'
Sunday, January 18, 2015
MICHUANO YA KOMBE LA TAIFA WANAWAKE YAINGIA RAUNDI YA PILI
Michuano ya Kombe la Taifa kwa Wanawake inaingia raundi ya pili kesho (Januari 17 mwaka
huu) kwa mechi za kwanza za raundi hiyo zitakazochezwa katika miji ya Bukoba, Arusha,
Mlandizi, Dar es Salaam na Katavi.
Jijini Dar es Salaam kutakuwa na mechi mbili ambapo mkoa wa kisoka wa Ilala utacheza na
Mtwara kwenye Uwanja wa Karume, wakati Uwanja wa Chuo cha Bandari uliopo Tandika
utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Temeke na Dodoma.
Mechi nyingine za michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Proin zitakuwa kati ya Kagera
na Mwanza itakayochezwa mjini Bukoba, Arusha na Tanga (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri
Abeid), Pwani na Kinondoni (Uwanja Mabatini, Mlandizi), na Katavi na Mbeya zitakazoonesha kazi
kwenye Uwanja wa Azimio.
Nazo Ruvuma na Iringa zitacheza Januari 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa Majimaji. Mechi
hiyo itachezwa tarehe hiyo ili kusubiri matokeo ya mechi ya marudiano kati ya Shinyanga na
Simiyu.
Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
ilikutana jana (Januari 15 mwaka huu) kupitia ripoti ya mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza
kati ya Shinyanga na Simiyu ambayo ilivunjwa na mwamuzi katika daika ya 70.
Baada ya kupitia ripoti, Kamati imebaini kuwa licha ya vurugu alizofanyiwa mwamuzi, bado
mechi hiyo ingeweza kuendelea kwa kuchezeshwa na mwamuzi wa akiba kwa vile usalama
ulikuwepo baada ya yeye kupigwa.
Pia Kamati imeagiza Katiba wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Simiyu, Emmanuel Sologo
aliyeripotiwa kumpiga mwamuzi suala lake lipelekwe kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa
hatua zaidi, wakati Kocha wa Simiyu, Emmanuel Babu ambaye naye alishiriki kumpiga mwamuzi
amesimamishwa wakati akisubiri kuchukua hatua zaidi.
Kamishna wa mechi hiyo Idd Mbwana, na mwamuzi Joseph Pombe wamefungiwa kwa miaka
miwili.
Mechi kati ya Shinyanga na Simiyu itamaliziwa dakika kumi zilizobaki kesho (Januari 17 mwaka
huu) mjini Shinyanga. Kila chama cha mkoa kitabeba gharama zake katika uendeshaji wa mechi
hiyo ambayo mwenyeji ni Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA).
Timu itakayosonga mbele baada ya mechi hiyo itacheza mechi ya kwanza ya raundi ya pili
ugenini Januari 19 mwaka huu dhidi ya Kigoma. Mechi za marudiano za raundi ya pili
zitachezwa kati ya Januari 21 na 22 mwaka huu.
Hatua ya robo fainali hadi fainali ambayo mechi zake zitachezewa jijini Dar es Salaam itaanza
Januari 26 mwaka huu. Fainali itachezwa Februari Mosi mwaka huu.
Vilevile Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya TFF imemfungia kwa miaka miwili Kaimu
Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA), Gabriel Gunda kwa
kushindwa kuingiza timu yake uwanjani kwenye mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza dhidi
ya Dodoma iliyokuwa ichezwe kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment