Na Mwandishi Wetu, Harare
TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars imesonga mbele katika michuano ya awali ya kuwania ubingwa wa Afrika baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Zimbabwe.
Katika mechi hiyo ya marudiano iliyochezwa mjini Harare, mabao ya Taifa Stars yalifungwa na beki Nadir Haroub 'Cannavaro' na mshambuliaji Thomas Ulimwengu.
Sare hiyo imeiwezesha Stars kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2, kufuatia ushindi wa bao 1-0 ilioupata wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Zimbabwe ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya tatu kabla ya Cannavaro kusawazisha dakikaya 21 baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Simon Msuva. Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko.
Kipa Deogratius Munish 'Dida' aliibuka shujaa wa Taifa Stars, kufuatia kuokoa mipira mingi ya hatari iliyopigwa kwenye lango la timu yake, ikiwa ni pamoja na kuwavaa washambuliaji wa Zimbabwe bila woga.
Taifa Stars ilipata bao la pili dakika ya 46 kupitia kwa Ulimwengu, aliyetumia vyema uzembe wa mabeki wa Zimbabwe waliojisahau.
Zimbabwe ilisawazisha dakika ya 54 baada ya kufanya shambulizi la kushtukiza kwenye lango la Taifa Stars. Bao hilo lilifungwa na Denver Mukamba.
Katika kipindi hicho cha pili, Kocha Mart Nooij alifanya mabadiliko kwa kuwaingiza Mrisho Ngassa, Frank Domayo na Said Mourad kuchukua nafasi za Simon Msuva, Amri Kiemba na Thomas Ulimwengu.
Taifa Stars: Deo Munishi ‘Dida’, Shomary Kapombe, Oscar Joshua, Nadir Haroub
‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mwinyi Kazimoto, Simon Msuva/Said Mourad dk78,
Amri Kiemba/Frank Domayo dk62, John Bocco, Thomas Ulimwengu/Mrisho Ngassa
dk88 na Erasto Nyoni.
No comments:
Post a Comment