'
Sunday, November 9, 2014
SIMBA YAFUTA MWIKO WA SARE, YAICHAPA RUVU SHOOTING 1-0
BAO lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi, jana liliiwezesha Simba kupata ushindi wake wa kwanza katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0.
Okwi alifunga bao hilo dakika ya 78 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Rashid Abdalla wa Ruvu Shooting, kutokana na shuti kali la Elias Maguri.
Ushindi huo uliwapa ahueni kubwa mashabiki wa Simba baada ya kuishuhudia timu yao ikitoka sare mechi sita mfululizo na hivyo kuhatarisha kibarua cha Kocha wao, Patrick Phiri kutoka Zambia.
Sare hizo pia zilisababisha uongozi wa Simba kuwasimamisha wachezaji wake nyota watatu, Amri Kiemba, Haruna Chanongo na Shaaban Kisiga kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.
Kwa matokeo hayo, Simba sasa inazo pointi tisa baada ya kucheza mechi saba na imechupa hadi nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa nyumba ya Yanga kwa tofauti ya pointi tatu.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilipata nafasi kadhaa nzuri za kufunga mabao, lakini umaliziaji mbovu wa washambuliaji wake ulikuwa kikwazo.
Kuingia kwa Elias Maguli katika kipindi cha pili, aliyechukua nafasi ya Saidi Ndemla, kuliiongezea uhai safu ya ushambuliaji ya Simba, ambayo ilifanya mashambulizi kadhaa kwenye lango la Ruvu Shooting.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Mtibwa Sugar ilitoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Manungu ulioko Turiani mjini Morogoro.
Awali, mechi hiyo ilichezwa juzi kwenye uwanja huo, lakini ililazimika kuahirishwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha uwanjani. Hadi mechi ilipovunjika, Mtibwa ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment