata hivyo, alikiri kuwa kikwazo kikubwa kwa wasanii
wanaochipukia ni kukosa promosheni kwa vile mapromota wanapenda zaidi kuwasaidia
wasanii waliokwishapata umaarufu, badala ya wale wanaochipukia.
“Unaweza kutunga nyimbo nzuri na kali, ikapendwa na
mashabiki, lakini ikakosa mtu wa kuitangaza. Hali hii imekuwa ikisababisha
wasanii wengi wanaochipukia kukata tamaa mapema,”alisema.
Msanii huyo amesema anamshukuru Mungu kwa kupata
uungwaji mkono wa kiwango kikubwa kila alipotembelea vituo mbalimbali vya redio
na televisheni nchini. Alisema hali hiyo imekuwa ikimtia moyo na kumfanya
ajitume zaidi.
“Japokuwa kumekuwa na malalamiko ya watangazaji wa
redio na televisheni kubania kazi za wasanii, kwangu mimi hali ni tofauti. Kila
ninapopeleka kazi zangu kwenye vituo vya redio na televisheni, zimekuwa
zikikubalika. Sikuwahi kuombwa rushwa,”alisema.
Msanii huyo pia amesema anaunga mkono uwepo wa sheria
ya hatimiliki nchini, ambayo inamwezesha msanii kulipwa kila kazi yake
inapotumika kwenye vituo vya redio na televisheni.
Amesema kazi ya muziki ni biashara, vivyo hivyo vituo
vya redio na televisheni navyo vimekuwa vikifanya biashara, hivyo vinapotumia
kazi za wasanii, havina budi kuwalipa.
Mo Flavour amesema binafsi anavutiwa na wasanii wote wa
kizazi kipya nchini kwa kuwa kila mmoja anajitahidi kufanya vizuri ili aweze
kupata mafanikio.
Ameyataja malengo yake katika siku zijazo kuwa ni
pamoja na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia muziki huo na pia kuwa
mwanamuziki wa kimataifa.
Amewataka wasanii wa muziki huo wawe makini katika kazi
yao, hasa wanapobahatika kupata udhamini kutoka kwenye kampuni na watu binafsi.
“Nawashauri wasanii wenzangu unapopata msaada wa
udhamini, jitume. Huwezi kuendelea kusaidiwa kama hufanyi jambo la
maana,”alisema.
Pia, aliwataka wasanii wa muziki huo kuacha tabia ya
kujikweza na kujiona wapo matawi ya juu pale wanapoanza kupata mafanikio.
Alisema kufanya hivyo kunawakera mashabiki na kutasababisha waporomoke mapema
kimuziki.
0000000
No comments:
Post a Comment