'
Thursday, January 1, 2015
KOCHA MPYA SIMBA ATUA DAR, WACHEZAJI WANANE WAGOMA KWENDA ZANZIBAR
KOCHA Mkuu mpya wa timu ya soka ya Simba, Goran Kopinovic, ametia saini mkataba wa kuinoa Simba kwa miaka miwili.
Goran, raia wa Serbia, alimwaga wino jana baada ya kufanya mazungumzo marefu na viongozi wa Simba.
Kocha huyo aliwasili nchini jana asubuhi na kufikia kwenye hoteli ya Double Tree iliyoko Masaki mjini Dar es Salaam.
Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, kocha huyo anatarajiwa kwenda Zanzibar leo kujiunga na timu hiyo, inayoshiriki kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Simba imepangwa kufungua dimba la michuano hiyo leo usiku kwa kumenyana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili nchini jana, Goran alisema amekuja nchini kufanyakazi na anaamini atapata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi wa klabu hiyo.
Goran anachukua nafasi ya kocha wa zamani wa Simba, Patrick Phiri, ambaye alitupiwa virago mwanzoni mwa wiki hii kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Wakati huo huo, kikosi cha Simba kimeondoka mjini Dar es Salaam leo kwenda Zanzibar bila ya wachezaji wake wanane nyota.
Wachezaji hao, wakiwemo Waganda watano, wamegoma kujiunga na timu hiyo kutokana na kutolipwa fedha zao za usajili.
Wachezaji wa Uganda waliomo kwenye mgomo huo ni Emmanuel Okwi, Joseph Owino, Dan Ssenkuruma, Simon Ssenkuruma na Juuko Murshid.
Kwa upande wa wachezaji wazalendo, ni kipa Ivo Mapunda, aliyekwenda Mbeya kwenye msiba wa mama yake, Shabani Kisiga na Jonas Mkude.
Kocha msaidizi wa timu hiyo, Selemani Matola, amesema hana taarifa za kutoweka kwa wachezaji hao. Amesema mchezaji pekee, aliyepata taarifa zake ni Mapunda.
Matola amekiri kuwa, anakwenda Zanzibar akiwa na wachezaji wachache, lakini aliahidi kuiongoza vyema timu hiyo kufanya vizuri katika michuano hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment