KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, November 9, 2014

AMIGOLAS WA TWANGA PEPETA AFARIKI DUNIA




MWIMBAJI nyota wa bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta Internationa, Hamisi Kayumbu 'Amigolas', amefariki dunia.


Amigolas, alifariki dunia juzi saa 5.30 usiku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alikokuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo.

Mwanamuziki huyo alikuwa kiongozi mpya wa bendi ya Ruvu Stars baada ya kutamba kwa muda mrefu na Twanga Pepeta, ambapo pia aliwahi kuwa kiongozi.

Amigolas atakumbukwa kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika bendi ya Twanga Pepeta, ambapo alikuwa mmoja wa waimbaji wake mahiri, akishirikiana na Ally Choki, Luiza Mbutu, Khalid Chokoraa, Ramadhani Masanja 'Banza Stone'.
Akizungumzia kifo cha mwanamuziki huyo, Mkurugenzi wa Kampuni ya African Stars Entertainment, Asha Baraka, alisema marehemu Amigolas alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo kwa miaka minne iliyopita.
Asha alisema tasnia ya muziki imempoteza mtu muhimu, ambaye alisaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa wasanii wanaong'ara katika bendi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Asha, Amigolas alijiunga na Twanga Pepeta mwaka 1998, wakati huo ikiwa inafanya maonyesho ya wazi kwenye baa kabla ya kuanza kupata umaarufu na kuteka soko la muziki nchini.
Marehemu Amigolas ameacha mke na watoto wanne na anatarajiwa kuzikwa leo kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment