KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, November 2, 2014

YANGA, AZAM ZAPATA VIPIGO LIGI KUU, SARE YAZIDI KUIANDAMA SIMBA




MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Azam jana walikwaa tena kisiki baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Ndanda FC katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Nangwande mjini Mtwara.


Kipigo hicho kilikuwa cha pili kwa Azam baada ya wiki iliyopita kuchapwa bao 1-0 na JKT Ruvu kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Chamazi mjini Dar es Salaam.

Bao pekee na la ushindi la Ndanda lilifungwa na Jacob Massawe dakika ya 15 na kuifanya ipate ushindi wake wa pili tangu ligi hiyo ilipoanza.

Washindi wa pili wa mwaka jana, Yanga nao walionja joto ya jiwe baada ya kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Bao pekee na la ushindi la Kagera Sugar lilifungwa na Paul Ngwai dakika ya 54 alipounganisha kwa kichwa krosi kutoka pembeni ya uwanja.

Katika mchezo huo, beki Nadir Haroub wa Yanga alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kichwa mchezaji mmoja wa Kagera Sugar.

Timu kongwe ya Simba nayo iliendelea kusuasua katika ligi hiyo baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa beki wake, Joseph Owino baada ya kuunganishwa wavuni kwa kichwa krosi kutoka kwa Emmanuel Okwi.

Mussa Hassan Mgosi aliisawazishia Mtibwa dakika ya 56 na kufuta ndoto za Simba za kutoka uwanjani na ushindi wa kwanza katika ligi hiyo.

Katika mechi hiyo, kipa Manyika Peter wa Simba alionyesha ushujaa wa aina yake baada ya kupangua penalti ya David Luhende baada ya beki Hassan Isihaka kumwangusha Ame Ali wa Mtibwa ndani ya eneo la hatari.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Coastal Union iliichapa Ruvu Shooting bao 1-0, Polisi Moro iliilambisha JKT Ruvu mabao 2-1.

No comments:

Post a Comment