RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Katibu Mkuu wake, Celestine Mwesigwa, wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Viongozi hao wawili walikamatwa juzi kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi, yakihusisha ubadhirifu wa mamilioni ya shirikisho hilo.
Malinzi na Mwesigwa hadi leo hii asubuhi bado walikuwa wakishikiliwa na taasisi hiyo na huenda Malinzi akashindwa kuhudhuria usaili wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa TFF.
TAKUKURU haikuwa tayari kusema lolote jana kuhusu kuwashikilia viongozi hao wawili na lini itawaachia.
Wakati huo huo, Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ nao wanashikiliwa na TAKUKURU kwa ajili ya uchunguzi juu ya tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutokana na mchezaji Emmanuel Okwi.
Habari za uhakika kutoka kwa taasisi hiyo zimeeleza kuwa, viongozi hao wakuu wa klabu hiyo walikamatwa jana kwa nyakati tofauti kwa ajili ya mahojiano juu ya tuhuma hizo.
Kwa mujibu wa habari hizo, imedaiwa kuwa kulifanyika udanganyifu katika mauzo ya Okwi kwenda klabu ya Esperance ya Tunisia.
Imeelezwa kuwa Dola 300,000, ambazo ni zaidi ya sh. milioni 600, zilizotajwa kuwa Simba ililipwa kutokana na mauzo ya mchezaji huyo, sicho ilicholipwa.
No comments:
Post a Comment