KLABU ya Simba itafanya uchaguzi wake mkuu kesho baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali maombi ya wanachama watatu wa klabu hiyo kutaka uchaguzi huo usimamishwe.
Wanachama hao wa Simba, Josephat Waryoba, Saidi Ally Monero na Hassan Hassan kwa niaba ya wenzao 60, waliwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakiomba amri ya zuio la muda la uchaguzi huo.
Walikuwa wakiiomba mahakama hiyo iwape kibali cha kufungua kesi ya uwakilishi na pia itoe amri ya zuio la uchaguzi huo.
Hata hivyo, Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa jana na Jaji Agustine Mwarija baada ya kusikiliza hoja za pande zote, yaani watoa maombi na wajibu maombi, ilikubaliana kufungua kesi ya uwakilishi, lakini ikatupilia mbali maombi ya zuio la uchaguzi.
Jaji Mwarija alifikia uamuzi wa kutupilia mbali maombi ya wanachama hao baada ya kubaini kuwa yamewasilishwa mahakamani isivyo sahihi kisheria, kutokana na kutokuwepo kesi ya msingi mahakamani.
Alisema kwa mujibu wa kanuni ya 1 (8) ya mahakama hiyo ya uendeshaji wa mashauri ya jinai, kesi inayowahusisha watu wengi wenye masilahi yanayofanana, inaweza kufunguliwa na mmoja wao au baadhi yao kwa niaba ya wengine baada ya kupata kibaku cha mahakama.
Kuhusu maombi ya zuio la muda, Jaji Mwarija alisiea mahakama inaweza kutoa zuio pale tu panapokuwepo na kesi ya msingi iliyofunguliwa mahakamani, lakini kesi hiyo haipo.
No comments:
Post a Comment