HAIKUWA rahisi kuamini, lakini ukweli ni kwamba mwandishi maarufu wa habari za michezo nchini, Innocent Munyuku, amefariki dunia.
Munyuku alifariki dunia jana alfajiri nyumbani kwake Kimara Kibo Dar es Salaam. Alifariki akiwa usingizini.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia yake, mwili wa marehemu Munyuku unatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda Mazimbu mkoani Morogoro kwa ajili ya mazishi. Mazimbu ndiko anakoishi mama yake mzazi, ambaye ni mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Taarifa za kifo cha Munyuku zilipokelewa kwa mshtuko mkubwa. Wafanyakazi wenzake wa Kampuni ya New Habari, inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Rai, Dimba na Bingwa, hawakuamini masikio yao baada ya kupata taarifa hizo.
Wapo waliozungumza na kuchati naye kwa simu hadi saa nne usiku juzi. Pia aliposti ujumbe wa aina mbalimbali kwenye mtandao wa facebook, ukiwemo ujumbe unaohusu masuala ya dini ya kikristo. Katika ujumbe wake wa mwisho, aliandika 'Usiku mwema'.
Mmoja wa wafanyakazi wenzake, Jimmy Chika, ambaye ni Mhariri wa gazeti la Dimba, anasema alitumiwa ujumbe na Munyuku, akimueleza kwamba amepata fedha alizoomba ofisini hivyo mambo yake yalikuwa safi.
Karibu kila mmoja aliyezungumza ama kuchati na Munyuku juzi, alisimulia kile walichozungumza naye. Zilikuwa simulizi za kuhuzunisha na kusikitisha. Hakuna anayeweza kutabiri ni lini ataondoka hapa duniani. Ni siri kubwa, ambayo imefichwa na Mwenyezi Mungu.
Mwanahabari mkongwe Abubakar Liongo aliandika kwenye mtandao wa facebook jana akisema:
" Japo lazima sote siku tutaipa kisogo dunia hii ya manani, lakini hakika habari za kifo cha comrade Innocent Munyuku, zimenistua sana. Si zaidi ya wiki nikiwa Dodoma, tulikuwa tukichati kupitia FB,tukitaniana kama kawaida yetu. Hakika kifo hakina hodi.Munyuku au Gaitanoama, tulivyokuwa tukiitana, umeondoka mapema ndugu yangu kama walivyoondoka Conrade Dunstan (kiona mbali) na Dan Mwakiteleko (mullah) na kuiachia pengo tasnia ya habari.".
Mwani Nyangasa naye aliandoka: "Ni vigumu kuamini, naona shida kuzungumzia kwa kuwa ni kitu ambacho sikiamini. Eti leo kaka zangu Innocent Munyuku na Baraka Karashani hatunao, wamekufa siku moja. Juzi nilipata taarifa za kuumwa Baraka, jana nikaenda hospitali na dada yangu Grace Hoka kumuangalia, tulitokwa na machozi. Baraka hakuwa na hali nzuri, tukajipa moyo atapona na tukamfariji mkewe kuwa asife moyo, Baraka atakuwa na nguvu, nikaondoka, Leo asubuhi naamshwa na simu eti Innocent amefariki nilipigwa na butwaa."
Kwa upande wake, Charles Mateso, alisimulia jinsi alivyokwenda ofisini kwa Munyuku, akamkosa, wakakutana siku inayofuata, wakazungumza mambo mbalimbali na kupanga kuyatekeleza jana, lakini Mungu hakupenda. Amemchukua Munyuku.
Binafsi nilipata taarifa za kifo cha Munyuku kupitia kwa Grace Hoka, Mhariri wa gazeti la Bingwa. Alinipigia simu saa 1.30, asubuhi na kuzungumza maneno matatu. Alisema: "Kaka Zahor, Munyuku amefariki." Akakata simu huku akiangua kilio.
Sikuamini masikio yangu. Nikakaa na kutafakari kwa sekunde kadhaa. Baada ya muda, nikaamua kupiga namba ya simu ya Munyuku. Ilipokelewa na mwanamke mmoja, ambaye naye alitamka maneno machache. Alisema: "Mwenye simu hii amefariki."
Nikamuuliza: "Amefariki lini?"
Akasema: "Leo alfajiri."
Nikaendelea kumuuliza: "Wewe ni nani?"
Akajibu: "Mimi mpangaji mwenzake."
Baada ya maneno hayo, yule dada alikata simu. Nadhani alichoshwa kupokea simu kutoka kwa watu mbalimbali waliokuwa wakiulizia taarifa za kifo cha mwanahabari huyo.
Nilipata uthibitisho zaidi wa kifo cha Munyuku baada ya kuelezwa na baadhi ya wafanyakazi wenzake kwamba, maofisa wa New Habari walikwenda nyumbani kwake na kuukuta mwili wake ukiwa bado kitandani kama alivyokuwa amelala. Wakauchukua na kuupeleka hospitali, bila shaka kwa lengo la kutaka kujiridhisha kuhusu sababu za kifo chake.
Hivyo ndivyo taarifa za kifo cha Munyuku zilivyoanza kusambaa katika vyombo mbalimbali vya habari. Taarifa zilizopokelewa kwa majonzi makubwa na wanahabari wengi waliomfahamu, hasa kutokana na ucheshi na vituko vyake, achilia mbali utendaji wake mzuri wa kazi.
Nilianza kumfahamu Munyuku tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000. Wakati huo alikuwa akiandikia magazeti mbalimbali. Alipenda kuniita kaka na mimi nilipenda kumwita 'kamanda'. Tuliitana hivyo kila tulipozungumza kwa simu au tulipokutana, hasa katika vikao vya nje ya kazi.
Nilianza kuwa naye karibu mwaka 2006, wakati yeye na swahiba wake mkubwa, Charles Mateso, walipoajiriwa na Kampuni ya Uhuru Publications Ltd, inayochapisha magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani. Kuajiriwa kwao kulilenga kuliendesha gazeti la Burudani.
Walifanyakazi pamoja kwa kipindi kisichopungua miaka miwili. Baada ya muda huo, wote wawili waliamua kuacha kazi kwa pamoja. Sababu za kufanya hivyo walizijua wenyewe.
Kwa uchapakazi, Munyuku alikuwa na sifa za aina yake. Hakutaka utani katika kazi. Na kila alipokuwa 'bize', hakupenda usumbufu kutoka kwa mtu yeyote. Akiona unamsumbua, atakwambia 'kamanda niache kwanza nimalize kazi, tutaongea baadae.'
Munyuku pia alikuwa mbunifu mzuri. Nakumbuka yeye na Mateso walifanikiwa kubadili sura ya gazeti la Burudani hadi likawa na mvuto wa aina yake. Walianzisha 'kolamu' nyingi zenye kusisimua na ambazo zinapendwa na vijana. Waliliweka gazeti hilo kwenye matawi ya juu.
Hatimaye Munyuku ametutoka. Ametangulia kwenda kule ambako, sisi viumbe wote wa Mwenyezi Mungu lazima tutakwenda. Maana yamenena maandiko matakatifu kwamba, 'Kila chenye roho, lazima kitaonja mauti.'
Buriani Innocent Munyuku. Tunamuomba Mwenyezi Mungu akupe mapumziko mema.
Wakati huo huo, habari zingine za kusikitisha zilizopatikana jana jioni zimeeleza kuwa, mwanahabari mwingine maarufu wa michezo, Baraka Karashani, amefariki dunia.
Baraka alifariki jana mchana kwenye hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa kwa siku kadhaa.
No comments:
Post a Comment