KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, January 13, 2015

MTEMVU AIAHIDI VYOMBO VIPYA VYA MUZIKI SIKINDE


MBUNGE wa Jimbo la Temeke (CCM), Abbas Mtemvu (kushoto), akizungumza na wanamuziki wa bendi ya Mlimani Park Orchestra 'Sikinde' wakati wa hafla ya kuwapongeza wenyeviti wapya wa serikali za mitaa, iliyofanyika juzi kwenye ukumbi wa Kata ya 15, Temeke, Dar es Salaam. Wengine pichani ni  wanamuziki wa bendi hiyo, Hassan Bitchuka, Mbaraka Othman na Ramadhani Mapesa. (Picha na Emmanuel Ndege).

Na Emmanuel Ndege

MBUNGE wa Jimbo la Temeke (CCM), Abbas Mtemvu, ameahidi kuinunulia vyombo vipya vya muziki bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra 'Sikinde'.

Mtemvu alitoa ahadi hiyo juzi wakati wa sherehe za kuwapongeza wenyeviti wapya wa serikali za mitaa kutoka CCM waliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Desemba 14, mwaka huu.

Katika sherehe hizo zilizofanyika kwenye ukumbi wa Kata ya 15, Temeke, Dar es Salaam, bendi za Sikinde, Msondo Ngoma na kikundi cha taarab cha Mashauzi Classic vilitoa burudani.

Mtemvu alisema ameamua kuinunulia vyombo vipya bendi hiyo, kutokana na maombi aliyoyapata kutoka kwa wanamuziki wake.

Mbunge huyo aliwahi kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Uchumi na Maendeleo la mkoa wa Dar es Salaam (DDC), lililokuwa likiimiliki bendi hiyo, ambapo pia aliwahi kuinunulia vyombo vya muziki.

"Viongozi wa Sikinde waliwahi kuniomba niwanunulie vyombo vipya na nilikuwa tayari kufanya hivyo, lakini ufuatiliaji wao haukuwa mzuri. Kwa vile mmewasilisha tena ombi hilo leo (juzi), naahidi kufanya hivyo hivi karibuni,"alisema Mtemvu huku akishangiliwa na wanamuziki wa bendi hiyo.

Kwa mujibu wa Mtemvu, atatekeleza ahadi hiyo wiki ijayo na aliwataka wanamuziki wa bendi hiyo kujituma zaidi ili waweze kupata mafanikio makubwa zaidi.

Kiongozi wa bendi hiyo, Abdalla Hemba, alimshukuru Mtemvu kwa kulikubali ombi lao na kuahidi kuvitumia vyombo hivyo kuongeza ufanisi zaidi ili waweze kufika matawi ya juu zaidi.

Wakati huo huo, bendi ya Mlimani Park, imeamua kuwarejesha kundini wanamuziki wake wa zamani, mpiga solo Gasper Kanuti na mwimbaji Eddo Sanga.

Hemba alisema juzi kuwa, Kanuti alitambulishwa rasmi mwishoni mwa wiki iliyopita wakati Eddo atatambulishwa Jumapili ijayo.

No comments:

Post a Comment